Tafuta

Vatican News
WAWATA Jimbo kuu la Arusha nchini Tanzania wamewasha moto wa Injili ya uchumi kwa kuzindua kiwanda cha kutengeneza sabani. WAWATA Jimbo kuu la Arusha nchini Tanzania wamewasha moto wa Injili ya uchumi kwa kuzindua kiwanda cha kutengeneza sabani.  (AFP or licensors)

WAWATA Jimbo kuu la Arusha wawasha moto wa Injili ya uchumi!

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, imetakiwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu aliyewaumba kwa sura na mfano wake, anayewalinda na kuwategemeza katika maisha na shughuli zao mbali mbali; Mungu anayewaongoza kuelekea kwenye utimilifu na utakatifu wa maisha. WAWATA wakite maisha yao katika Sala: Kusifu, kuomba, kutukuza na kushukuru.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania, ameitaka Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu aliyewaumba kwa sura na mfano wake, anayewalinda na kuwategemeza katika maisha na shughuli zao mbali mbali. Mwenyezi Mungu ndiye anayewongoza kuelekea kwenye utakatifu wa maisha. Amewataka WAWATA kukita maisha yao katika Sala: Kusifu, kuomba, kutukuza na kushukuru. Changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, kama waamini wanajenga na kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, awawezeshe kutekeleza vyema dhamana, majukumu na utume wao katika: familia, Kanisa na jamii katika ujumla wake. Bila kujiaminisha na kumtegemea Mwenyezi Mungu, yote ni bure.

Askofu mkuu Massawe ameyasema haya hivi karibuni wakati alipokua anazindua Mradi wa Kutengeneza Sabuni, uliobuniwa na kutekelezwa na WAWATA Jimbo kuu la Arusha kwa mtaji wa shilingi milioni 50, lakini hadi wakati huu, kiasi cha shilingi milioni 45 kimekwisha kusanywa kutoka kwa Wanawake Wakatoliki Jimbo kuu la Arusha. Mtaji huu ni mchango wa shilingi milioni moja kutoka katika kila Parokia pamoja na vikundi 21 vya wanachama waanzilishi wa mradi. WAWATA Jimbo kuu la Arusha wanasema, mradi huu ni utajiri na hazina kubwa katika mchakato wa kuwajengea wanawake uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao, ili kweli Jimbo kuu la Arusha nchini Tanzania liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi pamoja na kuendelea kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu.

“Tutumikie na kuwajibika” ndiyo kauli mbiu inayoongoza Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ambacho ni chombo kinachowaunganisha wanawake Wakatoliki Tanzania. WAWATA ilianzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kuwapatia wanawake fursa ya kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimengu kwa chachu ya tunu msingi za Kiinjili. Kila mwanamke Mkatoliki ni mwanachama wa WAWATA. Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni maendeleo, ustawi na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. WAWATA katika kipindi cha miaka 47 ya uhai na utume wake imekuwa mstari wa mbele kuwaendeleza wanawake:kiroho na kimwili ili waweze kutoa mchango wao kikamilifu katika: kujiendeleza na kujitegemea; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu: kiroho, kimwili.

WAWATA pia imendelea kuwajengea wanachama wake uwezo wa kiuchumi na kwa ajili ya ustawi wa familia zao, Kanisa na jamii katika ujumla wake. WAWATA imeendelea kuwaimarisha wanawachama wake katika misingi ya: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili pamoja na Sala kwa njia ya Ibada, Tafakari ya Neno la Mungu, Mafungo, Makongamano pamoja na hija mbali mbali ndani na nje ya Tanzania. WAWATA imekuwa mstari wa mbele kuwajengea uwezo wanawake na wasichana kwa njia ya mikopo na miradi midogo midogo, miradi ya kati na kwa sasa wanaanza kujielekeza kwenye miradi mikubwa zaidi, ili kujijenga zaidi kiuchumi na kuwa na nguvu ya kimaadili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha na hatimaye, kuchangia mchakato wa kuzitegemeza familia zao, kuendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia pamoja na jamii katika ujumla wake.

Mradi wa Kutengeneza Sabuni uliozinduliwa rasmi na Askofu mkuu Isaac Amani Massawe pamoja na mambo mengine, unapania kuwajengea uwezo wa kiuchumi wasichana na wanawake walioolewa katika umri mdogo pamoja na wajasiriamali wanaotaka kuboresha zaidi maisha yao. Pili, mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya Serikali ya Awamu ya tano inayopania kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda. Katika hili, Askofu mkuu Isaac Amani Massawe amewataka WAWATA kuwajibika barabara kwa kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa. Kwa kujikita katika ukweli na uwazi; uaminifu na uadilifu; ulinzi na usalama wa mali ya kiwanda. Kimsingi kila mfanyakazi kiwandani hapo atekeleze vyema dhamana na wajibu wake, kwa kujiaminisha kwanza kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu, huku wakizingatia kanuni maadili na utu wema.

Lengo ni kuwawezesha walengwa wakuu kuweza kufaidika na matunda ya kazi na jasho lao, huku wakiendelea kumshukuru Mungu chemchemi ya wema na utakatifu wa maisha! Mradi ukikomaa, utasaidia kupunguza michango kutoka kwa wanawake na wasichana. Ufunguzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Sabuni cha WAWATA Jimbo kuu la Arusha ilikuwa ni sehemu ya matukio muhimu ya Semina ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, wanaounda Kanda ya Kaskazini inayoshirikisha Majimbo ya Same, Moshi, Mbulu na Jimbo kuu la Arusha. Semina hii ilifunguliwa hapo tarehe 12 na kuhitimishwa tarehe 14 Julai 2019 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Isaac Amani Massawe kwenye Parokia ya Roho Mtakatifu, Ngarenaro. Mada zilizojadiliwa kwenye semina hii ni pamoja na: Elimu ya kuitikia wito wa kuyatakatifuza malimwengu iliyotolewa na Padre Festo Mangwangi.

Mada ya pili ilikuwa ni “Huduma kwa familia zinazoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi”, mada ambayo imewasilishwa na Padre Raphael Madinda, Katibu mtendaji, Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Mada ya tatu ilikuwa ni “Afya bora ya Dunia inatutegemea sote”. Hii ni mada iliyochambuliwa na mwamini mlei Mama Evaline Ntenga, kiasi cha kuleta mvuto mkubwa kwa wasikilizaji wake kwa jinsi alivyopembua na kuchambua kwa kina na mapana Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” mintarafu hali halisi ya maisha ya wanawake wa Tanzania. Amesema, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya utekelezaji wa misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii na kwamba, hii ni dhamana inayowawajibisha watu wote, kila mtu kadiri ya uwezo na nafasi yake.

Hii ni mada ambayo licha ya kuchota utajiri wake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Mafundisho Jamii ya Kanisa na jinsi ya kumwilisha mafundisho haya katika uhalisia wa familia ya Mungu nchini Tanzania katika ujumla wake, mada hii imechota pia amana na utajiri kutoka katika Furaha ya Injili na Uumbaji, kauli mbiu iliyoongoza Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2017 kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika ujumbe huu, Maaskofu kwa namna ya pekee wanapembua juu ya dhambi ya asili na matokeo yake kwa mwanadamu na maumbile. Maaskofu wanazungumzia juu ya Uumbaji unavyoshirikishwa katika kazi ya Ukombozi wa mwnadamu; wanakazia kwa namna ya pekee kwamba, utunzaji bora wa mazingira kuwa ni kazi mahususi ya mwanadamu!

Dhambi kimsingi haipatani kabisa na utakatifu na ukamilifu wa Mungu, kwani dhambi ni giza wakati Mungu ni mwanga, hapa changamoto kwa waamini ni kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa kiekolojia. Waamini wanakumbushwa kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya matendo ya huruma yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

WAWATA: Arusha
17 July 2019, 15:55