Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Waamini wanaandamana kutangaza na kushuhudia uwepo wa Kristo kati yao! Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Waamini wanaandamana kutangaza na kushuhudia uwepo wa Kristo kati yao! 

Ekaristi Takatifu: Chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Katika Ekaristi Takatifu fumbo la Ukombozi wetu linawekwa hai na kufikia kilele katika sadaka ya Bwana: “huu ndio Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu na hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu”, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” (Luka 22:19-20). Sisi sote tunaalikwa kwenye karamu hii ili tuweze kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo Yesu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Ekaristi Takatifu.  Maana ya Ekaristi. Neno Ekaristi asili yake ni lugha ya Kigiriki Eucharistein likimaanisha shukrani. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Pia huitwa Misa Takatifu, karamu ya Bwana, kumega mkate, kusanyiko la Kiekaristi, ukumbusho wa mateso kifo na ufufuko wa Bwana, Sadaka Takatifu ya Misa, Liturjia Takatifu, Sakramenti Takatifu sana ya Altare na Komunyo Takatifu. Ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo waamini humpokea Kristo na roho hujazwa neema na kupewa amana ya uzima wa milele (KKK 1322 – 1323, 1409).

Ekaristi ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa, kwa kuwa kwayo Kristo anachagamana na Kanisa lake na waamini wake wote na sadaka ya sifa na shukrani iliyotolewa mara moja Msalabani kwa Mungu Baba. Kwa sadaka hii anamimina neema za wokovu kwa mwili wake ambao ni Kanisa (KKK 1407). Papa Leo XIII anasema Ekaristi Takatifu ni roho ya Kanisa (Denz.3364). Ni Sakramenti ya umoja na upendo, kimsingi, Ekaristi ni kiini kamili katika Kanisa, na Kanisa haliwezi kitu pasipo hiyo. Kwasababu ni Kristo mwenyewe anayejitoa kweli kama sadaka kwa ajili ya Kanisa katika Ekaristi Takatifu na ni katika Ekaristi Kanisa hufikia uhalisia wake wa juu wa asili yake, yaani, kuwa linaonekana, la daima, na alama wazi ya neema ya wokovu ya Mungu iliyopo duniani kupitia Kristo.

Ekaristi ni chemchemu na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Katika Ekaristi tendo la Mungu kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo na kilele cha tendo la watu kumwabudu Mungu katika Kristo hufanyika. Katika Ekaristi mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, Pasaka wetu. Ekaristi ndio ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja ule wa Taifa la Mungu ambao unalifanya Kanisa liwepo. Kwa njia ya adhimisho la Ekaristi tunauungana tayari sisi wenyewe na liturjia ya mbinguni na tunaanza kutangulia kushiriki uzima wa milele (KKK 1324 – 1327, 1407). Katika sadaka Ekaristi, Kanisa hutolea maisha ya waamini, masifu yao, mateso yao, sala zao, kazi zao na kuyaunganisha na yale ya Kristo kwa Mungu Baba. Kwa vile ni sadaka, Ekaristi hutolewa kwa waamini wote, wazima na wafu kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na kupata rehema ya Mungu. Kanisa la Mbinguni pia linaungana na matoleo ya Kristo.

Ekaristi ni Sakramenti: Ekaristi ni mojawapo kati ya sakramenti saba za Kanisa ambazo ni alama wazi zilizowekwa na Yesu Kristo mwenyewe ili kutuletea neema ya wokovu. Ekaristi ni sakramenti inayokamilisha tendo zima la kumwingiza Mkatukumeni katika ukristo. Tofauti na sakramenti zingine Ekaristi ni Kristo mwenyewe katika maumbo ya mkate na divai. Ni sakramenti ya sakramenti (KKK. 1211). Mtakatifu Thomaso wa Akwino anasema Sakramenti zingine zote zimeimarishwa kwake kama ndio mwisho wa sakramenti hizo. Uwepo wa Kristo katika Ekaristi unaiinua Ekaristi juu zaidi kuliko sakramenti zingine ukiwa ndio Utimilifu wa maisha ya kiroho na ndio mwisho ambao sakramenti zote hulenga kwani ndani yake kuna mwili na damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, kweli, halisi na uwamo kamili pamoja na roho na umungu na hivi ni Kristo mzima kabisa (KKK 1 374).

Mababa wa Mtaguso wa Trenti walitoa tamko kuwa: “Kwa sababu Kristo Mkombozi wetu ndiye alisema mwenyewe kwamba ulikuwa ni mwili wake kweli ambao alikuwa anautoa sadaka kwa namna ya mkate na damu kwa namna ya divai, imekuwa tayari imethibitishwa kwa Kanisa la Mungu, kwamba kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate na divai kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na ya kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake (1376). Uwepo huu huanza dakika ya mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwepo. Hivyo Kristo yupo mzima na mkamilifu katika kila mojawapo ya maumbo ya mkate na divai na ni mzima na mkamilifu katika kila sehemu yao, kwa jinsi hii kwamba kuimega Ekaristi hakumgawanyi Kristo hata kidogo” (KKK 1377), uwepo wa Yesu unabaki kwenye kila kipande kidogo kilichovunjika na hata katika kila tone la damu yake uwepo wa Yesu umo kamili kabisa kama katika Ekaristi nzima. Ukweli huu Kristo mwenyewe anaudhihirisha katika muujiza wa Lanciano.

Chanzo na asili ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu iliwekwa na Yesu Kristo mwenyewe siku ya Alhamisi kuu, wakati ule wa karamu ya mwisho aliyokula pamoja na wanafunzi wake kwenye chumba cha juu-Cenaculum, usiku ule aliotolewa kwake ili kuendeleza sadaka ya msalaba siku zote mpaka atakaporudi kwa utukufu (1Kor. 11:23 -26, KKK. 1337). Uwezo wa kuugeuza mkate kuwa mwili wake na divai kuwa damu yake aulitoa Yesu Kristo mwenyewe siku hiyo kwa Maaskofu na Mapadre wote wa Agano Jipya kwa njia ya mitume (Lk 2:19; 1Kor 11:23-25). Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unathibitisha kwamba, Ekaristi ni “Chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo” (Lumen Gentum, n. 11), “chemchemi na kilele cha uinjilishaji wote” (Presbyterorum Ordinis, n. 5).

Kumbe Ekaristi inaunda Kanisa na Kanisa linaitengeneza Ekaristi, na ndimo linamochota nguvu ya kiroho. Hivyo hakuna jumuiya ya Kikristo inayoweza kujengwa na kusimama imara bila adhimisho la Sakramanti Kuu ya Ekaristi Takatifu (Presbyterorum Ordinis, n. 6). Katika Ekaristi Takatifu fumbo la Ukombozi wetu linawekwa hai na kufikia kilele katika sadaka ya Bwana, kama inavyotamkwa katika maneno ya konsekrasio: “huu ndio Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu na hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu”, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” (Luka 22:19-20). Sisi sote tunaalikwa kwenye karamu hii ili tuweze kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo.  “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. 

Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yn 6:56-57). Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, hivyo inatuunganisha na watu wote kwa muda wote bila kujali tofauti zetu za aina yoyote ile. Huu ni ukweli ulio wazi. Kristo anasema, “aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu nami ndani yake.” Kwa kuwa tunakuwa kile tunachokula, tukila mwili na kunywa damu ya Kristo tunakuwa na ukristo ndani mwetu tunakuwa kitu kimoja, ndiyo maana tunaitwa wakristo. Mbele ya Ekaristi Takatifu, tofauti zetu za kisiasa, kikabila, kivyama, kitaifa, kirangi hazina nafasi kwa kuwa kila mmoja ana Ukristo ndani yake na Ekaristi Takatifu inatupatia msamaha wa dhambi nasi tunasameheana na kuwa wamoja.

Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu ni tendo la toba linatutakasa kabisa kutokana na dhambi ndogondogo, linatupatia nguvu katika vita dhidi ya uovu na hutuepusha na kuanguka tena dhambini. Lakini kwa habari ya dhambi za mauti, Sakramenti ya Kitubio haiepukiki. Mtakatifu Ambrosi anasema; “Ekaristi ni mkate wetu wa kila siku kwa ajili ya dhambi zetu za kila siku, inatunapatia silaha bora dhidi ya vishawishi”. Didache yaani mafundisho ya mitume yanasema; “Pasiwepo mtu wa kunywa wala kupokea Ekaristi pamoja nanyi isipokuwa wale tu waliobatizwa kwa jina la Bwana, kwa maana ilikuwa ni kwa marejesho ya jambo hili kwamba Bwana alisema, ‘Msiwape mbwa vitu vitakatifu’ Mt. 7: 6.

Ifikapo siku ya Bwana baada ya kukusanyika na kuwa pamoja, mtamega na kutoa Ekaristi, baada ya kuungama makosa yenu, kusudi sadaka yenu iweze kuwa safi. Lakini asiruhusiwe mtu yeyote aliye na ugomvi na jirani yake ajiunge nanyi mpaka awe amefanya usuluhisho, la sivyo sadaka yenu ni batili” (Didache 9,14,1-2). Hivyo, kwa mkristo kuinua upanga dhidi ya mwingine ni kwamba unajiinulia upanga mwenyewe na unamuinulia Kristo upanga. Hivi ndivyo alivyomwambia Paulo alipokuwa anawatesa Wakristo “ni mimi Kristo unayenitesa” na ndiyo maana anasema “chochote ulichowatenda hawa wadogo umenitendea mimi.” Ekaristi yatufanya tujitoe mhanga kwa maskini (KKK 1391 – 1397, 1416).

Ni hasara kubwa sana kutopokea Ekaristi kwa kuwa umejiwekea vizuizi, umejifungia. Wale wasiopokea Ekaristi nawasihi fanyeni bidii kubomoa kuta za vizuizi mpokeeni Ekaristi, ili muungane na jamii ya waamini katika Ekaristi na kuwa kweli wakristo. Tukiwa na tofauti katika familia, katika nafasi za kazi, katika vyama vyetu vya siasa, tuiangalie Ekaristi ili iwe sababu yetu ya kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana kwa kuwa Ekaristi inatuunganisha inatufanya tuwe wakristo kwelikweli. Tumsifu Yesu Kristo katika Sakramenti kuu ya Altare!

Ekaristi Takatifu
19 June 2019, 14:59