Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Wakarismatiki Wakatoliki ni mkondo wa neema katika maisha na utume wa Kanisa! Papa Francisko: Wakarismatiki Wakatoliki ni mkondo wa neema katika maisha na utume wa Kanisa!  (Vatican Media)

Wakarismatiki Wakatoliki ni mkondo wa neema katika Kanisa!

Askofu mkuu mwandamizi Ruwa'ichi amewataka waamini kuhakikisha kwamba, kongamano hili: Linamtukuza Mungu na mwanadamu anatakatifuzwa. Iwe ni fursa ya kutangaza, kushuhudia, kueneza na kuimarisha imani. Kongamano lijikite katika azma ya kukoleza roho, moyo na utamaduni wa sala na Ibada Takatifu; toba na wongofu wa ndani, ili kuambata utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha kitengo maalum kijulikanacho kama “CHARIS” kinachosimamia na kuratibu shughuli za Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki. Kitengo hiki kimezinduliwa rasmi wakati wa maadhimisho Sherehe ya Pentekoste, 9 Juni 2019. Wakarismatiki Wakatoliki ni mkondo wa neema kwa Kanisa zima. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwanzo mpya kwa Wakarismatiki Wakatoliki baada ya safari ya miaka 52 tangu kuanzishwa kwake na sasa kimeenea na kukita mizizi yake katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Mwanzo mpya unapania kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Wakarisimastiki wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, upya huu ni baraka na neema ya Mungu inayofumbatwa katika huduma na ushuhuda wa umoja katika utofauti wake. Mama Kanisa anatarajia kuona upya wa maisha na utume wa Wakarismatiki ukishuhudiwa na Wakristo wote, kwa kuishi kwa namna ya pekee neema ya Ubatizo wao; kwa kuendeleza na kudumisha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mambo msingi ni Ubatizo katika Roho Mtakatifu, Umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo na huduma kwa maskini, ni shuhuda zenye mvuto na mashiko katika mchakato mzima wa uinjilishaji!

Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Ijumaa, tarehe 7 Juni 2019 amezindua rasmi kongamano la Roho Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste na Jubilei ya Miaka 50 ya Baraza la Waamini Walei nchini Tanzania. Katika mahubiri yake, amewataka waamini kuhakikisha kwamba, kongamano hili linamtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu anatakatifuzwa. Iwe ni fursa ya kutangaza, kushuhudia, kueneza na kuimarisha imani: katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anasema, Kongamano lijikite katika azma ya kukoleza roho, moyo na utamaduni wa sala na Ibada Takatifu, ili kusaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata utakatifu wa maisha. Kongamano lisaidie kukuza na kudumisha umoja na upatanisho katika maisha na utume wa Kanisa. Wito wa kwanza, ni kukoleza utakatifu wa maisha. Utume wa Wakarismatiki Jimbo kuu la Dar es Salaam uwe mstari wa mbele kuliombea Kanisa; Kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu; kuombea maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam amewaambia Mapadre wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kwamba, Utume wa Wakarismatiki unayo haki na hitaji la kupata Mapadre watakaowaongoza katika maisha na utume wao kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa.

Kongamano DSM
08 June 2019, 14:08