Tafuta

Vatican News
Kardinali Pengo: Utume wa waamini walei unapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake! Kardinali Pengo: Utume wa waamini walei unapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake! 

Jubilei ya Miaka 50 Utume Walei Tanzania! Chimbuko lake: Upendo wa Utatu Mtakatifu

kardinali Polycarp Pengo anasema, waamini walei ni mhimili wa Kanisa la Kristo katika kuyakatifuza malimwengu. Utume wao unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kielelezo cha upendo wa Mungu Baba aliyemtuma Mwanaye wa Pekee Kristo Yesu, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti; utume unaendelezwa na Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utume wa waamini walei nchini Tanzania ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaobainisha: wito, wajibu na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu, na Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Waamini walei ni mhimili wa Kanisa la Kristo katika kuyakatifuza malimwengu. Utume wa waamini walei unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kielelezo cha upendo wa Mungu Baba aliyemtuma Mwanaye wa Pekee Kristo Yesu, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Mchakato wa utume, huu unaendelezwa na Roho Mtakatifu anayeliongoza, kulitegemeza na kulitakatifuza Kanisa. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania, kuanzia mwaka 1969 hadi mwaka 2019 yameongozwa na kauli mbiu “Kuyatakatifuza malimwengu”. Mgeni rasmi katika maadhimisho haya alikuwa ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Tanzania, CDF, Jenerali Venance Mabeyo. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumapili, tarehe 16 Juni 2019 katika adhimisho la Fumbo la Utatu. Utume wa waamini walei unapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kanisa linakiri na kumtukuza Mungu mmoja aliyejifunua katika Nafsi tatu yaani: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa linaamini juu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa sababu Mungu mwenyewe amelifunua hatua kwa hatua katika historia ya wokovu; katika kazi ya Uumbaji, Ukombozi wa mwanadamu na katika Fumbo la kumtuma Roho Mtakatifu. Hizi ni Nafasi tatu katika Mungu mmoja. Hili Fumbo kuu la Imani Katoliki, linalovuka mipaka ya akili, ufahamu na uelewa wa binadamu! Kristo Yesu alipokuwa anatangaza Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni Mwili na Damu yake Azizi, wafuasi wake wakagawanyika na wengine wakaondoka na kwenda zao!

Kristo Yesu alipoona hayo, akawauliza Mitume wake, ikiwa kama hata wao walitaka kuondoka, lakini Mtakatifu Petro akamwambia, hawana sababu msingi ya kuondoka kwani Kristo Yesu alikuwa na maneno ya uzima wa milele. Fumbo la Utatu Mtakatifu limefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, amana na utajiri wa maisha ya kiroho, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa waja wake. Kardinali Polycarp Pengo anakiri kwamba, Fumbo la Utatu Mtakatifu lilimhangaisha sana Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, lakini hatimaye, akafunuliwa kwamba, Fumbo hili limefunuliwa katika upendo uliomfanya Mungu Baba hata akamtuma Mwanaye wa Pekee Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Lengo kuu ni kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu alipokamilisha kazi ya Ukombozi, akamtuma Roho Mtakatifu, Nafsi ya tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kuendeleza kazi ya Ukombozi, hadi utimilifu wa dahali. Fumbo la Utatu Mtakatifu linaunganisha utume wa waamini walei katika maisha ya Kanisa kama ulivyoratibiwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kusoma alama za nyakati. Hata kabla ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa lilikuwa na Makatekista mahiri waliotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, waliotoa katekesi makini bila ya kujibakiza!

Kumbe, utume halisi wa waamini walei, unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofumbatwa katika umoja na upendo. Kardinali Pengo anasema, hii ndiyo changamoto kwa waamini walei wanayopaswa kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Jubilei ni kipindi cha kuomba toba na msamaha, ili kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Katika kipindi cha Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania kumekuwepo na viashiria vya udhaifu na mapungufu ya binadamu, kinyume kabisa cha umoja na upendo wa Mungu, yaani ubinafsi na uchoyo! Kumekuwepo na tabia ya watu kujitafuta na kutaka kujikuza, kwa ajili ya mafao yao binafsi pamoja na kupenda sifa kupita kiasi!

Kardinali Polycarp Pengo kwa msisitizo anasema, chimbuko la utume wa walei uwe ni umoja na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini walei washiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Nafasi za uongozi wa utume wa walei isiwe ni “kichaka” cha kujitafutia ajira, kwani hali hii inapotosha lengo la utume wa walei. Miaka 50 ya Utume wa Walei, kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Familia ya Mungu nchini Tanzania, kamwe isiendekeze udhaifu na mapungufu ya kibinadamu, iwe na ujasiri na ari ya kupiga hatua kwa kujikita katika umoja na upendo kwa ajili ya mafao ya watu wa Mungu!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amewapongeza waamini walei kwa utume uliotukuka, kwa kufanya maamuzi ya busara na hekima; kwa kusoma alama za nyakati, ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zilizojitokeza katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita. Ameomba msamaha kwa niaba ya Wakleri ambao wametekeleza dhamana na wajibu wao kinyume cha matarajio ya waamini walei, lakini bado wanayo nia njema ya kuwa wachungaji wema. Rasimu ya Katika ya Halmashauri Walei Tanzania inaendelea kufanyiwa kazi na ikiwa tayari itapitishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tayari kuanza kutumika!

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga amewakumbusha waamini walei kwamba, utume wao unakita mizizi katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima:kiroho na kimwili. Kwa namna ya pekee kabisa, wanatumwa kuyatakatifuza malimwengu na hatimaye, kumkomboa mwanadamu kutoka katika maovu yanayomzunguka na kumwandama: Huu ndio ukatili, utekaji nyara; mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; Ukosefu wa haki, heshima na utu wa binadamu; unyanyasaji wa kijinsia na unajisi kwa watoto wadogo; tabia ya watu kukengeuka kimaadili na kutopea kwa imani. Askofu mkuu Gervas Nyaisonga anakaza kusema, kumeibuka tabia ya watu kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote! Kumbe, mchango wa waamini walei katika kuzuia na kukomesha maovu haya yanayoiandama jamii ni mkubwa sana, changamoto kwa waamini walei ni kuondokana na chachu ya kale, kwa kujivika weupe wa moyo na kweli, ili kuukomboa wakati!

Kwa upande wake, Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amewataka waamini walei nchini Tanzania kuendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa kushikamana katika umoja na upendo unaomwilishwa katika unyenyekevu kama ushuhuda wa imani, amana na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho! Askofu Desiderius Rwoma, ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania katika maadhimisho ya Mwaka wa Familia, matunda ya adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania, iwe ni fursa ya kuimarisha Familia kama Kanisa la nyumbani na shule ya imani na maadili.Tunu msingi za maisha ya Kikristo zipewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa waamini wale nchini Tanzania. Waendelee kusali na kuombea miito mitakatifu, ili Kanisa la Tanzania liweze kupata mihimi mikuu itakayojikita katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Watambue kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu amewatendea makuu katika kipindi cha Miaka 50 ya Utume wa Walei nchini Tanzania!

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Tanzania, CDF, Jenerali Venance Mabeyo, mgeni rasmi katika maadhimisho haya, kwa namna ya pekee kabisa amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendeleo aliomkirimia, ambao umekuwa ni nafasi kwake kusali, kutafakari na hatimaye, kukubali kupokea mwaliko huu kwa moyo wa utulivu na amani ya ndani. Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania ni muda wa shukrani kwa baraka na neema ambazo Roho Mtakatifu ameliwezesha Kanisa la Tanzania, kiasi cha kupiga hatua kubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili. Jenerali Venance Mabeyo, amesema, waamini walei kwa kushirikiana na kushikamana na viongozi wa Kanisa wamekuwa na mwamko mkubwa wa imani na washiriki wazuri katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Anasema, idadi ya miito mitakatifu imeongezeka maradufu na kwamba, waamini walei wameendelea kujisadaka kwa ajili ya kulitegemeza Kanisa mahalia kwa hali na mali kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana na wajibu wao. Waamini walei wameendelea kuimarisha uchumi wa Kanisa katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wao ni mitume wamisionari wanaopaswa kusoma alama za nyakati! Katika kipindi cha miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania, kumekuwepo na ongezeko kubwa la waamini hali ambayo imechangia pia kupanuka kwa huduma za shughuli za kichungaji katika ngazi mbali mbali. Waamini walei wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa kwa kuchangia, sadaka, zaka na mavuno.

Jenerali Venance Mabeyo anasema changamoto kubwa kwa walei ni: Uimarishwaji wa vyama na mashirika ya kitume, kwa kuwapatia walezi, mafunzo na katekesi endelevu ili waweze kuwajibika barabara, kwa kujikita katika uongozi bora. Waamini waelimishwe umuhimu wa kulitegemeza Kanisa kama njia ya kuenzi na kukuza imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu wa Mungu! Imani ipewe kipaumbele cha kwanza na wala si fedha! Mapato na matumizi ya rasilimali fedha ya Kanisa yazingatie misingi ya ukweli, uwazi na uaminifu kwa kutambua kwamba, lengo kuu ni kwa ajili ya huduma ya uinjilishaji.

Jenerali Venance Mabeyo amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa nidhamu, utii na unyenyekevu pasi na unafiki, ili kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake msingi. Uchaguzi mkuu wa viongozi walei, ufanyike kwa umakini mkubwa, ili Kanisa la Tanzania liendelee kusonga mbele! Katika maadhimisho haya, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Tanzania, CDF, Jenerali Venance Mabeyo amezindua pia kitabu chake kijulikanacho “Je, wewe ni Shahidi wa Kristo”?

Jubilei Walei
18 June 2019, 12:14