Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania: Dhamana, wito na wajibu wa walei kuyatakatifuza malimwengu! Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania: Dhamana, wito na wajibu wa walei kuyatakatifuza malimwengu! 

Jubilei ya Miaka 50 Utume wa Walei Tanzania! Dhamana & Wajibu!

Utume wa waamini walei nchini Tanzania ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaobainisha: wito, utume na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Waamini walei ni mhimili wa Kanisa la Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuanzia tarehe 14 hadi 16 Juni 2019 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei nchini Tanzania, inayoongozwa na kauli mbiu “Kuyatakatifuza Malimwengu”. Utume wa waamini walei ndani ya Kanisa ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, unaowataka waamini walei kutambua kwamba, wanashiriki kikamilifu huduma za Kristo za kikuhani, kinabii na kifalme na kwamba, wanapaswa kutimiza wajibu wao kadiri ya hali yao katika Kanisa, na Ulimwengu katika ujumla wake. Waamini walei wanamahasishwa kushiriki kwa dhati kabisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Jambo la msingi kwa walei kuhakikisha kwamba, wanashikamana na viongozi wao wa Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea nchini Tanzania kunako mwaka 1990, katika hotuba yake kwa waamini walei Jimbo kuu la Tabora alisema, alikuwa kati yao ili kuwaimarisha katika imani na kuwatia moyo katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kutumia kikamilifu karama na matunda ya Roho Mtakatifu waliyokirimiwa katika maisha! Mtakatifu Yohane Paulo II alisema, karama na mapaji haya yawaongoze katika utakatifu wa maisha na ushuhuda wa kazi njema zinazofumbatwa katika huduma, ili kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu na kwamba, kila mwamini anayo nafasi ya pekee katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa!

Mtakatifu Yohane Paulo II, aliwataka waamini walei kuimarisha familia kama kitalu cha miito mbali mbali ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, kwa kuishi vyema ukuhani, unabii na ufalme wao! Kila mwamini ajibidishe kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kwa kujituma na kamwe asiwepo mtu anayebweteka, ili waweze kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania! Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini walei washiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika ulimwengu mamboleo! Waamini walei wakuze na kudumisha moyo wa: Sala, Ibada na Tafakari ya Neno la Mungu. Wajenge ndani mwao utamaduni wa haki, amani na utulivu, ili waweze kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya mataifa!

Wazazi na walezi washiriki vyema katika malezi, makuzi na majiundo ya watoto wao katika familia: kiroho, kimwili, kiutu na kitamaduni. Makatekista waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia kikamilifu ukweli wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Juhudi za uinjilishaji nchini Tanzania hazina budi kwenda sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano ndani na nje ya Tanzania! Watanzania wawe ni mashuhuda wa ukweli, huruma na upendo unaomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Waamini waendelee kushiriki kikamilifu katika siasa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini washiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watanzania wote! Sera na mikakati ya siasa nchini Tanzania ilenge kukuza na kudumisha: ulinzi na usalama; ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote bila ubaguzi! Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliwakumbusha watanzania kuwa ni nchi inayojipambanua kwa ukarimu na upendo kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa! Ushuhuda huu unapaswa kuendelezwa. Kwa hakika, Kanisa la Tanzania linawahitaji Wakristo waliokaaa, wenye busara na hekima; watakatifu, watu wanaoweza kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Kwa upande wake, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika mazungumzo yake na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwakaribisha wawakilishi wa waamini walei kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania, ili kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei nchini Tanzania, amekiri kwamba, Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa waamini walei katika maisha na utume wake. Waamini walei, watambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana katika Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania.

Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa waamini walei nchini Tanzania ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani; ni wakati wa kuomba msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 50 iliyopita na kuomba huruma, neema na upendo wa kuanza upya kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kardinali Pengo amewataka wajumbe wa Halmashauri Walei kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania kushirikishana uzoefu na mang’amuzi waliojichotea wakati walipokuwa wanahudhuria semina mbali mbali kwenye Viwanja wa Msimbazi Center, Jimbo kuu la Dar Es Salaam.

Wakati huo huo, Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hapo tarehe 15 Juni 2019 katika Ibada ya ufunguzi wa maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa walei Tanzania amewakumbusha kwamba, wanawajibishwa na upendo wa Kristo kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo, Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Ili kufanikisha zaidi utume wao, wanapaswa kushikamana na Kristo pamoja na jirani zao, ili kwa kutakatifuzana, wote waweze kufika mbinguni. Waamini walei wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, ukweli na maridhiano kati ya watu; ushuhuda unaopaswa kudhihirishwa kwa njia ya matendo pamoja na kutekeleza ahadi zao kwa Mwenyezi Mungu.

Waamini walei watambue: wito, wajibu na dhamana yao, ili waweze kutenda kwa haki. Waendelee kudumu katika imani, matumaini na mapendo; daima wakijitahidi kuimarisha familia, jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, kwa kukita maisha yao katika njia ya utakatifu wa maisha! Waamini walei ni washauri wazuri sana wa wakleri. Askofu Rwoma, amewapongeza waamini walei kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kituo cha Walei Bakanja. Ili wamelifanikisha kwa njia ya upendo, umoja na mshikamano. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni moto wa kuotea mbali katika maisha na utume wa Kanisa, lakini Umoja wa Wanaume Wakatoliki, bado unasuasua sana, changamoto na mwaliko wa kuanza kucharuka zaidi.

Askofu Desiderius Rwoma, ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kumwilisha ndani mwake fadhila na tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu, kwa kutambua kwamba, kila mtu analo jambo analoweza kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Watanzania wapendane, waheshimiane, wathaminiane, wasahihishane na kukosoana kwa huruma na upendo, kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Katika ulimwengu mamboleo, dini zinaendelea kuibuka kila kukicha kama uyoga! Ni fursa kwa waamini kutambua kwa kina kabisa: Imani ya Kanisa, Sakramenti, Amri za Mungu na Maisha ya Sala: Kwa muhtasari tu, hiki ni kiini cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki.

Imani potofu ni chanzo kikuu cha uvunjwaji wa haki msingi za binadamu pamoja na kukomaa kwa ushirikina ambao unaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu. Umefika wakati kwa watanzania kuondokana na imani za kishirikina, kwa kuwa ni mashuhuda amini wa Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Utume Walei 50 Yrs
16 June 2019, 16:45