Tafuta

Vatican News
Fumbo la Utatu Mtakatifu: Nafsi Tatu: Lakini uwapo mmoja tu, uwamo mmoja, tu, au asili moja! Fumbo la Utatu Mtakatifu: Nafsi Tatu: Lakini uwapo mmoja tu, uwamo mmoja, tu, au asili moja! 

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Ushuhuda wa Umoja!

Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Taifa lake Israeli kwa kulijulisha jina lake. Jina linaloeleza uwapo (essentia), Umoja wa Nafsi, na maana ya maisha yake. Mwenyezi Mungu analo jina. Yeye si nguvu isi na jina. Kanisa linasadiki na kukiri kwamba, kuna Mungu mmoja tu, wa kweli, wa milele; Mkuu asiyebadilika, asiyetambulika na mwenye uwezo wote. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Kanisa katika maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu linaungama Mungu mmoja katika Nafsi tatu: Yaani Mungu Baba Muumbaji, Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayetakatifuza; wote wanaoungana katika umoja na upendo. Yesu Kristo ndiye aliyewafunulia waja wake Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baada ya ufufuko, akawatuma Mitume kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kuwafundisha na kuwabatiza watu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ni amri ambayo Yesu mwenyewe amelikabidhi Kanisa kwa nyakati zote na kurithi kutoka kwa Mitume dhamana hii ya kimissionari inayopaswa kutekelezwa pia na kila Mkristo, kwani kwa nguvu ya Sakramenti ya Ubatizo, wote wanafanyika kuwa ni sehemu ya Jumuiya yake.

Maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, kwa kuiga mfano wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Watu watambue kwamba, wanategemeana na kukamilishana, mwaliko wa kupokea na kushuhudia uzuri wa Injili kwa pamoja. Mungu ameongea nasi katika historia. Hivyo hata hii sherehe ya leo ni matokeo ya uwepo huo wa Mungu katika matukio ya maisha yetu. Mungu amejionesha katika matukio ya maisha ya mwanadamu. Katika somo la I – halizungumzii Utatu Mtakatifu - ila zipo dalili za ukweli huo. Iko wazi habari ya Mungu mmoja wa Israeli - Mungu ni mmoja. Na huyu Mungu anaonekana kwao katika matukio mbalimbali ya maisha yao ambayo kabla yake hayakuwa hivyo.

Katika somo la II - Mtakatifu Paulo, tunaona Utatu ukiwa kazini - hatuna maelezo ya utatu mtakatifu yanayotolewa - bali ni nini Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanafanya katika maisha yetu. Aongea juu ya ua na n.k ila hilo linawezekana kwa sababu ya ufunuo wa Mwana na kwa njia yake sisi tunakuwa wana. Je, Mtume Paulo alifahamuje ukweli huu? Ni katika maisha ya wafuasi na katika maisha yake mwenyewe. Wote walimwita Mungu Baba kama alivyofanya Yesu. Ni nguvu gani inamsukuma Paulo? Ni roho wa Mungu. Katika barua nyingine za mtume Paulo aongea kumtambua roho katika nafasi mbalimbali kama kufundisha, kuponya n.k Katika Rom.5:1-5 huunganisha utatu mtakatifu na maisha ya kila siku ya mkristo. Mt. Paulo anaunganisha mtandao mzima wa haki na wokovu kama kuwa na amani na Mungu. Kuwa na uhusiano na Mungu ni wajibu wetu mkuu na ni njia ya Kristo - 5:1-2 - basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani na tuwe na amani kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake katika tumaini la utukufu wa Mungu.

Katika Injili– habari juu la Fumbo la Utatu Mtakatifu iko wazi. Mitume na wafuasi wanatumwa kubatiza na katika ubatizo, fumbo la Utatu Mtakatifu huanza kuwepo katika maisha yetu. Ungamo la imani yetu huthibitisha rasmi tamko letu la upendo kwa fumbo hilo.  Mtakatifu Agostino wa Hippo akitaka kueleza utatu mtakatifu kadiri ya akili ya mwandamu - siku moja akitafakari jambo hili maeneo ya ufukweni ghafla akamwona mtoto mdogo peke yake ufukweni. Huyo mtoto alikuwa ametengeneza kishimo na alikuwa akichota maji baharini na kuyamwaga katika kale kashimo. Mtakatifu Agostino akamwuliza unafanya nini? Mtoto akamjibu nataka kuweka bahari hii katika kashimo haka. Mt. Agostino akamwambia itawezekanaje? Kujaza kashimo haka kwa maji ya bahari yaliyo mengi kiasi hiki? Naye yule mtoto akamwambia nawe je wadhani kuwa kichwa chako kidogo na moyo wako mdogo utaweza kuelewa kwa kina na kupenda kikamilifu fumbo la utatu mtakatifu? Mara mtoto yule akatoweka.

Lengo letu ni kuwa pamoja na Baba. Hii inawezekana kwa njia ya Kristo. Matumaini yetu ni kushiriki utukufu wa Mungu. Hii huwezekana kwa njia ya imani inayotupa matumaini. Mungu ametupa matumaini hayo – Rom. 5:5 na tumaini halihatarishi kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumininwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Huu upendo wa Mungu umemwagwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu.  Msingi wa maisha ya Kristo hujengwa katika Utatu Mtakatifu na hii ndiyo tofauti moja kubwa kati ya dini ya kikristo na dini nyingine. Dini nyingine hutazama mhusika (mwamini) na Mungu wake tu. Ukristo pia una mtazamo huo, ila huongeza uwepo wa Yesu kristo anayetuunganisha na Baba na Roho Mtakatifu anayetutakatifuza. Wajibu wetu wa kikristo hauanzii na kuishia tu katika imani kwa Kristo na kupewa haki na Mungu. Huo tu ni mwanzo, toka hapa huanza kazi ya kusaka wokovu, kuwa watakatifu kama Baba alivyo mtakatifu. Sherehe ya PENTEKOSTE  tuliyosherekea jumapili iliyopita inashika kasi hapa. Kwa njia ya roho upendo wa Mungu humwagwa mioyoni mwetu na kwa njia yake tunajifunza kumpenda Mungu na jirani kama alivyotufundisha Bwana.

Swali muhimu - hili fumbo linatuambia nini juu ya Mungu tumwaminiye na ni aina gani ya watu tunapaswa kuwa? Mambo mawili. Katika Mt. 5:48 tunasoma hivi basi ninyi mtakuwa wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Mungu ni wa ushirika - tasaufi ya kikristo inatuwajibisha ulimwenguni. Pendo la kweli lahitaji watu watatu – angalia msemo wa zamani - wawili ni ushirika, watatu ni umati. Baba/mama/mtoto hutengeneza upendo. Huyu Mungu tumwaminiye sisi hufahamika kwetu katika Utatu. Kidunia tunahusiana kati yetu, kimbingu tunahusishwa na Mungu. Mimi ni mkristo kweli nikiishi katika ushirika wa upendo na Mungu na watu wake.

Fumbo la Utatu Mtakatifu haliwezi kueleweka wazi. Ukuu wake hubaki kuwa fumbo. Na leo hatutegemei kupata jibu kwa fumbo hilo. Wakristo wa kwanza kwa akili yao walielewa ufunuo wa Baba kwa njia ya Mwanae. Yesu ameongea nasi habari ya Baba aliyemtuma na juu ya Roho Mtakatifu atakayempeleka na hii iko wazi kwenye maandiko matakatifu. Yesu hutuambia wazi kuwa Mungu amemkabidhi yote naye amemkabidhi yote Roho Mtakatifu. Hapa tunaona muungano wa UTATU. Katika historia ya wokovu Mungu Baba ni mwumbaji, Mungu Mwana ni mkombozi na Mungu Roho ni Mtakatifu hutakatifuza.  Ingawa ni nafsi tofauti Umungu ni mmoja kama ilivyokuwa kwa Mt. Agostino - hatutaelewa ni kwa namna gani ila ni kwanini Mungu amejifunua kwetu.

UKUU WA FUMBO HILI NI HUU: SISI TUMEUMBWA KWA MFANO NA SURA YAKE MUNGU. KWA KADIRI TUNAVYOMUELEWA MUNGU NI JINSI HIYO HIYO TUNAVYOJIELEWA ZAIDI. WATAALAMU WA MAMBO YA DINI WANATUAMBIA KUWA WAABUDUO HUJITAHIDI KUFANANA NA KILE WANACHOKIABUDU. WANAOABUDU MUNGU WA VITA HUWA WATU WA VITA. WANAOABUDU MUNGU WA UPENDO HUWA WATU WA MAPENDO N.K KAMA ALIVYO MUNGU ANAYEABUDIWA NDIVYO WALIVYO WALE WANAOMWABUDU.

Usifiwe Utatu Mtakatifu!

12 June 2019, 16:14