Tafuta

Vatican News
Utume wa Wakarismatiki Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kuanzia tarehe 7 Juni hadi 30 Juni 2019 unaadhimisha Kongamano la Roho Mtakatifu: Miaka 50 Halmashauri Walei Tanzania Utume wa Wakarismatiki Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kuanzia tarehe 7 Juni hadi 30 Juni 2019 unaadhimisha Kongamano la Roho Mtakatifu: Miaka 50 Halmashauri Walei Tanzania 

Kongamano la Roho Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania

Utume wa Wakarismatiki Wakatoliki, Jimbo kuu la Dar es Salaam nchini Tanzania umeandaa kongamano linalofunguliwa na Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Ijumaa tarehe 7 Juni 2019, majira ya saa 6:00 kwa saa za Afrika Mashariki, kwenye Viwanja vya Kituo cha Emaus, Ubungo. Kongamano hili litahitimishwa tarehe 30 Juni 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika mapambazuko ya millennia ya tatu ya Ukristo, waamini wanahamasishwa zaidi na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha! Ni kipindi cha kujikita katika majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika maisha ya sala, kwa kushirikiana na waamini wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo ili kuweza kuombea umoja wa Kanisa. Ni muda wa kushikamana katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa.

Jubilei ya Miaka 50 ya Wakarismatiki Wakatoliki, ilikuwa ni fursa ya kumwimbia Mungu, Roho Mtakatifu utenzi wa shukrani kwa neema na baraka zake kwa Kanisa la Kristo, kwani Chama hiki kimetoa fursa kwa waamini kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao kwa njia matendo ya huruma. Maaskofu, Mapadre na viongozi mbali mbali wa Kanisa wanakumbushwa kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kuwalea, kuwaongoza na kuwasaidia Wakarismatiki kuweza kujitambua, kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu zinazotolewa na Mama Kanisa kwa waja wake.

Kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2019, Utume wa Wakarismatiki Wakatoliki, Jimbo kuu la Dar es Salaam nchini Tanzania umeandaa kongamano linalofunguliwa na Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Ijumaa tarehe 7 Juni 2019, majira ya saa 6:00 kwa saa za Afrika Mashariki, kwenye Viwanja vya Kituo cha Emaus, Ubungo. Kongamano hili litahitimishwa tarehe 30 Juni 2019. Jimbo kuu la Dar es Salaam, limeandaa Makongamano kumi na moja katika Dekania 10 zinazounda Jimbo kuu la Dar es Salaam. Katika kipindi chote hiki, mahubiri yataanza saa 8:00 mchana hadi 12:00 jioni na wahubiri ni Mapadre kutoka ndani na nje ya Tanzania pamoja na waamini walei, wanaoitwa na kutumwa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kongamano la Roho Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam linaongozwa na kauli mbiu “Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi. Na katika mahali hapa nitawapa amani” ( Hagai 2:9). Katika mahojiano maalum na Vatican News Eleuter Augustine Mange, Katibu Karimastiki Katoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam anasema, Kongamano la  Roho Mtakatifu ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania yanaongozwa na kauli mbiu “Kuyatakatifuza Malimwengu”. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania yalizinduliwa rasmi na Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hapo tarehe 16 Juni 2018.

Waamini walei wanamahasishwa kushiriki kwa dhati kabisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Watambue haki na wajibu wao katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Wanayo dhamana ya kuinjilisha kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko na kwamba, wanatumwa kuyatakatifuza malimwengu, kwani upendo wa Kristo unawawajibisha. Waamini walei wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Utume wao uonekane katika Jumuiya za Kikristo, katika familia na hata katika mazingira ya kijamii: kitaifa na kimataifa!

Jambo la msingi kwa waamini walei ni kuhakikisha kwamba, wanashikamana na viongozi wao wa Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Halmashauri Walei Tanzania, tarehe 16 Juni 2019 inaadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969 na Hayati Askofu James Sangu aliyekuwa Mwenyekiti Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kumbe, kuanzishwa kwa Halmashauri Walei Tanzania ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Huo ukawa ni mwanzo wa Baraza la Walei ambalo baadaye mwaka 1983 lilifanyiwa marekebisho na kutambulikana kama Halmashauri ya Walei Tanzania.

Dar es Salaam
06 June 2019, 12:34