Tafuta

Vatican News
Bikira Maria wa Mlima Karmeli ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya sala, ukimya na tafakari ya kina; kufunga, kujinyima na kujisadaka katika huduma pamoja na maisha ya ufukara. Bikira Maria wa Mlima Karmeli ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya sala, ukimya na tafakari ya kina; kufunga, kujinyima na kujisadaka katika huduma pamoja na maisha ya ufukara. 

Bikira Maria wa Mlima Karmeli: Malkia, Mlinzi na Mhudumu wa Injili ya upendo!

Bikira Maria wa Mlima Karmeli ni mfano bora wa kuigwa katika kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazofumbatwa katika: maisha ya sala endelevu na dumifu; katika ukimya na tafakari ya kina; katika mchakato wa kufunga, kujinyima na kujisadaka ka ajili ya jirani na umuhimu wa kudumisha ufukara kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Bikira na Mama!

Na Sr. Veronica Silvester Buganga, CMTBG - Roma.

Bikira Maria wa Mlima Karmeli  tunamtambua kama  Mama wa Mungu na Mama wa Kanisa lakini zaidi tunajisikia kuwa ni Mama yetu na dada kutokana na fadhira  yake ya unyenyekevu, wema na upole tunajisikia ndugu wa karibu ambaye unakuwa huru kumshirikisha kila kitu hata kumfungulia moyo  kama mtoto kwa mama, Mama wa Skapulale takatifu (ulinzi-katika hatari zote za roho za na mwili) .Tunamuenzi kama Mlezi na Kiongozi, Malkia,… Tunaalikwa kumuiga Bikira Maria katika tunu msingi hasa : Sala endelevu, umaskini, upweke na kufunga, upole, utayari, usafi, kuwa wafuasi na wamissionari wa mwanae, “kuwa Maria mwingine maana yake kumvaa Kristo na kumpeleka duniani kote, kumzaa Yesu katika maisha ya watu” Mwenye heri Tito Brandsma.

Roho ya Wakarmeli: Kukutana na Mungu katika undani wa maisha! Roho ya Wakarmeli ni hamu moto moto wa nafsi, shauku ya kutaka kuwa na uzoefu wa moja kwa moja na Mungu, kukutana naye rohoni. Kwa maneno mengine, roho ya Wakarmeli i katikati ya roho ya sala, anayeeleweka kama rafiki wa upendo kati ya nafsi ya mtu na Mungu, ambaye hujizamisha katika tafakari kama zawadi ya bure ya Mungu. Roho ya Wakarmeli inalenga kukuza uhusiano makini kati ya mwamini na Yesu Kristo. Huu ndio mvuto ambao Wakarmeli wameuona na kuutamani kwa Bikira Maria na Nabii Eliya. Hawa wawili walikutana na Mungu rohoni mwao, katika upweke na utii wa sauti ya Mungu.

Mvuto wenye mashiko na Ushawishi makini! Wakarmeli tuna uhusiano wa kipekee na Bikira Maria na Nabii Eliya. Uhusiano huu una maana ya “nafasi yake katika maisha yetu” ambayo inatufanya tumtambue katika dhamiri zetu kwamba yeye ni, Dada, Mama na Mlezi wetu. Wakarmeli wa kwanza walikuwa na dhamiri hiyo tangu walipoanza kuishi katika mlima Karmeli. Bikira Maria na Eliya ni watu wenye mvuto na ushawishi mkubwa kwa Wakarmeli kutokana na maisha yao na uhusiano wa pekee waliokuwa nao na Mungu. Mfano mzuri na wa wazi ni jinsi Neno la Mungu lilivyopata nafasi katika maisha yao. Imani yao kwa Mungu ilikuwa ni dhabiti na haikuteteleka kamwe.

Kutokana na sifa za kiimani, kimapendo, na kimatumaini walizokuwa nazo, Wakarmeli walipenda na tunaendelelea kumtukuza Mungu kwa kuwaiga wao yaani walitaka kuzifuata nyayo za Mama Maria na Nabii Elia hasa katika sala, taamuli na huduma kati ya watu. Tamanio hilo walilokuwa nalo la kuwaiga, liliwasukuma kuzifuata nyayo zao si kiroho tu wakiwa mbali, bali hata kwa kwenda wenyewe mahali walipoishi watumishi hawa wa Mungu (Mlima Karmeli ulioko nchi takatifu). Kutokana na heshima kubwa waliyokuwa nayo kwa Bikira Maria na kwa kuvutwa naye, basi Wakarmeli wa kwanza walijenga kikanisa cha kwanza kabisa pale mlima Karmeli na wakakiweka wakfu kwa heshima yake. Yeye alikuwa mama katikati yao. Ndugu msikilizaji tujiulize leo katikati ya nyumba ya familia zetu kuna hirizi au picha ya Yesu na Maria? na rohoni mwetu Je,? kuna hamu na kiu ya nini?

Malkia, Mlinzi na Mhudumu wa Injili ya upendo kwa Mungu na jirani! Uhusiano wa Wakarmeli na Maria una uzito wa kipekee na ni wa ndani zaidi ukilinganisha na uhusiano tulionao kati yetu na Eliya. Tangu mwanzo kabisa mwa ukarmeli kama inavyoelezwa katika «Propositum» [1], nia ya Wakarmeli ya kumtii au kujitoa wazima kwa Kristo ambaye ndiye Mtawala na «Bwana wa eneo», yaani Nchi Takatifu, iliwasababisha wawe na uhusiano wa moja kwa moja na Maria Mama wa Yesu Kristo. Waliamini kuwa kwa kuwa Yesu alikuwa «Bwana wa eneo» basi hata mama yake alikuwa «Mama wa eneo». Maelezo hayo ya kiuhusiano na ya kiutawala, yaani: «Bwana wa eneo» na «Mama wa eneo» yalitokana na fikra za kiutawala za nyakati zile ambazo zilikuwa zikiukweza ukabaila usiokuwa na mvuto wala mashiko. Eneo lilolengwa ilikuwa ni Nchi Takatifu. Wakarmeli waliamini kuwa, kazi kubwa ya Mama Bikira Maria “Mama wa eneo” ilikuwa ni kuwahudumia na kuwasaidia watumishi wa mwanae katika mahitaji yao msingi. Suala hilo liliwafanya wamtambue Maria kama mlezi wa Shirika.

Bikira Maria ni Mlezi na Kiongozi wa Shirika na Kanisa: Wakarmeli walipomchagua Maria kuwa Mlezi lakini zaidi kuwa Mlinzi wa Shirika walijua kuwa anao uwezo na nafasi ya kufanya hivyo kutokana na neema tele alizojaliwa na nafasi yake pamoja na utukufu wa mwanae mpendwa. Katika imani yetu, sisi Wakatoliki tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu ametupatia malaika walinzi ili watulinde na watuepushe na hatari zote za kiroho na za kimwili (Rej. Zab 91:11-12)[2]. Lakini ulinzi wa Bikira Maria ni wa aina yake kwani yeye ni Malkia wa malaika na mama wa Kanisa zima. Ameshiriki kwa namna ya pekee katika kazi ya ukombozi. Kwetu sisi Wakarmeli ishara ya ulinzi wa Bikira Maria ni skapulari. Imani hiyo tumeipokea kutoka kwa Wakarmeli wa kwanza kabisa ambao walijenga kikanisa cha kwanza katikati ya makazi yao, yaani katika mlima Karmeli, na wakakiweka wakfu kwa heshima ya Bikira Maria.

Ulinzi wake kwa wanashirika, kama ilivyo kwa wanakanisa wote, unatokana na nguvu za neema alizojaliwa na Mwenyezi Mungu ambazo zilimwezesha kushiriki kwa namna ya pekee kabisa katika kuufanikisha mpango wa Mungu wa kuwakomboa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Kwa kuwa Wakarmeli wa kwanza walimweka Kristo katikati ya maisha yao, kama Mwongozo wa Maisha ulivyowaelekeza, walitumia muda mwingi wa maisha yao kumtafakari Yesu mfufuka, wakiamini kuwa walikuwa wakisali pamoja na Maria. Kadiri walivyokuwa wakimtafakari Kristo kwa undani zaidi, ndivyo walivyopatiwa hekima ya kuifahamu hata nafasi ya Bikira Maria katika fumbo la Kristo na la Kanisa.

Usafi wa moyo kwa mfano wa Bikira Maria! Inafahamika katika mafundisho ya Kanisa kuwa usafi wa Maria ambao uliotokana na kujazwa neema nyingi ulimfanya akubali mpango wa Mungu bila kusita kwa kuitikia “Ndiyo” wakati alipopashwa habari na Malaika Gabrieli. Sisi Wakarmeli, kama ilivyo hata kwa Wakristo wengine, tunaalikwa kumwiga kikamilifu Bikira Maria, aliyekingiwa dhambi ya asili na aliyejaa neema, tukiamini kuwa tunaweza kufanya hivyo kwa njia ya sala, tafakari na kusikilizaji Neno la Bwana na kushiriki Sakramenti kwa unyenyekevu mkubwa. Usafi wa Maria ni uzuri uliomvutia Mungu ambaye kwa utayari wa Maria aliipatia dunia Mwokozi. Ndiyo maana maisha ya wakfu yanamtaka mtu kuwa tayari kumsikiliza na kumwamini Mungu wakati wote ili moyo uwe safi.

Sikio la Bikira Maria lilimwelekea Mungu daima [3]. Maria alimsikiliza hata mwanae katika kazi yake ya ukombozi ndiyo maana anaitwa “mwanafunzi wa kwanza wa Yesu”. Hili lilirutubishwa na usafi wa moyo aliojaliwa na Mungu naye akautunza. Kwa mantiki hiyo basi, kila Mkarmeli anayetaka kumtumikia Kristo kwa uaminifu inabidi ajifunze kutoka kwa Maria. Ndiyo maana hata Maria anaitwa mwalimu na kiongozi. Kama walivyowahi kusema watakatifu na wenye heri Wakarmeli (Kwa mfano, Elisabetta wa Utatu Mtakatifu) kuwa Maria anaonyesha njia ya utakatifu uliyomshinda Eva. Njia hiyo ni kumwamini Mungu kabisa, kumtii na kumpenda.

Tunampomtafakari Maria tunaalikwa kumwiga katika tunu zifuatazo: Sala endelevu na dumifu! Sala katika maisha ya kikarmeli ni tunu ambayo hutokana na mwito wa kumweka Kristo katikati ya mambo yote. Sala ni maongezi yenye uhusiano binafsi kati ya mtu na Mungu na humwezesha anayesali kuwa na uwezo wa kulisikiliza na kulipokea Neno la Mungu kwa utayari wa kuliweka katika matendo kama alivyofanya Maria. Tunu hii ya ndani huongeza shauku ya kumtafuta Mungu katika maisha ya kila siku. Moyo uliozoea kusali hujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu kwa ajili ya kusimama imara katika imani kwa lengo la kuyashinda majaribu ya yule mwovu.

Tabia ya kupenda sala ni tunu ya ndani kabisa ya roho ambayo mtu anatakiwa aikuze. Sala kama tabia ya kudumu ya kuufungua moyo kwa ajili ya kuongea na Mungu, humuongoza mtu katika kujifahamu vizuri na hivyo huboresha uhusiano wa kimapendo kati yake na Mungu aliye Upendo wa ndani kabisa wa roho. Anayesali kwa imani huboresha uhusiano wake na watu wengine wanaomzunguka, katika jumuiya au katika jamii. Mkarmeli anatakiwa awe mwalimu wa sala. Sehemu muhimu katika sala ya jumuiya na ya binafsi ni kushiriki adhimisho la Misa Takatifu ambayo ni chemchemi na kilele cha maisha ya kijumuiya na ya kikristo. Ekaristi ni nguvu ya maisha ya kitawa na ya kikristo kwa ujumla wake. Sala ina nguvu ambazo huunganisha moyo wa anayesali na Mungu kwa ajili ya kuonja upendo usioelezeka kwa maneno bali hutambulika katika nafsi.

Ukimya na tafakari ya kina katika maisha! Ukimya ni mojawapo ya vitu muhimu tunavyovikuta kwa Maria na Eliya. Maria alikuwa ni mama wa ukimya na tafakari (Lk 2:19,51). Lengo kuu la kusisitiza ukimya ni kumsaidia mtu kuwa tayari kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu na kumpa nafasi nzuri ya kulitafakari Neno la Mungu kwa kina na mapana yake. Mafumbo yasiyoeleweka hutafakariwa katika ukimya. Fumbo la ukombozi linahitaji ukimya. Maandiko Matakatifu yanasema kuwa Mungu wetu ni Mungu wa ukimya na hunena Neno lake katika ukimya. Lakini kuwa kimya haina maana ya kuwa mpweke, yaani mwenye huzuni asiye na neno lolote la kuongea kwa wengine na asiye na watu wengine wa kuongea naye. Hiyo si maana ya ukimya, bali ukimya ni mojawapo ya kipawa cha kihekima ambacho ni uhalisia wa mpangilio kamili wa utendaji wa haki ndani ya roho.

Ushuhuda huo unapatikana katika kitabu cha Hekima ya Sulemani mahali panapoongelea tukio la kuokolewa kwa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri,: «Kwa maana majira mambo yote yalipokuwa kimya, na usiku ulikuwa katikati ya mwendo wake mwepesi, Neno lako Mwenyezi alishuka toka mbinguni, kutoka kiti chako cha kifalme….mwenye upanga mkali» (Rej. Hek 18:14-18; Yoh 1:1.14). Kuishi katika ukimya ni kutoa nafasi ya kutosha kwa Mungu ili aweze kunena Neno lake la wokovu ambalo hufanya kazi ndani mwetu. Kuwa kimya ni kuwa katika hali ya usikivu makini kwa lengo la kusikiliza kile anenacho Mungu. Ndiyo maana nyumba nyingi za kikarmeli huweka mazingira mazuri ya ukimya na upweke, kwa lengo la kumsaidia Mkarmeli aweze kuyaelekeza mawazo na fikra zake katika mambo ya kiroho. Watakatifu wengi Wakarmeli wanasema kuwa kuishi katika hali ya ukimya kwa lengo la kuyatafakari mafumbo ya wokovu, humfanya mtu aingie katika hali ya muungano na Mungu kwa kiwango cha juu kabisa.

Kufunga, kujinyima na kutoa sadaka kwa ajili ya wengine! Kitu kingine ambacho Wakarmeli wamekiendeleza katika hali ya kumwiga Maria ni na Eliya ni kufunga na kujinyima. Maisha ya sala hupata nguvu kwa kujinyima na kufunga. Kujinyima kwa watawa ni jambo la maana sana kwani huilainisha roho na huwapatia wanaojinyima nguvu za ziada za kuitiisha miili yao ili isiwe tegemezi katika anasa za kidunia. Tendo hili la kujinyima huisafisha roho na kuifanya iwe katika hali ya kupokea mwanga wa Kristo bila kuweka ukinzani wa ndani. Nguvu za kiroho huwa ndiyo silaha za kuvishinda vishawishi viletwavyo na vionjo vya kimwili. Mtu anayetaka kuupanda mlima Karmeli kwa ajili ya kukutana na Kristo na kulipokea Neno lake, inambidi awe tayari kujikatalia kwa ajili ya Mungu na jirani. Awe tayari kumtumikia Kristo kwa: «moyo safi na kwa dhamiri nyoofu».

Ufukara kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu: Ni hali ya kumtegemea Mungu kwa kila kitu na kwa kila hali. Maskini ni yule asiye na kitu cha manufaa ya kibinafsi. B. Maria ni mwalimu na kiongozi  wa hizi tunu msingi za maisha ya ukomavu wa kikiristo. Hali hiyo ndiyo inayosisitizwa katika maisha ya Wakarmeli, wawekwa wakfu na Kanisa zima. Mtakatifu Yohane Paulo wa II anasema “Kujua kumtegemea Mungu kila siku ni njia inayokuelekeza katika maisha ya ukamilifu , kama walivyofanya watakatifu wakubwa wa karmeli (Mtakatifu Theresa wa Yesu),kama vile kukwea mlima karmeli, (Mtakatifu Yohane wa Msalaba) katika hii safari yupo B.Maria msaada, mwombezi, kioo cha fadhira, mtii na msikivu kwa mpango wa Mungu kwa njia ya Kristo na Roho Mtakatifu. Ndio maana huwezi kumtenga na wakarmeli ambao kwa yeye inakuwa ni namna mpya ya kuishi kwa na ajili ya  muungano kamili na Mungu na kuendeleleza duniani upendo wa Mwanae…anawaalika watu  wote wenye ibada kwa kwa Bikira Maria kupitia Skapulare wajibidiishe kumuenzi na kumuiga Maria kama Mama, Mlezi, Dada, Bikira mwenye usafi kamili wakizama zaidi katika Neno, Sala na Maisha ya Kisakramenti na kuibuka kwa ari kuwahudumia watu, huu ni mwaliko kwa watu wote wanaomheshimu Bikira Maria na kumkimbilia ili aweze kuwa mwombezi wetu, tuweze kusafiri na kufika salama katika kilele cha mlima  Mtakatifu yaani BWANA WETU, YESU KRISTO”.

Bikira Mari9a Karmeli

 

15 July 2019, 16:39