Tafuta

Askofu Mstaafu Damiani Kyaruzi wa Jimbo Katoliki Sumbawanga, Tanzania anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, Januari 1968! Askofu Mstaafu Damiani Kyaruzi wa Jimbo Katoliki Sumbawanga, Tanzania anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, Januari 1968! 

Askofu Mstaafu Damiani Kyaruzi: Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre!

Askofu Mstaafu Kyaruzi alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 29 Januari 1968. Kumbe, amelitumikia Kanisa kama Padre katika kipindi cha miaka 51. Aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga hapo tarehe 21 Januari 1997. Kumbe, anamshukuru Mungu pia kwa zawadi ya ukamilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre kama Askofu amehudumia miaka 22.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma, upendo na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema na baraka ya kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama shuhuda na chombo cha huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko na changamoto ya kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa imani, matumaini na mapendo thabiti!

Askofu Mstaafu, Damian Kyaruzi wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga nchini Tanzania, Jumamosi iliyopita ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Jubilei ya Miaka zaidi ya 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 29 Januari 1968. Kumbe, amelitumikia Kanisa kama Padre katika kipindi cha miaka 51. Itakumbukwa kwamba, aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga hapo tarehe 21 Januari 1997 na kuwekwa wakfu tarehe 29 Juni 1997! Kumbe, anamshukuru Mungu pia kwa zawadi ya ukamilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre kama Askofu ambaye amelihudumia Kanisa kwa muda wa miaka 22 si haba yataka moyo kweli kweli! Tarehe 19 Aprili 2018 akang’atuka kutoka madarakani.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga,  wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akiwa mjini Vatican kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani sanjari na kupewa Pallio takatifu, amemtumia salam na matashi mema anapomshukuru Mungu kwa kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kimsingi, sherehe hizi zilipaswa kufanyika Juni 2018, lakini, siku kuu hii iliangukia kwenye Sherehe ya kuwekwa wakfu na hatimaye, kusimikwa kwa Askofu Beatus Christian Urassa, ALCP/OSS kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

Katika kipindi cha uongozi na huduma yake ya Kiaskofu amekuwa ni hazina na amana katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Ni kiongozi ambaye wakati wote ameonesha moyo wa utume, majitoleo na sadaka safi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Askofu Mstaafu Damian Kyaruzi ni kiongozi ambaye amejisadaka kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kuchota utajiri na amana kutoka katika maisha ya sala, tafakari ya kina katika Maandiko Matakatifu pamoja na uzoefu wa shughuli za kichungaji. Amefanya kazi kubwa Jimboni Sumbawanga na matunda ya maisha na utume wake yanajidhihirisha wazi kutokana na ukomavu wa imani ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

Kumekuwepo na ongezeko kubwa la miito mitakatifu ya kitawa na kipadre na kwamba, wakati wote waamini wameonesha umoja, mshikamano na upendo. Mafanikio yote haya anasema Askofu mkuu Nyaisonga, yamechangia pia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Mbeya na Mpanda pamoja na majimbo jirani ambayo kimsingi yana uhusiano mkubwa wa kihistoria, kijiografia na hata katika shughuli za kichungaji. Familia ya Mungu nchini Tanzania inamshukuru na kumpongeza Askofu Mstaafu Damiani Kyaruzi kwa sadaka, maisha na utume wake kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Wanamshukuru Mungu, kwa kumjalia Askofu Mstaafu Kyaruzi, afya njema, iliyomwezesha kuchakarika usiku na mchana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

Askofu Mkuu Nyaisonga anasema, kwa kweli, Askofu Mstaafu Kyaruzi, akibahatika kuwa na fadhila ya uvumilivu na udumifu na sasa katika uzee wake, anajisikia kuchoka. Familia ya Mungu nchini Tanzania hata katika hali na mazingira kama haya, bado inamwombea afya njema, imani thabiti, upendo na matumaini, ili aendelee kushirikisha hekima na busara zake katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga,  wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, anahitimisha mahojiano haya maalum na Radio Vatican kwa kusema,  wazee ni hazina na amana ya utume na maisha ya Kanisa!

Askofu Mstaafu Damiani Kyaruzi, enzi zetu tukiwa Seminari kuu ya Ntungamo, tulimtambua kama Dokta Kyaruzi, yaani hadi raha, Jumamosi wakati wa “Outing” kama bado hujajiandaa kwa tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili inayofuata, ilikuwa ni ngumu kuomba “lift njiani” na matokeo yake....! Yaani, Baba Askofu Damian Kyaruzi, shukrani kwa maisha na utume wako, leo hii wengi wetu tumekuwa hivi tulivyo ni kutokana na changamoto ulizotupatia katika malezi na makuzi ya kipadre! Utukumbuke katika sala na sadaka yako, ili hata sisi ambao tuko katika huduma hii, tuchote utajiri wa hekima yako kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania!

Askofu Damian Kyaruzi
01 July 2019, 17:18