Tafuta

Vatican News
Caritas Australia: Kipaumbele cha kwanza ni kupambana na baa la njaa DRC; ili kuokoa maisha ya watu pamoja na kupambana na ugonjwa wa Ebola unaopukutisha maisha ya watu! Caritas Australia: Kipaumbele cha kwanza ni kupambana na baa la njaa DRC; ili kuokoa maisha ya watu pamoja na kupambana na ugonjwa wa Ebola unaopukutisha maisha ya watu!  (AFP or licensors)

Balaa la njaa linazidi kuwapekenya wananchi wa DRC!

Jitihada za uhakika na usalama wa chakula nchini DRC zinakwamishwa pia na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Caritas Australia inasema, pamoja na changamoto zote hizi, lakini kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mapambano ya baa la njaa na utapiamlo nchini DRC, ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaoendelea kufariki dunia kwa sababu ya kukosa chakula bora na lishe safi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bwana Michael Landau, Rais wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Australia, Caritas Australia, hivi karibuni amehitimisha ziara ya kikazi kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC na kukiri kwamba, watu wanateseka sana kwa baa la njaa nchini humo, kumbe, mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza sanjari na kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinarejeshwa tena nchini humo. Wananchi wengi wa DRC wanateseka sana na baa la njaa na kwamba, wanazidiwa tu kwa sasa na Yemen ambayo inapekenywa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha! DRC ina ya utajiri mkubwa wa madini na rasilimali mbali mbali za nchi, lakini bado inasiginwa na baa la njaa, kiasi kwamba, pato ghafi la uchumi nchini humo kwa mwaka 2019, linakadiriwa kuwa ni asilimia 4.6.%.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe, kinzani na mipasuko ya kisiasa na kijamii; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa ulinzi, usalama, amani na utulivu ni mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa ukosefu wa usalama na uhakika wa chakula nchini DRC. Hali hii inaathiri sana hata ubora na kiwango cha elimu inayotolewa nchini humo na kwamba, waathirika wakubwa ni watoto hasa wale wanaotoka kwenye familia maskini zaidi. Watoto wengi wanaishi katika mazingira tete na hatarishi kiasi kwamba, hata malezi na makuzi yao yako mashakani sana! Jitihada zote hizi, zinakwamishwa pia na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao umekuwa ni tishio kubwa kwa usalama na maisha ya wananchi wengi nchini DRC. Caritas Australia inasema, pamoja na changamoto zote hizi, lakini kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mapambano ya baa la njaa na utapiamlo nchini DRC, ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaoendelea kufariki dunia kwa sababu ya kukosa chakula bora na lishe safi.

Caritas Australia inakaza kusema, sababu zinazopelekea kuendelea kushamiri kwa baa la njaa nchini DRC ni vita, ugonjwa Ebola pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Caritas Autsralia kwa muda wa miaka ishirini imekuwa ikitembea bega kwa bega na familia ya Mungu nchini DRC katika utekelezaji wa sera na mikakati ya huduma na maendeleo fungamani ya binadamu kama sehemu ya kutangaza na kumwilisha Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbali mbali! Kuna haja pia ya kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kupambana na hali pamoja na mazingira yao kutokana na ukweli kwamba, mchango unaotolewa na wafadhili wa Caritas Australia umeporomoka kwa kiasi kikubwa kwa miaka ya hivi karibuni. Kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea kufanyika kwenye Serikali ya Australia, yote haya yanachangia kwa sehemu kubwa mapato ya Caritas kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Kumbe, kwa sasa Caritas Australia inataka kutekeleza miradi inayopania kuwajengea wananchi wa DRC uhakika wa usalama wa chakula, lakini kwanza, Serikali ya DRC inapaswa kujifunga kibwebwe kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

DRC:Balaa la Njaa
08 July 2019, 10:48