Tafuta

Fumbo la Pentekoste linaendelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwani Kanisa ni ushirika katika Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana anayeabudiwa na Baba na Mwana. Fumbo la Pentekoste linaendelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwani Kanisa ni ushirika katika Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana anayeabudiwa na Baba na Mwana. 

Sherehe ya Pentekoste: Roho Mt. katika maisha na utume wa Kanisa

Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni jina halisi la yule ambaye tunamwabudu na kumtukuza pamoja na Baba na Mwana. Kanisa limempokea Roho Mtakatifu kutoka kwa Bwana na linamuungama katika ubatizo wa watoto wake wapya. Roho Mtakatifu anaitwa pia mfariji, msaidizi, mtakasa, Roho wa Bwana, kidole cha Mungu na Roho wa Mungu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha sherehe ya Pentekoste, sherehe ya ujio wa Roho Mtakatifu katika Kanisa, sherehe ambayo inahitimisha kipindi cha siku 50 za Pasaka. Katika siku hii ya leo Kanisa la Tanzania linaadhimsha Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri ya Walei Tanzania. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kuyatakatifuza malimwengu”.

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mdo. 2:1-11) ni kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume. Ni somo linaloelezea tukio la ujio wa Roho Mtakatifu kama lilivyotokea Yerusalemu. Tukio hili liligongana na siku ambayo wayahudi walikuwa wakifanya sherehe ya vibanda au sherehe ya Pentekoste ya Wayahudi. Hii ilikuwa ni sherehe yao ya shukrani kwa mavuno na waliadhimisha siku waliyopokea Agano mlimani Sinai. Hii ndiyo siku ambayo mitume wanampokea Roho Mtakatifu na ni siku ambayo Kanisa linazaliwa. Kugongana kwa ujio wa Roho Mtakatifu ambao ni siku Kanisa lilipozaliwa na sherehe ya Wayahudi ya Pentekoste na ya Agano ni alama kuwa Kanisa hili ndio matunda au mavuno ya kwanza ya Kristo Mfufuka na pia kuwa Kanisa ndiyo jumuiya mpya ya watu wa Agano na Mungu.

Somo linaonesha pia kuwa katika siku hii unatokea muujiza wa kunena kwa lugha. Muujiza huu wa kwanza wa Roho Mtakatifu katika kitabu cha Matendo ya Mitume unakuwa ni wa kunena kuashiria kuwa wito wa kwanza wa kanisa, wito wa kwanza wa mitume ni kunena au kutangaza Habari Njema na hivi kumshuhudia Kristo Mfufuka. Wananena kwa lugha ambayo kila mmoja anaelewa katika lugha yake mwenyewe. Hiki kinakuwa pia kiashiria kingine cha kusambaa kwa Kanisa. Ushuhuda wa Habari Njema unaolitoa Kanisa utawafikia watu wa lugha zote na kabila zote nao wataupokea kwa lugha zao wenyewe, kuuelewa na kuuishi katika tamaduni zao njema. Na katika hayo, yatatangazwa matendo makuu ya Mungu.

Somo la pili (Rum 8:8-17 ) ni kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika sura ya 8 ya waraka huu, mtume Paulo anaelezea ubinadamu mpya wa wakristo, ubinadamu unaotokana na Roho Mtakatifu. Anaonesha kuwa ubinadamu unaoishi chini ya dhambi ni ubinadamu unaomweka mwanadamu katika utumwa bali ule unaoishi katika Roho Mtakatifu unamweka katika uhuru. Ule wa kwanza, wa kuishi katika dhambi ni ule wa kuishi kwa kufuata vionjo vya mwili na huo anasema haumpendezi Mungu. Ule wa pili wa kuishi katika Roho unampendendeza Mungu.

Katika somo hili Mtume Paulo anaongeza kuonesha faida ya uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya maisha ya mwamini. Faida hiyo ni kwamba Roho huyu humfanya mwamini kuwa mwana wa Mungu vile vile kama Kristo alivyo Mwana wa Mungu. Na uthibitisho wa kuwa mwamini anafanyika mwana wa Mungu ni kuwa kwa njia ya Roho yeye naye anawezeshwa kumwita Mungu vile vile kama Kristo alivyomwita. Kristo anamwita Mungu “Abba” yaani baba na mwamini aliye na Roho Mtakatifu naye anawezeshwa kumwita Mungu “Abba” yaani Baba. Kumbe, kwa njia ya Roho huyu sisi ni warithi pamoja na Kristo wa ule uwana wa Mungu.

Injili (Yoh 14, 15-16, 23b-26) Injili ya leo Kutoka kwa mwinjili Yohane inaelezea kazi za Roho Mtakatifu kwa jumuiya ya waamini na kwa kila mwamini. Yesu akiwa katika karamu ya mwisho na wanafunzi wake anawaahidi ujio wa Roho Mtakatifu. Ni Roho anayekuja kwao kama msaidizi, kuwasaidia na kukaa nao milele. Roho huyu atakuja kuwafundish, yaani atakuwa kuwafafanulia kikamilifu Neno la Kristo na mafundisho yake yote aliyowapa alipokuwa nao. Ni Roho abaye pia atawakumbusha, yaani atafanya hai daima ndani yao uwepo wa Kristo na uwepo wa nguvu yake inayookoa. Ndivyo ambavyo kwa njia ya Roho Mtakatifu Kristo anakuwa hai katika maadhimisho ya sakrameti na katika liturujia ambazo Kanisa linaziadhimisha.

Katika Injili hii Kristo anawaalika wanafunzi wake kumtambua Roho Mtakatifu kama kigezo cha kumpokea. Anawaambia “ulimwengu hauwezi kumpokea Roho Mtakatifu kwa sababu haumtambui; bali ninyi mnamtambua kwa sababu anakaa kwenu.” Kumtambua Roho Mtakatifu na kufanya makazi yake ndani ya nafsi ya mwamini ni muhimu ili kumpokea Roho mwenyewe.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Sherehe ya Pentekoste ni adhimisha llinalohitimisha kipindi cha Pasaka ya Kristo kwa kumminina Roho Mtakatifu ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama nafsi ya Mungu. Ni siku ya kutafakari juu ya uwepo wa Roho Mtakatìfu katika Kanisa na katika maisha ya waamini na ni siku ya kuomba kuimarishwa kwa  mapaji yake saba na kujazwa na matunda yake ambayo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi kama anavyofundisha mtume Paulo (Rej. Gal 5:22).

Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja. Ni jina halisi la yule ambaye tunamwabudu na kumtukuza pamoja na Baba na Mwana. Kanisa limempokea Roho Mtakatifu kutoka kwa Bwana na linamuungama katika ubatizo wa watoto wake wapya.  Licha ya jina lake hili halisi, Roho Mtakatifu anaitwa pia mfariji, msaidizi, mtakasa, Roho wa Bwana, kidole cha Mungu na Roho wa Mungu. Roho Mtakatifu yupo tangu hata kabla ya nyakati akitenda kazi katika umoja na Baba na Mwana. Utume wake huu hata hivyo ulibaki umejificha hadi ulipowadia utimilifu wa nyakati alipomininwa ulimwenguni. Roho Mtakatifu amekuwapo katika uumbaji ikitulia juu ya uso wa maji (Mwa 1:2). Ameshiriki kumuumba mwanadamu pamoja na vitu vyote.

Mtakatifu Ireneo anasema “Mungu amemuumba mwanadamu kwa mikono yake mwenyewe yaani Mwana na Roho Mtakatifu na juu ya mwili ulioumbwa alitengeneza sura yake mwenyewe hivi kwamba kile kilichoonekana kilichukua sura ya Mungu” (Rej. KKK 704). Ni Roho Mtakatufu aliyewaongoza Waisraeli kutoka Misri kueelekea nchi ya ahadi, mchana akiwa mbele yao kama wingu na usiku kama mnara wa moto. Roho huyu ndiye aliyenena kwa vinjwa vya Manabii akiwafundisha kulishika Agano na kumtumainia masiha ajaye.

Wakati wa kuja kwake Masiha ni Roho huyu aliyemtayarisha Bikira Maria kwa neema yake ili awe “amejaa neema”. Ndani ya Bikira Maria ni Roho Mtakatifu aliyetekeleza mpango wa Baba uliojaa upendo wa kuzaliwa duniani Mwanae wa Pekee. Katika Maria, Roho Mtakatifu alimdhihirisha mwana wa Baba aliyefanyika mwili: na kwa njia ya Maria Roho Mtakatifu akaanza kuwaweka watu katika ushirika pamoja na Kristo ambao ndio lengo la pendo la huruma ya Mungu. Kristo mwenyewe ametekeleza utume wake katika ushirika na Roho Mtakatifu. Baba alimpaka mafuta kwa Roho Mtakatifu alipobatizwa Yordani na kumuongoza daima.

Naye Kristo ndiye aliyemfunua Roho Mtakatifu na kummimina kwa wanafunzi wake na kwa Kanisa lake katika utimilifu wa nyakati, adhimisho tunalolifanya katika Pentekoste hii. Jambo moja kati ya mengi tunayoweza kutafakari leo kumhusu Roho Mtakatifu ni lile la umoja linalooneshwa na somo la kwanza. Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume katika umoja wao na tangu hapo alama wazi ya uwepo halisi wa Roho Mtakatifu ni umoja. Roho Mtakatifu ni Roho anayewaunganisha watu katika Kanisa na ndani ya Kanisa kama jumuiya ya waamini. Tunapomwadhimisha na kumshukuru Roho Mtakatifu kwa uwepo wake katika maisha yetu tuombe kuongozwa na dhamira ya umoja. Ndani ya Roho Mtakatifu tuulinde umoja wa Kanisa; ndani ya Kanisa na kwa jina la Kanisa.

Liturujia: Pentekoste
07 June 2019, 13:35