Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, anawataka wasomi kujenga utamaduni wa kurejea nchini mwao, ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, anawataka wasomi kujenga utamaduni wa kurejea nchini mwao, ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.  (ANSA)

Askofu mkuu Nkwande, Wasomi rudini nyumbani kumenoga hadi raha!

Askofu mkuu Nkwande amewataka watanzania wanaojipatia elimu, ujuzi na maarifa kujenga utamaduni wa kurejea nyumbani mara tu wanapohitimu masomo yao, ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji, ujenzi wa Kanisa na Ufalme wa Mungu! Kwa hakika nyumbani kumenoga! Wasomi wanaotumwa ughaibuni watambue kwamba, hii ni sadaka na majitoleo makubwa ya watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza nchini Tanzania, amewataka watanzania wanaojipatia elimu, ujuzi na maarifa kujenga utamaduni wa kurejea nyumbani mara tu wanapohitimu masomo yao, ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji, ujenzi wa Kanisa na Ufalme wa Mungu! Kwa hakika nyumbani kumenoga! Wasomi wanaotumwa ughaibuni watambue kwamba, hii ni sadaka na majitoleo makubwa ya watu wa Mungu, ili kuwajengea uwezo utakaosaidia wongofu wa shughuli za kichungaji kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima. Askofu mkuu Nkwande, ameyasema hayo, Jumamosi, tarehe 29 Juni 2019 kwenye hafla iliyoandaliwa na Jumuiya ya watanzania wanaoishi na kusoma Roma.

Hili ni tukio lililofuatia mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na Miamba ya imani, ambamo, Baba Mtakatifu Francisko alibariki na kuwakabidhi Maaskofu wakuu wapya 31, Pallio Takatifu, alama ya Kristo Mchungaji mwema, umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika hafla hii, Askofu mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya pamoja na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu wamehudhuria. Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania ni ushuhuda tosha wa kwamba, imani ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania inazidi kukua, kupanuka na kushuhudiwa kwa namna ya pekee kabisa na watu wa Mungu.

Waamini walei wanaendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko sanjari na kulitegemeza Kanisa mahalia. Askofu mkuu Nkwande anasema, zote hizi ni juhudi za wongofu wa kichungaji, ari na mwamko wa kimisionari unaowasukuma waamini kutoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na kuendelea kupongezana kwa mafanikio makubwa yanayoshuhudiwa na watu wa Mungu nchini Tanzania. Wataalam wa mambo ya imani wanasema, leo hii Tanzania ni kati ya nchi za Kiafrika ambazo lina nguvu sana kutokana na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Wongofu wa kichungaji imekuwa ni chachu muhimu sana katika kukua na kukomaa kwa Kanisa. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya wakleri, watawa na waamini walei wanaotumwa na Kanisa nchini Tanzania kwenda ughaibuni ili kujichotea ujuzi, elimu na maarifa, wanapohitimu masomo yao, watambue kwamba, Kanisa la Tanzania linawasubiri kwa hamu kubwa kuona wanarejea nyumbani, ili kuchangia katika mchakato wa uinjilishaji wa kina, ujenzi wa Kanisa pamoja na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Kwa hakika anasema Askofu mkuu Nkwande kwamba, wasomi wanapaswa kurejea nyumbani kwa furaha na shangwe kwani kwa hakika nyumbani kumenoga!

Wasomi wanaotumwa ughaibuni kutafuta elimu, ujuzi na maarifa watambue na kuthamini sadaka kubwa inayotolewa na watu wa Mungu. Kumbe, wanapaswa kujenga utamaduni wa kusoma kwa bidii, juhudi na maarifa, tayari kurejea nyumbani ili kushiriki katika maendeleo, ustawi na mafao ya watu wa Mungu. Tabia ya kuzamia na kupotelea kusikojulikana ni alama ya kukosa shukrani kwa watu wa Mungu! Askofu mkuu Nkwande anatambua na kuthamini mchango unaoendelea kutolewa na watanzania ambao wanaishi na kufanya utume wao ndani na nje ya Italia kwa idhini ya Maaskofu na viongozi wao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Kuna baadhi ya wakleri na watawa wanaoishi ndani na nje ya Italia kwa sababu ya utume unaotekelezwa na mashirika yao!

Kizaazaa ni wale "wanaopotelea huko kusikojulikana"! Wasomi wajenge tabia ya kumshukuru Mungu kwa elimu, ujuzi na maarifa anayowakirimia, tayari kuwekezwa katika ujenzi wa Kanisa la Mungu, ili kukuza na kudumisha imani sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Wasomi wahimizane kujenga utamaduni wa kurejea nyumbani tangu wanapowasili kwa masomo! Askofu mkuu Renatus Nkwande amesema kwa ujumla hali ya Tanzania ni shwari, kuna amani na utulivu na watu wanasonga mbele na shughuli zao za kila siku! Migogoro na kinzani za kisiasa ni sehemu ya maisha ya binadamu! Lakini, kimsingi, Tanzania kumenoga, yapo mambo makubwa na mazuri yanayoendelea kufanyika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote! Amewashukuru watanzania wanaishi na kusoma Roma kwa moyo wao wa: umoja, upendo na ukarimu, kielelezo na utambulisho wa watanzania sehemu mbali mbali za dunia!

Kwa upande wake, Padre Paschal Ighondo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma, kwa niaba ya watanzania wote, amewashukuru Maaskofu wakuu kwa kuitikia mwaliko wao, ili kuja kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Ujio wao ni neema na baraka kubwa kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Anasema, moyo usio na shukrani unakausha baraka na neema! Watanzania wanawaombea heri na baraka, Maaskofu wakuu wapya, ili waendelee kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ari na moyo mkuu. Umoja huu, umekuwa na mshikamano wa pekee wakati wa raha na majanga ya maisha; kwa kusaidiana kwa hali na mali! Wanafunzi watanzania wanasema, wamekisikia kilio cha Maaskofu kwamba, wanapaswa kufanya tafiti na kuchapisha Maandiko yao, ili yawasidie watu wa Mungu nchini Tanzania wenye kiu ya kutaka kuchota utajiri katika masuala mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa! Muda wa kubweteka na “Macaroni” umekwisha, sasa ni wakati wa kuchakarika, ili kushirikisha ujuzi, maarifa na hekima wanayoendelea kujichotea huku ughaibuni!

Askofu Mkuu Nkwande
03 July 2019, 16:54