Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Jumapili ya XIV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Utume wa waamini walei na Utukufu wa Fumbo la Msalaba! Tafakari ya Jumapili ya XIV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Utume wa waamini walei na Utukufu wa Fumbo la Msalaba!  (ANSA)

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XIV: Utukufu wa Fumbo la Msalaba!

Mama Kanisa katika dominika ya XIV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa anatukumbusha kuwa sisi sote tumeitwa kuihuburi Injili kwa kuishi Ukristo wetu vyema sio kwa sheria za maumbile bali kwa kuwa viumbe vipya ndani ya Kristo na kuona fahari juu ya Msalaba wa Yesu Kristo ambao kwao tumekombolewa. Waamini wanatumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 14 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Mama Kanisa katika dominika hii anatukumbusha kuwa sisi sote tumeitwa kuihuburi Injili kwa kuishi Ukristo wetu vyema sio kwa sheria za maumbile bali kwa kuwa viumbe vipya ndani ya Kristo na kuona fahari juu ya Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao kwao tumekombolewa. Katika somo la kwanza kutoka sura ya mwisho ya kitabu cha nabii Isaya linatupa matumaini na faraja ya kushangilia na kufurahi kuwa Mungu atasimamisha ufalme mpya wenye haki kwa wale wanaompenda na wanaomcha. Hii ni kusema kwamba wenye haki watashiriki baraka za milele katika mbingu mpya na nchi mpya yaani uzima wa milele.

Utabiri huu wa nabii Isaya unatimilika katika Kristo kwa kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Kazi imebaki kwetu kulisha na kuishi maisha ya kikristo. Wakati wa enzi za mitume jumuiya zilizoipokea Injili zilikuwa na hamasa kubwa ziliikumbatia Imani. Furaha iliijaza mioyo yao. Walikuwa wachache kwa idadi, lakini waliishi imani hiyo kiaminifu na kwa furaha kubwa. Furaha hiyo iliongezeka kadiri idadi yao ilivyoongezeka kwani wengi walipendezwa na maisha yao wakaamini na kubatizwa. Lakini taratibu, ile hamasa ilianza kufifia, ugomvi na mpasuko kati yao ukaanza kutokea, wengi wakaanza kurudi nyuma katika imani yao. Wakristo katika Kanisa la Galatia nao walikata tamaa na kuanza kurudi nyuma katika imani. Katika mazingira hayo Paulo katika somo la pili ambalo ni hitimisho la barua yake kali aliyowaandikia Wagalatia hata kuumbia, ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaloga? Akiwataka waujue ukweli na wasipotoshwe na mafundisho ya uongo ya baadhi ya walimu wa uongo na Wayahudi wapotoshaji.

Mtume Paulo alikuwa amewahubiria watu wa Galatia katika safari yake ya kwanza ya kueneza Injili (Mdo 13:14-14:23). Baada ya yeye kuondoka, kikundi cha Wayahudi walioamini walifika, wakaanza kusisitiza kwamba ni lazima watu wa Mataifa walioamini watimize kwanza sheria za Musa ili wapate kuokoka. Paulo anaandika kupinga mafundisho hayo kwa kuonyesha jinsi ambavyo Abrahamu, ambaye aliishi miaka 400 kabla ya sheria ya Musa kutolewa, alivyookolewa kwa imani. Anaonyesha kwamba, kama vile ambavyo sheria haiwezi kumwokoa mtu, hakuna mtu anayeweza kuwa mkamilifu kwa kujitahidi kwa uwezo wake mwenyewe katika kutimiza sheria. Paulo anakazia hoja hiyo kwa kuthibitisha jinsi ambavyo yeye mwenyewe ni mtume wa Kristo na kwa kutoa mafundisho kuhusu jinsi mkristo anavyopaswa kuishi. Paulo anatetea kwa bidii kweli ya Injili ambayo kiini chake ni kwamba, Mtu anaokolewa kwa neema ya Mungu kwa kumwamini Kristo.

Mtu anayeongeza chochote katika ukweli huu anapotosha kweli ya Mungu. Tunahesabiwa haki mbele za Mungu kwa njia ya imani na tunakuwa watoto wa Mungu kwa imani. Kwa kuwa Kristo ametuweka huru, basi tusimruhusu mtu yeyote aturudishe kwenye mawazo ya kudhania kuwa matendo ya sheria yanatosha kutupatia wokovu. Kama watu waliookolewa kwa neema, tuna wajibu wa kuishi maisha yanayolingana na imani yetu. Ndiyo maana anasema, mimi hasha sioni fahari juu ya kitu cho chote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa Yeye ulimwengu umesulibiwa kwangu, nami nimesulibiwa kwa ulimwengu. Kwa maana katika Kristo Yesu kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! Tangu sasa mtu ye yote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ikae pamoja na roho zenu. Amina. Huu ni wosia wa Paulo kwa Kanisa la Galatia, ndio wosia kwetu sote tuliobatizwa na kukubali kuwa Kristo ndiye mwokozi wa maisha yetu na kupigwa chapa ya Kristo ambayo ni msalaba.

Katika Injili Mwinjili Luka anasema, “Bwana aliweka wengine 72 nje na wanafunzi 12, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda katika kila mji alipokusudia kwenda mwenyewe. Namba 72 inasimama mahali pa makabila 72 au koo zilizoorodheshwa katika Sura ya 10 ya kitabu cha Mwanzo, namba kamili kama walivyofikiri Wayahudi, ikiwakilisha Makabila au Koo zote za dunia kwa wakati ule. Huu ni ujumbe kuwa kutangaza habari njema ni jukumu la kila mmoja wetu. Hivyo kila mbatizwa anawajibu wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo popote pale alipo katika maisha yake. Wazazi wana jukumu la kuwaridhisha na kuwafundisha imani watoto wao. Watoto nao wanaowajibu wa kuwafundisha wazazi wao imani na kuwakumbusha wajibu wao katika maisha ya sala na kulitafakari Neno la Mungu pale wanapojisahau. Mume anaalikwa kumpenda na kumwenjilisha mkewe, kadhalika mke anao wajibu kwa Mumewe kuona kwamba imani ndani ya familia inakuwa na kupewa kipaumbele hususani kwa malezi na makuzi ya watoto.

Ndugu katika familia: Kaka, dada na marafiki wanapaswa kuhubiriana Habari Njema. Hivyo kila mwanafamilia ni Mmisionari kwa mwenzake. Kila mbatizwa ni mmisionari kwa mwenzake. Tukishirikiana na maaskofu, mapadre, mashemasi na watawa tumpeleke Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Tunapaswa kupeleka habari njema kwa wasio wakatoliki. Baadhi yao wakiwa ni ndugu zetu katika familia: Siku hizi si ajabu ndani ya  kabila, ukoo  hata familia kuona kuna watu wa imani mbali mbali. Hivyo tunajukumu bado la kumshuhudia Kristo katika mazingira yetu ili watu wengine pia wamjue. Kristo anatoa masharti katika kumtangulia akisema, “Msimwamkie mtu njiani” ili tusichelewe pia tusiweke matumaini yetu katika watu au vitu: “Msichukue mfuko wala fedha, wala viatu”. Si fedha, wala elimu, wala mamlaka ya kibinadamu inayohitajika katika kumhubiri Kristo. Kinachohitajika ni ushuhuda wa maisha ya Kikristo na kuona fahari juu ya Msalaba.

Tunaitwa kuwa mabalozi wa amani na Upendo: ndiyo maana Kristo anasisitiza, katika kuenenda kwenu hii iwe ni salamu yenu: “Amani iwe ndani ya nyumba hii”. Kila Mkristo anapaswa kuwa mleta amani na mpatanishi wakati wote. Hatuwezi kuwa waleta amani au wapatanishi ikiwa amani ya Kristo haimo ndani yetu. Tuombe daima imani hiyo na upendo wa Kristo utawale katika mioyo yetu na katika jumuiya zetu. Tuwe jasiri na tusiokata tamaa katika kumshuhudia Kristo kwani anatuambia, “Na mji wowote mtakaoingia, nao hawakuwakaribisha, tokeni humo nanyi mkipita katika njia zake semeni, hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandama na miguu yetu, tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili “Ufalme wa Mungu umekaribia”. Hatupaswi hata mara moja kukata tamaa, wala kuogopa.

Ukweli ni kwamba kuwaleta watu kwa Yesu kunaleta furaha kuu ndani ya mtu binafsi na katika Jumuiya. Wote wanaojitahidi kuwaweka watu huru kutoka utumwa wa shetani, wanapata nguvu wanazohitaji katika shughuli hiyo ya kumshinda shetani. wakati wa majaribu kutoka kwa Mungu. Lakini furaha kubwa zaidi ni kuuridhi ufalme wa mbinguni ndivyo anavyotumbia Yesu: “Msifurahi kwa vile pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”

J14 Mwaka

 

04 July 2019, 14:38