Tafuta

Vatican News
Kongamano la Vijana wa Jimbo kuu la Mwanza: Vijana wametakiwa kuwa ni mashuhuda wa imani, maadili na utu wema, wasikubali kumezwa na malimwengu Kongamano la Vijana wa Jimbo kuu la Mwanza: Vijana wametakiwa kuwa ni mashuhuda wa imani, maadili na utu wema, wasikubali kumezwa na malimwengu  (AFP or licensors)

Kongamano la Vijana Jimbo kuu la Mwanza: Imani, Maadili & Utu wema

Vijana wasimame imara katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili yanayoongozwa na kusimamiwa na Amri za Mungu pamoja na Sala kama majadiliano na Mwenyezi Mungu. Hizi ni chemchemi za utakatifu wa maisha ya ujana. Vijana wawe imara katika imani yao na kamwe wasitafute njia za mkato. Waone fahari kulikimbilia Kanisa ambalo kimsingi ni Mama na Mwalimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, aliweka sahihi kwenye Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Wosia huu umezinduliwa rasmi, tarehe 2 Aprili 2019. Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito”. Huu pia ni mwendelezo wa mchakato wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, kwani utume wa Kanisa kwa familia na vijana ni sawa na chanda na pete; unategemeana na kukamilishana! Wosia huu wa kitume umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana na Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo.

Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018. Katika sura ya kwanza, Baba Mtakatifu anakita tafakari yake kwenye Neno la Mungu kuhusu vijana tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya. Sura ya Pili inamwonesha Kristo Yesu ambaye daima ni kijana na chemchemi ya ujana wa Kanisa kama ilivyo hata kwa Bikira Maria, msichana wa Nazareti. Sura ya tatu, Vijana wanaambiwa kwamba, wao ni leo ya Mungu inayofumbatwa katika matamanio halali ya vijana, madonda wanayokumbana nayo katika hija ya maisha yao pamoja tafiti endelevu kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya ujana.

Baba Mtakatifu anagusia changamoto za ujana zinazoibuliwa katika ulimwengu wa kidigitali, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo pamoja na kuonesha mwanga unaoweza kuwaokoa vijana kutoka katika giza hili la maisha. Sura ya nne ni mbiu kwa vijana wote kwamba, “Mungu ni upendo”, Kristo Yesu anaokoa na kwamba, yu hai kabisa na kwa njia ya Roho Mtakatifu, vijana wanaweza kuboresha maisha yao. Sura ya tano inaonesha mapito ya ujana katika makuzi na ukomavu; vijana wanaojisadaka na kujitosa kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Vijana wanakumbushwa kwamba, wanaitwa na kutumwa kama wamisionari jasiri, ili kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya maisha yao katika ukweli, hii ni changamoto kwa vijana wote!

Sura ya sita, inawaonesha vijana waliokita mizizi yao katika mambo msingi ya maisha. Hawa ni wale vijana wenye uwezo wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na wazee; ili kumwilisha ndoto na maono, ili kwa pamoja, wazee na vijana waweze kuthubutu! Sura ya saba ni kuhusu utume wa Kanisa kwa vijana, kwa kuwasindikiza na kuwaongoza, wao wenyewe wakionesha kipaji cha ubunifu. Mkazo katika utume kwa vijana: tafiti na ukuaji! Kanisa linapaswa kujenga mazingira yatakayosaidia kumwilisha vipaumbele hivi. Kanisa pia linapaswa kuwekeza zaidi katika utume wa vijana kwenye taasisi za elimu na vyuo vikuu; kwa kuendesha pia utume wa vijana katika “vijiwe vya vijana” ili kuwatafuta na kuwaendea huko huko waliko, daima kwa kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu. Daima vijana wakumbuke kwamba, wao ni wamisionari, kumbe, utume kwa vijana unapaswa kujikita katika umisionari, huku vijana hawa wakiwa wanasindikizwa na watu wazima na wakomavu, ili kujitambua na kwamba, wanapaswa kutembea bega kwa bega, huku wakiheshimu na kuthamini uhuru wao!

Sura ya nane, Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu miito, kwa kukazia upendo na familia, ili kujisadaka bila ya kujibakiza katika kazi na hatimaye, ujenzi wa familia bora! Baba Mtakatifu anatambua fika changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana, lakini wawe wepesi kusoma alama za nyakati kwa kuondokana na kishawishi cha kutaka kuchagua kazi, jambo la msingi kwanza ni huduma! Baba Mtakatifu anahitimisha sura ya nane kwa kuangalia wito maalum unaowasukuma vijana kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya kipadre na kitawa, kama utimilifu wa maisha yao! Sura ya tisa ni kuhusu: Mang’amuzi ambao ni mchakato unaomwezesha kijana kutambua wito wake katika maisha! Hii ni dhamana inayohitaji ukimya na tafakari ya hali ya juu, ili kuweza kutoa maamuzi mazito katika maisha.

Mang’amuzi ya miito yanapaswa kuzingatia mambo makuu matatu: kusikiliza kwa makini; kufanya maamuzi ya busara na hatimaye, kusikiliza kutoka katika undani wa maisha, ili kutambua ni mahali gani ambako Mwenyezi Mungu anamtaka kijana huyu kwenda. Baba Mtakatifu anahitimisha Wosia huu wa kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” kwa kuonesha hamu ya furaha ya moyo wake kwani anataka kuwaona vijana ambao wanaonekana kwenda taratibu na waoga katika maisha, kuanza kutimua mbio na kumwendea Kristo Yesu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kanisa linahitaji ari na mwamko wa vijana wa kizazi kipya; maoni yao, lakini zaidi imani inayomwilishwa katika ushuhuda wa matendo! Baba Mtakatifu kwa unyenyekevu anawakumbusha vijana kwamba, wakifanikiwa kwenda mbio na kufika mwishoni mwa safari, wawe na uvumilivu ili kuwasubiria wazee wanaojikongoja! Ni katika muktadha huu, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania linaloundwa na Majimbo ya Kanda ya Ziwa Victoria yaani: Jimbo Katoliki la Bukoba, Rulenge-Ngara, Geita, Shinyanga, Bunda na Musoma, hivi karibuni yameadhimisha Kongamano la Vijana wa Jimbo kuu la Mwanza ambalo limeongozwa na kauli mbiu “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Wafilipi 4:13).

Kongamano hili limeadhimishwa Jimboni Bunda na kuzinduliwa na Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, mtaalam wa utume wa vijana wa kizazi kipya. Askofu Kassala katika mahubiri yake amewakumbusha vijana athari wanazoweza kukumbana nazo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwa kama hawatadumisha kanuni maadili na utu wema. Changamoto inayokuja kwa kasi katika nchi nyingi za kiafrika ni uhuru usiokuwa na mipaka wala nidhamu mintarafu mapenzi ya watu wa jinsia moja, dalili za utamaduni wa kifo!

Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kwa kuheshimu utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pamoja na umuhimu wa watu kushiriki katika mpango wa kazi ya uumbaji. Umaskini wa hali na kipato sanjari na hali nguvu ya maisha wanayokumbana nayo, isiwe ni sababu ya kujiingiza katika vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha uhuru wa kuabudu, Injili ya uhai, umoja na mafungamano ya kijamii. Vijana wajenge na kukuza utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kushirikisha maoni yao na kusikiliza pia ushauri kutoka kwa wazazi na walezi wao, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu kadiri ya mwanga wa Injili ya Kristo!

Vijana waoneshe jeuri ya kuutafuta, kuutambua, kuukumbatia na kushuhudia ukweli, unaowaweka huru. Vijana wasimame imara katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili yanayoongozwa na kusimamiwa na Amri za Mungu pamoja na Sala kama majadiliano na Mwenyezi Mungu. Hizi ni chemchemi za utakatifu wa maisha ya ujana. Vijana wanapaswa kuwa imara katika imani yao na kamwe wasitafute njia za mkato kwa kutangatanga ovyo, bali waone fahari kulikimbilia Kanisa ambalo kimsingi ni Mama na Mwalimu. Askofu Kassala anasema, Kongamano la Vijana Jimbo kuu la Mwanza iwe ni fursa kwa vijana kufunguka zaidi ili kuangalia changamoto zinazowaandama, tayari kuzivalia njuga kadiri ya miongozo inayotolewa na Mama Kanisa na kwa wakati huu, vijana wajielekeze zaidi katika kutafakari na kumwilisha katika uhalisia wa maisha yao, Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo Anaishi”.

Hii ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa vijana katika Kanisa Katoliki. Vijana wawe mstari wa mbele katika kutafuta, kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi wakitambua kwamba, wao kimsingi wanapaswa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa haki, amani na maridhiano katika maeneo yao. Mwalimu wa kwanza kabisa kwa vijana ni maisha yao, wakiyachezea wakati huu, watakiona cha mtema kuni kwani kama kawaida Waswahili wanasema, eti fainali uzeeni! Vijana wakimbilie ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kuhusiana na changamoto changamani za Uinjilishaji mada iliyodadavuliwa na Padre George Nzugu amegusia kuhusu: ujana na changamoto zake; Uinjilishaji na changamoto zinazohitaji majadiliano ya kiekumene; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Mafanikio ya chapuchapu na utajiri usiokuwa na jasho ni mambo yanayowapelekea vijana kujiingiza katika ushirikina sanjari na utovu wa nidhamu; bila kusahau utumwa mamboleo unaokumbatia: biashara ya ngono: ushoga na usagaji; matumizi haramu ya dawa za kulevya, biashara ya binadamu na viungo vyake. Haya ni mambo ambayo watu wanadhani kwamba, yanatungwa, lakini huu ndio ukweli wa mambo!

Mada ya vijana na mahusiano, iliwasilishwa na Bwana William Bhoke kutoka Jimbo Katoliki la Bunda ambaye amewataka vijana kukuza na kudumisha mahusiano mazuri na Mwenyezi Mungu, Kanisa na Jirani zao. Vijana wafanye mang’amuzi ya kina kabla ya kuanzisha mahusiano na hatimaye, uchumba na ndoa au wito na maisha ya kitawa na kipadre. Mada nyingine zilizojadiliwa kwenye Kongamano la Vijana Jimbo kuu la Mwanza ni pamoja na: Imani yaUkristo na Ushirikina; Changamoto ya ukosefu wa ajira na nafasi za kazi miongoni mwa vijana: Vijana na utetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na umuhimu wa Liturujia kama mahali pa kumsifu, kumwabudu na kumtukuza Mungu ili mwanadamu pia aweze kutakaswa na hatimaye, kuokolewa.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walifanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika Liturujia kwa kutambua nafasi ya Liturujia katika Fumbo la Kanisa, kwani Liturujia ni kilele na chemchemi ya maisha ya Kanisa. Mama Kanisa anaendelea kuwachangamotisha viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika malezi makini ya Kiliturujia pamoja na ushiriki hai wa waamini katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kwa mara ya kwanza Kongamano la Vijana Jimbo Kuu la Mwanza liliadhimishwa Jimboni Geita, kisha Jimbo la Bukoba na Mwaka 2019 Jimbo Katoliki la Bunda. Zote hizi ni jitihada za Jimbo Kuu la Mwanza kuanzia mwaka 2016 kuwekeza kwa kasi kubwa katika utume wa vijana!

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza nchini Tanzania ambaye wakati wa maadhimisho ya Kongamano hili alikuwa mjini Vatican kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu katika Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na Miamba wa imani, kwa njia ya Radio Vatican aliwatumia vijana ujumbe akiwatakia heri na baraka katika maadhimisho ya kongamano lao. Iwe ni fursa ya kusali, kutafakari na kufanya mang’amuzi mazito katika maisha. Vijana waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu awajenge na kuwaimarisha katika maisha na wito wao kama vijana Wakatoliki. Kongamano hili anasema Askofu mkuu Nkwande, iwe ni fursa ya vijana kukutana ili kujenga na kudumisha majadaraja yanayowakutanisha, ili kufahamiana na hatimaye, kujenga urafiki wenye tija na mashiko.

Askofu mkuu Nkwande, kwa niaba ya Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga,  wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wamewatakia kila jema na wamewaombea ili wawe vijana imara, thabiti na jasiri; walipende na kuliheshimu Kanisa lao. Wawe tayari kusimama kidete kulinda, kutangaza na kuitetea imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kama hata ilivyokuwa kwa Mitume, watakatifu na waungama imani. Hii ndiyo amana na utajiri wanaoona fahari kuungama, kuutangaza na kuushuhudia, kwani ni urithi ambao unapaswa kuendelezwa kizazi baada ya kizazi.

Kongamano Vijana
06 July 2019, 15:28