Askofu mkuu Gervas Nyaisonga katika tafakari kuhusu Daraja Takatifu anawakumbusha kutafakari kuhusu: Vigezo vya Mungu; Udhaifu na Utume katika Neno, Sakramenti na huduma! Askofu mkuu Gervas Nyaisonga katika tafakari kuhusu Daraja Takatifu anawakumbusha kutafakari kuhusu: Vigezo vya Mungu; Udhaifu na Utume katika Neno, Sakramenti na huduma! 

Askofu mkuu Nyaisonga: Vigezo vya Upadre? Udhaifu na Utume!

Mapadre kumbukeni kuhusu:Uteuzi wenu na vigezo vilivyozingatiwa na Mungu. Wtambue na kukiri udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu tayari kuambata utakatifu. Mapadre wanatumwa kutangaza Neno la Mungu, Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na Kumwilisha Injili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu wanaowahudumia!

Na Thompson Mpanji, Mbeya & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Daraja Takatifu ni Sakramenti ambayo kwayo, utume uliokabidhiwa na Kristo Yesu kwa Mitume wake huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati. Hivyo, basi, hii ni Sakramenti ya huduma ya kitume nayo ina ngazi kuu tatu: yaani: Uaskofu, Upadre na Ushemasi kadiri ilivyofafanuliwa na Baba wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mapadre kwa mamlaka wanayokabidhiwa na Mama Kanisa wanakuwa ni wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma yanayotekelezwa katika maeneo yao. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hutenda kwa nafsi ya Kristo na kutangaza Fumbo lake; huyaunganisha maombi ya waamini na Sadaka ya Kristo Msalabani, inayoadhimishwa kila siku katika Ibada ya Misa Takatifu.

Ni daraja linalowataka kujenga na kuimarisha umoja kati yao kama Mapadre pamoja na Askofu wao mahalia. Mapadre wanapaswa kuadhimisha na kugawa Mafumbo ya Kanisa kwa imani, uchaji na ibada! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakumbusha kwamba, Mapadre wanatwaliwa katika wanadamu na kuwekwa kwa ajili ya wanadamu wenyewe katika mambo yamhusuyo Mungu, ili watoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; nao wanaishi kati ya wanadamu wengine kama ndugu. Maana ndivyo alivyoishi Yesu aliye Bwana na Mwana wa Mungu, mtu aliyetumwa na Baba wa milele kwa wanadamu, ambaye alikaa nao, akataka kuwa sawa na ndugu zake katika mambo yote, isipokuwa dhambi. Kimsingi Mapadre anateuliwa kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, kumbe, wanapaswa kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Vatican News katika mahojiano maalum na Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kuhusu Daraja Takatifu ya Upadre anasema, familia ya Mungu inapaswa kutambua kwamba, Daraja takatifu ya Upadre ni zawadi na kila Padre ni zawadi ya Mungu kwa ajili ya Kanisa. Waamini waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu ili alijalie Kanisa: Mapadre wema, watakatifu na wenye bidii, ari na moyo wa kichungaji. Wasali na kumwomba Bwana wa mavune apeleke watenda kazi katika shamba lake. Hawa ni Mapadre kwa ajili ya Majimbo mbali mbali, Mapadre wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na kuombea karama mbali mbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Mungu. Tafakari kuhusu maisha, wito na utume wa iwe ni fursa kwa wanadaraja wenyewe kujichunguza na kuangalia wameishije wito, wakfu na utume wao kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Pale walipofanya vyema, wamshukuru Mungu, pale walipoteleza na kuanguka, waombe neema ya toba na wongofu wa ndani na msamaha ili kuanza tena upya! Ni nafasi kwa familia ya Mungu katika ujumla wake kujipima na kuangalia uhusiano wake na Mapadre wao katika ujumla wao; katika malezi na makuzi; katika ushirikiano na mshikamano kwenye kazi na utume. Waamini wawe mstari wa mbele kuwakumbuka, kuwaombea na, kuwaenzi na kuwategemeza Mapadre kwa hali na mali, ili waweze kutekeleza vyema dhamana, wajibu na utume wao katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, huku wakisaidiana na Maaskofu wao mahalia! Mapadre wanahimizwa kukuza na kudumisha fadhila zinazoheshimiwa katika jamii ya kibinadamu, kama vile: wema wa moyo, unyofu, uthabiti wa roho na saburi, juhudi kwa ajili ya haki, ukarimu, na fadhila nyingine anazokazia mtume Paulo asemapo, “Mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo” (Flp 4:8).

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, hivi karibuni ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Daraja Takatifu kwa Mashemasi: Alex Mwampashe pamoja na Benedikto Mwamlima. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Parokia ya Mtakatifu Petro Claver, Mlowo, Jimbo Kuu la Mbeya. Katika tafakari na wosia wake kwa Mapadre wote, lakini hasa kwa Mapadre wapya, amewataka kukumbuka daima mambo makuu matatu: kwanza ni kuhusu uteuzi wao na vigezo vilivyozingatiwa na Mwenyezi Mungu; watambue na kukiri udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu tayari kuambata utakatifu wa maisha na tatu, kama Mapadre wanatumwa kutangaza Neno la Mungu, Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na Kumwilisha Injili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu wanaowahudumia!

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga amewataka wakleri na watawa kuonesha unyenyekevu mkuu kwani hawajui ni vigezo gani ambavyo vimemsukuma Mwenyezi Mungu hata akawateuwa kuwa ni wahudumu wa Neno, Sakramenti na huduma ya upendo kwa waja wake. Walimwengu wanateuwa wafanyakazi wao kwa kuzingatia kigezo cha: elimu, uzoefu kazini na uhodari. Kimsingi kila kazi ina sifa na vigezo vyake vinavyopaswa kuzingatiwa na kufuatwa kikamilifu. Lakini kwa wito na maisha ya Daraja Takatifu mambo ni tofauti sana, kwani Mwenyezi Mungu anawatambua waja wake kutokana na udhaifu wao, ndiyo maana anawakabidhi hazina na amana kubwa katika vyombo vya udongo, ili kuendeleza kazi ya ukombozi! Ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu huu nyeti, wanapaswa kuwa ni watu wa Sala, wanaotafakari kwa kina na mapana Neno la Mungu na kujitahidi kulimwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wao!

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga anawataka wajitahidi kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti za Kanisa. Daima wakleri na watawa waoneshe juhudi na bidii ya kumtafuta na kumwambata Kristo Yesu kwa njia ya Kanisa lake. Wajenge na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano na Askofu wao mahalia. Wakuze na kuimarisha umoja wa wakleri pamoja na kushikamana na taifa la Mungu kama Mababa wa Mtaguso wa Pili wa Vatican wanavyofafanua na kukazia zaidi, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kutakasa na kuwaongoza watu wa Mungu, huku wakiwa wameungana na Askofu wao mahalia. Mapadre wasaidiane katika mambo ya kiroho na kimwili; katika shughuli za kichungaji, ili hatimaye, kukuza na kudumisha umoja na upendo katika maisha. Mapadre wawe na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwateuwa bila hata ya wao wenyewe kufahamu vigezo alivyotumia!

Wasijivunie wito na maisha ya Upadre, bali watekeleze yale ambayo Mwenyezi Mungu anataka kutoka kwao kama Mapadre. Lengo la Daraja Takatifu ya Upadre ni kuendeleza kazi ya ukombozi. Wameteuliwa si kwa sababu wana akili nyingi kuliko vijana wengine wote Jimbo kuu la Mbeya au kwa sababu nyingine yoyote ile! Mwenyezi Mungu amewateuwa jinsi walivyo kwa kutambua udhaifu wao wa kibinadamu na amewakabidhi dhamana na jukumu la kuendeleza. Wameteuliwa na kuwekwa wakfu ili kutangaza Neno la Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko wa maisha yao. Wanahimizwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa kwa ari, moyo mkuu, unyenyekevu, ibada na majitoleo thabiti. Mapadre ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika huduma makini kwa waja wake.

Daima wakumbuke kwamba, amana na utajiri wa Daraja Takatifu unahifadhiwa katika chombo cha udongo, katika udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, lakini, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuambata utakatifu wa maisha. Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga amewapongeza waamini walei wanaojibidisha kusali Sala ya Kanisa pamoja na familia zao, lakini wakleri na watawa watambue kwamba, wanfungwa kisheria kusali Sala ya Kanisa. Mapadre na wakleri pamoja na watu wote wa Mungu anasema Askofu mkuu Nyaisonga waendelee kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Daraja Takatifu



13 July 2019, 16:43