Tafuta

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni msingi wa imani na maisha ya Kikristo. Ni fumbo ndani yake Mwenyewe, kwa hiyo ni chanzo cha mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayoangaza! Fumbo la Utatu Mtakatifu ni msingi wa imani na maisha ya Kikristo. Ni fumbo ndani yake Mwenyewe, kwa hiyo ni chanzo cha mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayoangaza! 

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Msingi na Maisha ya Kanisa!

Wakristo wanabatizwa kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni msingi wa imani na maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Kwa hiyo ni chanzo cha Mafumbo mengine yote ya imani; nuru inayoangaza. Historia nzima ya wokovu ni ufunuo wa Mungu unaopatanisha na kuwaunganisha watoto wa Mungu katika umoja!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa radio Vatikani, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya Utatu Mtakatifu. Utatu Mtakatifu ni fumbo la imani kuwa katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Hizi nafsi tatu za Mungu mmoja, zote ni sawa katika uasili. Na kwa kuwa ni fumbo la imani, imani tu, imani tu yaelewa. Wimbo wa mwanzo unatoa wasifu wake ukisema: Asifiwe Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu; kwa sababu ametuonyesha huruma yake. Na wimbo wa katikati unatoa sifa kwa Mungu ukisema "Umehimidiwa, Ee Mungu wa Babu zetu. Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele" (Dan. 3:52).

Ukweli kuhusu Fmbo la Utatu Mtakatifu: Siri ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni fumbo la Imani. Kuelewa muungano na umoja uliopo katika nafsi hizi tatu katika Mungu mmoja si jambo rahisi kwa akili zetu za kibindamu.  Mtakatifu Augustino alijaribu kwa akili yake yote kupembua siri hii kuu ya Utatu Mtakatifu ili audhibitishe lakini Mungu mwenyewe alimuweka wazi kupitia malaika katika mfano wa mtoto mdogo na kumwambia wazi akili ya mwanadamu ni ndogo kiasi kwamba haiwezi lolote ndiyo maana anatufundisha akisema inatupasa kusadiki kwa sababu Mungu ametufunulia. Anaendelea kusema; lakini mafumbo kama haya katika imani yetu ni kama mifupa katika nyama. Kama tusivyoitupilia mbali mifupa moja kwa moja na nyama iliyo juu yake bali tunakwangua nyama yote na kuachana na mifupa, na haya mafumbo hatuwezi kuyakimbia moja kwa moja tutafanya tuwezalo ili kuelewa kinachoweza kueleweka; ikibaki mifupa kabisa tutaacha tunapiga magoti na kusadiki.

Mtakatifu Thomaso wa Akwino aliyejaliwa uelewa mkubwa na wa hali ya juu wa mambo yamhusuyo Mungu anasema; waficha Umungu msalabani na ubinadamu altareni mafahamu yangu yadanganya yanapokuona. Ndiyo maana Mtume Paulo akisema: “Basi, sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho. Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtumpu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho. Maandiko yasema, nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Lakini sisi tunayo akili ya Kristo (1Kor.2:13-16). Thomaso wa Akwino anatushauri kwamba: ukikutana na lolote ambalo hulielewi ama katika Biblia au katika mafundisho ya Kanisa usiseme mambo haya hayaeleweki au yamekosewa bali useme akili zangu ni ndogo kuelewa ukweli huu.

Fanya juhudi kuelewa utakavyoweza. Yatakayokushinda “Inamisha kichwa mpaka nchi na kusema pamoja na Mtakatifu Hipoliti kuwa; nasadiki kwa kuwa sina uwezo wa kueleza ni ubatili mtupu! Fundisho la Utatu Mtakatifu ni moyo na kiini cha imani yetu ya kikristo. Ni fumbo asili la imani na maisha ya Kikristu. Kwa Utatu Mtakatifu tunafunuliwa huruma, wema na upendo ambavyo ni asili ya Mungu. Ni katika Utatu Mtakatifu ndimo tunamopata ufupisho na simulizi la asili yetu tangu kuumbwa hata ukombozi kwa njia ya Yesu Kristo nafsi ya pili ya Mungu, ndimo zinamolala sala zetu na matumaini yetu kufikia utimilifu wa upendo kwa kuungana na yule aliye upendo.

Msingi wa fundisho la Utatu Mtakatifu: Imani katika Utatu Mtakatifu imefunuliwa kwetu na Mungu mwenyewe katika maandiko matakatifu. Mtume Paulo anapowasalimu wakristo katika Salamu-tangulizi za barua zake haachi kusema “neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote.” Katika kitabu cha Mwanzo 1:1-2 tunasoma; “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji. Roho wa Mungu akatulia juu ya uso wa Maji” Hii yadhihirisha kuwa Roho Mtakatifu alikuwepo tangu mwanzo. Katika kitabu cha Methali 8: 1-36 kinamtaja Hekima (Neno wa Mungu ambaye ni Kristo) anasema “Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi”. Mwa 1:24 “Mungu akasema, Natumfanye mtu kwa mfano wa sura na mfano wetu. Mungu akasema (ni mmoja anayesema), kwa sura na mfano wetu (ni wingi).

Hii tayari inatuonyesha kuwa Mungu ni Mmoja katika Nafsi zaidi ya moja. Kumbukumbu la Torati linatuambia, 6:4 “Sikiliza ee Israeli Bwana Mungu wetu Bwana ndiye Mmoja”. Jn 14: 15-17 Yesu anasema; “Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine ndiye Roho wa Ukweli.” “Filipo; aliyeniona mimi amemwona Baba, Mimi ni ndani ya Baba na Baba yu ndani yangu” (Yon. 14:8-10). Huu ni udhibitisho wa Kibibilia wa ufunuo wa Utatu Mtakatifu kwa sababu aliyetufunulia ni Mungu mwenyewe Yesu Kristu aliye nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu hatuna budi kuamini na kusadiki.

Kutangaza na kukiri imani yetu juu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Katika maisha yetu ya kila siku tunakiri na kuutangaza Utatu Mtakatifu. Kila mara katika sala zetu tunaanza na kuhitimisha kwa ishara ya msalaba huku tukitamka waziwazi maneno; “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” Tunapaswa kufanya hivyo kila tunapoamka, kabla na baada ya kula, kabla na baada ya kazi, wakati wa sala zingine na ibada mbalimbali na kabla ya kulala. Ni kwa njia hii tunatangaza waziwazi msingi wa imani yetu.

Mtakatifu Augustino anasema, ‘‘Roho Mtakatifu anatoka kwa Baba kama chanzo cha kwanza, na kwa paji la milele analolitoa Baba kwa mwana, anatoka katika umoja wa Baba na Mwana’’. Kupelekwa kwa Roho Mtakatifu ambaye Baba anamtuma kwa jina la Mwana na ambaye Mwana anamtuma toka kwa Baba, kunafunua kwamba yeye pamoja nao ni Mungu huyo huyo mmoja (Yon. 14:15-17) katika nafsi tatu. Ni kwa upendo wa Mungu dunia na vyote vilivyomo, vinavyoonekana na visivyoonekana vilifanyika (Yon.1:2). Ni kwa upendo wa Mungu taifa la Israeli liliandaliwa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Ni kwa upendo wa Mungu, “Kristo alijinyenyekeza akawa mtii mpaka mauti, naam hata mauti ya msalaba” (Wafilipi. 2:8) na ni kwa upendo wa Mungu Kanisa liliimarishwa na kuendelea kukua kutokana na ujio wa Roho Mtakatifu aliyetoka kwa Baba na Mwana (Mdo.1:8; 2:1-13). Na huu ndio ufunuo wa Utatu Mtakatifu.

Tunaposherehekea Fumbo la Utatu Mtakatifu tuombee umoja katika familia kama Kanisa la nyumbani na katika Kanisa kwa ujumla. Yesu aliomba: Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma” (Jn 17:21). Ufunuo unatuonyesha kuwa Baba ni Muumbaji, Mungu Mwana ni Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ni Mfariji. Lakini katika yote haya hawakuachana. Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu walikuwepo na kushiriki katika uumbaji: “Hapo mwanzo kulikuwa Neno naye Neno alikuwa kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika” (Yoh.1:1).

Katika kutukomboa Mungu Baba na Mungu Roho Mtakatifu hawakumwachia Mungu Mwana ahangaike peke yake. Wote walikuwepo: “Yesu akasema, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yangu yu pamoja nami’ (Yn.16:32). Luka anatuambia tena kuwa Yesu alipokuwa Gethseman alisali akasema: “Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki, hapo malaika kutoka mbinguni akamtokea ili kumtia moyo” (Lk.22:42-43).  Tuzingatie wosia wa Paulo: “Hatimaye ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi katika Utatu Mtakatifu. Salimianeni kwa busu takatifu” (2Kor 13:11-14).

Lisifiwe na kuabudiwa Fumbo la Utatu Mtakatifu!

Utatu Mtakatifu

 

 

13 June 2019, 17:28