Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Mtakuwa ni mashahidi wangu! Liturujia ya Neno la Mungu: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Mtakuwa ni mashahidi wangu! 

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Mtakuwa ni mashahidi wangu!

Fumbo hili la kupaa Bwana ni fumbo linalohusiana kwa ukaribu sana na fumbo la ukombozi wetu. Linatuonesha kutukuzwa kwa Kristo baada ya kukamilisha kazi ya ukombozi na kiashirio kuwa huko alikoenda yeye ambaye ni kichwa cha Kanisa, ndipo uliko pia mwisho wetu sisi sote tunaomwambini na tulio sehemu ya mwili wake wa fumbo. Ni kumbu kumbu ya hatima ya maisha yetu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Dominika ya leo ni sherehe ya Kupaa Bwana. Siku 40 baada ya kufufuka, Kristo,  mbele ya macho ya wanafunzi wake, anapaa mbinguni kurudi kwa Baba na huko anaketi mkono wake wa kuume. Dominika hii pia bi Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya unaongozwa na kauli mbiu "Kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo" (Efe. 4:25): Kutoka Jumuiya ya mtandaoni kwenda kwenye Jumuiya halisi ya watu! Hii ni changamoto ya ujenzi wa Jumuiya halisi ya binadamu! Na kwa ujumbe huu Baba Mtakatifu Francisko anatualika kutumia mitandao ya kijamii katika namna inayojenga jumuiya halisi yenye ubinadamu.

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mdo. 1:1-11) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Hiki ni kitabu ambacho tumekuwa tunakisoma katika kipindi chote cha Pasaka na kimetuonesha namna ukristo ulivyokuwa na kusambaa baada ya kifo na ufufuko wa Kristo. Somo la leo linaturudisha mwanzoni kabisa mwa kitabu hiki. Ni katika mwanzo huu tunaona kusudio la msingi la kitabu cha Matendo ya Mitume. Kwanza ni kitabu kilichoandikwa kama mwendelezo wa Injili ya Luka. Kitabu cha kwanza tunachosikia kinazungumziwa sio kingine bali ni Injili ya Luka. Kama ambavyo Injili ya Luka ilieleza yote ambayo Yesu alifanya na kufundisha alipokuwa na wanafunzi wake, kitabu hiki kinaeleza yote ambayo wanafunzi wake waliendeleza baada ya yeye kuondoka, kupaa kurudi kwa Baba.

Kabla ya kupaa, Kristo mfufuka aliendelea kuwatokea kwa muda wa siku 40. Namba 40 imetumika daima katika Biblia kama kipindi cha kujitakasa, kujitenga na kujiandaa kwa tukio maalumu. Kwa siku hizi Kristo anawaandaa wanafunzi wake kuuanza utume wa kumshuhudia – “nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu na katika Uyahudi wote na Samaria na hata miisho ya dunia”. Hata hivyo Yesu anawaambia watapokea nguvu akishawajilia Roho Mtakatifu. Ni katika mazingira haya Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaeleza tukio la Kupaa Bwana. Ni tukio linalohitimisha kazi ya ukombozi ya Kristo hapa duniani, anarudi kwa Baba kule alikokuwako mwanzo. Ni tukio linaloashiria mwanzo wa utume mpya wa Kanisa na wa wanafunzi wote wa Kristo kuwa baada ya kumpokea Roho Mtakatifu wanakuwa mashahidi wake. Kupaa Bwana ni tukio la kieskatolojia, tukio linalohusisha mwisho wa nyakati kuwa kwa jinsi Yesu alivyopaa kwenda mbinguni ndivyo atakavyorudi.

Somo la pili (Ebr 9:24-28, 10:19-23 ) ni kutoka Waraka kwa Waebrania.  Katika somo hili, tukio la kupaa Bwana linalinganishwa na tendo la kiibada walilokuwa wakifanya makuhani wa Agano la Kale, kuingia patakatifu pa patakatifu. Katika hekalu la kiyahudi palikuwa na chumba kilichotengwa, chumba kitakatifu kuliko vyote ambacho kuhani mkuu peke yake aliingia mara moja tu kwa mwaka kwa ajili ya kutolea sadaka kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote. Kitabu hiki kinaonesha kuwa Yesu ambaye ndiye Kuhani Mkuu wa Agano Jipya na la milele kwa kupaa kwake ameingia pale patakatifu halisi. Sio katika chumba kilichotengenezwa na mikono ya binadamu bali pale alipo Mungu mwenyewe, Mtakatifu wa watakatifu. Haingii na damu ya wanyama bali na damu yake mwenyewe na wala haingii mara moja tu kwa mwaka bali anaketi huko milele.

Kwa jinsi hii nguvu ya sala yake kwa Mungu ni kubwa kuliko ile ya makuhani wa Agano la Kale. Wao walifanya ibada kwa alama na ishara bali yeye ameifanya ibada halisi. Kwa jinsi hiyo tendo la kupaa Bwana ni tendo linalowapa waamini ujasiri kuwa kwa njia ya Kristo wote wanapata nafasi ya kuingia katika patakatifu pa patakatifu. Wanapata nafasi kwa sababu ya kibali cha damu ya Kristo. Damu ya Kristo imemwagika kwa ajili ya wote na wote wanaoipokea na kuenenda katika ushujaa wa maisha ya kikristo, wanaolishika ungamo la imani kwa tumaini na kutokugeuka wanatiwa muhuri wa damu yake na kustahilishwa kuingia kule ambako Kristo mwenyewe ameingia, yaani mbinguni kwa Baba.

Injili (Lk. 24:46-53) Injili ya leo ni kadiri ya mwinjili Luka. Ni injili inayochukua dhamiri ya somo la kwanza kuwa kupaa Bwana ni kiashirio cha mwanzo wa utume na maisha mapya kwa wanafunzi wa Yesu. Yesu anapopaa anawaachia wanafunzi wake wajibu wa kuendeleza yote aliyowafundisha na wajibu wa kushuhudia yote aliyoyafanya hadi kifo chake msalabani. Ni mwanzo wa maisha ya kuwa Mashahidi. Katika Injili inatajwa pia ahadi ya Baba. Hii ni ahadi ya Roho Mtakatifu. Yesu anawaagiza wanafunzi wake kuwa kabla hawajaanza rasmi utume wao wasubiri: anasemaa “kaeni humu mjini hadi mvikwe uwezo kutoka juu”. Uwezo huu ni ule wa Roho Mtakatifu. Wanafunzi wanapoambiwa kukaa na kusubiri kuvikwa uwezo wa Roho Mtakatifu walikaa wakisubiri kwa kukesha na kusali naq hii ndiyo inayokuwa Novena ya kwanza ya Roho Mtakatifu au novena ya Pentekoste.

Ndiyo maana baada ya Sherehe ya Kupaa Bwana huanza mara moja Novena ya Roho Mtakatufu inayomalizika siku ya Pentekoste. Novena hii ndiyo imekuwa mama wa novena zote katika Kanisa, kipindi cha sala ya mfululizo cha siku 9 kwa ajili ya nia maalumu ya mwombaji au ya waombaji. Tendo hili la kupaa Bwana halikuwahuzunisha Mitume, walirudi Yerusalemu kwa furaha kuu wakimsifu Mungu kwa sababu imani yao ilikuwa tayari imeimarika na matumaini ya kumpokea Roho Mtakatifu yaliwapa nguvu daima.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika kanuni ya imani Katoliki tunasadiki kuwa Yesu Kristo baada ya ufufuko wake “akapaa mbinguni ameketi kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi na toka huko atakuja kuwahukumu walio hai na wafu nao ufalme wake hautakuwa na mwisho”.  Leo ni siku ya kuiadhimisha kiri hii ya imani yetu. Fumbo hili la kupaa Bwana ni fumbo linalohusiana kwa ukaribu sana na fumbo la ukombozi wetu. Linatuonesha kutukuzwa kwa Kristo baada ya kukamilisha kazi ya ukombozi na kiashirio kuwa huko alikoenda yeye ambaye ni kichwa cha Kanisa, ndipo uliko pia mwisho wetu sisi sote tunaomwambini na tulio sehemu ya mwili wake wa fumbo.

Ni adhimisho linalotukumbusha kwa mara nyingine tena kuwa hatima ya maisha ya binadamu haipo hapa duniani bali ipo katika makao ya Baba, kule alikotangulia kwenda Kristo Bwana wetu. Fundisho hili linaendana pia na dhamira ya Baba Mtakatifu Fransisko kwa Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, Kanisa linasifu hatua iliyopigwa katika maendeleo ya mifumo ya mawasiliano hasa katika mitandao ya jamii. Hata leo linazidi kukumbusha kuwa iko hatari ya mitandao hii kutuondoa katika maisha halisi ya kibinadamu na kutubakiza katika jumuiya hewa za mitandaoni. Anakazia Papa Francisko kuwa kasi ya mawasiliano katika mitandao ya kijamii itusukume zaidi kupenda kuishi katika jumiuya halisi na kuujenga ubinadamu halisi.

Liturujia ya Kupaa Bwana
01 June 2019, 14:07