Tafuta

Siku za Kuombea Amani Japani kuanzia tarehe 6-15 Agosti: Amani inasimikwa katika: Ukweli, haki, upendo, uhuru, utu na heshima ya binadamu! Siku za Kuombea Amani Japani kuanzia tarehe 6-15 Agosti: Amani inasimikwa katika: Ukweli, haki, upendo, uhuru, utu na heshima ya binadamu! 

Amani ni tunda la maendeleo fungamani ya binadamu!

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika ujumbe wake wa Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kwa mwaka 2019 anasema, amani ya kweli ni matunda ya maendeleo fungamani ya binadamu. Kunako mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Hiroshima, nchini Japani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kuandika na kushuhudia Injili ya amani inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika tunu msingi za Kiinjili yaaani: Ukweli, haki, upendo, uhuru pamoja na utu na heshima ya binadamu. Hii ni misingi inayopambana na vitendo vyote vya kigaidi, vita na machafuko ya aina mbali mbali ambayo kimsingi ni kashfa kubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia kwamba, amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo endelevu ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo!

Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Askofu mkuu Mitsuaki Takami wa Jimbo kuu la Nagasaki ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika ujumbe wake wa Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kwa mwaka 2019 anasema, amani ya kweli ni matunda ya maendeleo fungamani ya binadamu. Kunako mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Hiroshima, nchini Japani. Tangu wakati huo, familia ya Mungu nchini Japan kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti ya kila mwaka imekuwa ikisali kwa ajili ya kuombea amani.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Japani Mwezi Novemba 2019, miaka 38 na miezi tisa tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotoa mwaliko kwa ajili ya Kuombea Amani Hiroshima. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwamba, Baba Mtakatifu Francisko atatumia tena fursa hii kutangaza na kushuhudia Injili ya amani kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu amekuwa mstari wa mbele kukemea kwa “macho makavu kabisa bila hata kupepesa pepesa kope” kuhusu biashara haramu ya silaha duniani inayoendelea kusababisha maafa na majanga makubwa kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana katika mambo muhimu yanayogusa mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa; kwa kusimamia kikamilifu Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani uliotiwa mkwaju hapo tarehe 20 Septemba 2017.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, amani ya kweli kamwe haiwezi kujengwa katika mazingira ya hofu na vitisho. Amani inakita mizizi yake katika haki, maendeleo fungamani ya binadamu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Amani ni chachu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Amani inatabia ya kukoleza demokrasia shirikishi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Amani inasaidia maboresho ya huduma ya elimu na afya bora kwa wananchi wote. Hii ni fadhila inayosimikwa katika majadiliano katika ukweli na uwazi; upendo na mshikamano wa dhati! Askofu mkuu Mitsuaki Takami anasema, vitendo vya kigaidi, mashindano ya utengenezaji wa silaha, ukosefu wa uhakika wa usalama wa mawasiliano ni kati ya mambo ambayo yanatishia usalama na amani duniani, kiasi cha watu kuendelea kuishi katika hofu na mashaka.

Mashindano ya silaha yanayosikika sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha Mataifa makubwa kutaka kupimana nguvu za kijeshi. Vatican ilikuwa ni nchi ya kwanza kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, maendeleo fungamani ya binadamu yanawambata na kuwashirikisha wote pasi na ubaguzi. Kumbe, uchumi, utamaduni, maisha ya kifamilia pamoja na masuala ya kidini, yote yanapewa umuhimu wa pekee katika maisha ya mwanadamu. Hii ni sehemu ya mchakato wa uundaji wa familia ya Mungu inayowajibika. Kwa hiyo ili kuweza kujenga na kudumisha misingi ya amani ya kweli duniani, kuna haja ya kufutilia mbali utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia, ili rasilimali fedha na vitu, iweze kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Askofu mkuu Mitsuaki Takami wa Jimbo kuu la Nagasaki ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, anahitimisha ujumbe wake wa Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kwa mwaka 2019 kwa kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuombea amani duniani na kuendelea kuwa mashuhuda na vyombo vya amani na maendeleo fungamani ya binadamu.

Japan: Amani
19 July 2019, 11:49