Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwaichi: Jubilei ya Miaka 50: Utume wa Walei Tanzania: Dhamana, wito na utume wa familia katika kuyatakatifuza malimwengu! Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwaichi: Jubilei ya Miaka 50: Utume wa Walei Tanzania: Dhamana, wito na utume wa familia katika kuyatakatifuza malimwengu! 

Jubilei ya Miaka 50 Utume wa Walei Tanzania! Utume wa familia!

Jubilei ya Miaka 50: Utume wa Walei Tanzania: Ni vema kuikabili kwa kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo: Kanisa: Chimbuko, hulka na utume wake. Pili, Walei: Wito na Utume wao kadiri ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Tatu, Halmashauri ya Walei: chimbuko na malengo yake. Nne, Utume wa Familia: chimbuko, maana, changamoto na utume wake! Familia Kanisa la nyumbani.

Askofu Mkuu Mwandamizi  Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi OFMCap., - Dar es Salaam.

UTANGULIZI: Nimealikwa nitoe mada juu ya Miaka 50 ya halmashauri ya walei na Utume wa familia. Nianze kwa kuwapongeza kwa tukio hili la kihistoria la mnapoadhimisha jubilee ya dhahabu ya Utume wa Walei hapa kwetu Tanzania. Miaka 50 ni safari ndefu ya baraka na neema, ya kukua na kujenga mang'amuzi, kuinjilishwa na kuinjilisha, ya kushirikishwa na kukua katika uhai na utume wa kanisa. Bila shaka, katika kipindi hicho, kanisa la Tanzania limeuonja uwepo na utendaji wa Mungu ambaye analipenda na kulisitawisha kanisa lake. Ndiyo maana ni vema na haki tumrudishie sifa na shukrani. Sambamba na hayo, hii pia ni fursa ya kujitathmini na kujipanga upya ili uwepo wetu uzidi kuutumikia mpango mtakatifu wa Mungu. Nilipoitazama mada niliyopewa, nilihisi kwamba ni vema kuikabili kwa kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo: Kanisa: Chimbuko, hulka na utume wake. Pili, Walei: Wito na Utume wao kadiri ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Tatu, halmashauri ya Walei: chimbuko na malengo yake. Familia: chimbuko, maana, changamoto na utume wake. Nne, Utume wa Familia. Nitajaribu kuvipitia vipengele hivyo kwa kifupi.

KANISA: Ukizungumza juu ya walei, watu wa maisha ya wakfu, wakleri, familia na halmashauri ya walei, huna budi kuzingatia kwamba uhalisi wa vikundi hivyo unapatikana katika kanisa. Maandiko matakatifu yanatufundisha kwamba Kanisa ni mwili wa fumbo wa Kristu. Kama vile mwili unavyoundwa na viungo mbalimbali, vivyo na hivyo kanisa ambalo Kristo ni Kichwa chake na waamini ambao kulingana na vipaji, karama, miito na majukumu ya kila mmoja, ni viungo vyake. Kuhusu jambo hili, Paulo Mtume anatufundisha kwamba: Kanisa la Kristo ni kama mwili: mwili ni mmoja wenye viungo vingi. Lakini viungo vyote vya mwili huo ijapo ni vingi, huunda mwili mmoja. Kwa maana Sisi sote tumebatizwa kwa Roho mmoja kuwa mwili mmoja ..."1 — Hiyo ndiyo sifa na hulka yetu kama Wakristo.

Kutokana na hulka yake kama mwili wa Kristo, kanisa haliwezi kuwa na waamini wanaotambulika kuwa halisi na wengine wanaodhaniwa kuwa baki. Kama vile viungo ya mwili, kila mwamini ana hadhi, wito na utume wake.2 Sisi tumeingizwa ndani ya Kanisa au Mwili wa Fumbo wa Kristo kwa njia ya ubatizo. Kutokana na ukweli huo, kila mbatizwa anaitwa na kutumwa kuwa shahidi wa Ufufuko wa Bwana, jambo ambalo ni chimbuko na mhimili wa kanisa.3 Kwa maneno mengine kutokana na kusimikwa kwetu ndani ya kanisa, Sisi sote tumeaminishwa wito na jukumu la kukiri Imani yetu kwa maneno na kwa matendo.[1] Ni wazi kwamba licha ya kuwa viungo vya mwili mmoja, miongoni mwa waamini, kuna vipaji na miito mbalimbali kadiri anavyogawa Roho Mtakatifu. Hivyo havipaswi kukinzana kwa namna yoyote; vinatakiwa kukamilishana, kutegemezana na kuchangia katika kufanikisha usitawi wa kanisa. Kwa hiyo vipaji mabalimbali vinapaswa kupambanuliwa na kulelewa ili uwepo wake umtumkuze Mungu na kulifaa kanisa.5 Ndiyo maana kanisa limeagizwa naye Kristo Mfufuka kupeleka Habari Njema kwenye nja zote za dunia.[2] Nalo linapaswa kutekeleza utume huo kwa njia ya kila mmoja wa waana wake kulingana na wito wa kila mmoja.

WALEI: Kanisa ambalo ni Mwili wa Kristo, linaundwa na mafiga matatu yaani walei, watu wa maisha ya wakfu na wakleri. Kwa kuzingatia maudhui ya maadhimisho tunayoyafanya, hatutatumia muda kuzungumza kuhusu watu wa maisha ya wakfu na makleri; hilo tunalifanya siyo kwa minajili ya kubeza au kupuuzia, bali kwa nia ya kuzingatia zaidi lengo la maadhimisho na muda tuliopewa. Neno mlei au walei, linatokana na neno la Kigiriki yaani LAIKOS. Kwa kukosa uelewa wa kutosha na sahihi, baadhi ya watu hulibeza, au hata kulinyanyapaa jina hilo. Kimsingi lakini, mtazamo huo siyo sahihi na hakuna sababu za kufanya hivyo. Katika mazingira ya kanisa, neno laikos au mlei, linajitokeza hasa kwenye karne ya tatu baada ya Kristo. Katika matumizi ya awali neno au jina hilo lilimaanisha raia wa kawaida, tofauti na watawala au viongozi.[3] Nao Mtaguso wa pili wa Vatican umefafanua kwamba: " Kwa jina la walei kumaanisha ... waamini wote isipokuwa wale wenye Daraja takatifu na wenye hali ya watawa iliyokubaliwa katika Kanisa" .[4]

Ukisoma kwa makini Agano Jiipya, hasa Matendo ya Mitume, utabaini kwamba katika kanisa la mwanzo walikuwako walei maarufu, wake kwa waume, ambao walishirikiana na mitume katika jukumu la uinjilishaji; yatosha kuwataja wachahe kama: Priscilla na Akwila, Foebe, Epaneto, Maria, Androniko, Junia, Ampiato, Apolo, Trifonia,Trifosa, Persidia,Rufo, Asinkrito, Hermas, Filologo, Julia, Nereo na Olimpia.[5] Hawa waliheshimiwa na kutambuliwa siyo tu na mitume bali pia na wanakanisa wote. Mchango na ushiriki wao kama walei katika utume na usitawi wa kanisa la mwanzo ulikuwa wa kutukuka sana. Katika mapito ya muda, inaonekana kwamba ushiriki hai na thabiti wa walei ulizorota au kufifia. Yatakuwa yamechangia mengi. Kwa kiwango kikubwa kwa hiyo, walei walibaki kando. Wakati huo, ulishamiri mtazamo kwamba wajibu wa walei ni kusali, kulipa na kutii! [6]

Bila shaka mtazano huo siyo sahihi, lakini ikumbukwe kwamba hata katika zama zetu hizi, kwa bahati mbaya sana, hawakosekani baadhi ya walei na wakleri ndani ya kanisa ambao wanadhani mambo ndivyo yañavyotakiwa yawe. Katika hati juu ya Utume wa Walei, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaweka bayana kwamba kanisa haliwezi kuwepo bila utume wa walei, kwani utume huo unatokana na wito wa kila mwamini mlei kama Mkristo.ll Naye Papa Mstaafu Benedikto XVI akaweka msisitizo kwa kuainisha kwamba kwa njia ya uwepo wa walei, kanisa lipo na linatekeleza utume wake katika mazingira na makandokando mengi duniani. [7]

MTAGUSO MKUU WA PILI WA VATICAN:

Kwa njia na namna za ajabu, Mungu analiongoza kanisa lake takatifu katika mapito ya nyakati. Katika zama za 'kanisa la kitume' hasa katika miaka ya 1950, kulikuwa tayari na vuguvugu la kutafuta kupambanua maana na nafasi ya mlei na utume wake katika kanisa. Hakika, uamuzi wa kuitisha na kuadhimisha Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni tunda la uvuvio wa Roho wa Mungu kwa kanisa lake. Mtaguso huo, ambao ni kilele cha vuguvugu lililokuwa limejidhihirisha ndani ya kanisa kwa namna mbalimbali, ni jambo lililohitajika sana kwa usitawi wa kanisa. Kupitia Mtaguso huo, Roho Mtakatifu alileta upyaisho katika kanisa, vitengo vyake na utendaji wake. Bila kuvuruga hulka, utume na uhalisia wa kanisa, Mtaguso wa Pili wa Vatican uliruhusu hewa mpya kupenya ndani ya kanisa na pia kuondoa kutu la uchakavu lililougubika mtazamo, mahusiano na utendaji ndani ya kanisa la Mungu.

Ikumbukwe kwamba imepita zaidi ya miaka 50 tangu kuhitimishwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hata hivyo, tunaweza kutamka kwa unyofu na ukweli kwamba hadi leo hii, wengi katika kanisa, hatujaweza kuhitimisha jukumu la kuchambua, kujifunza, kuyasambaza na kutekeleza mafundisho yaliyotokana na mtaguso huo. Itawashangaza nikiwaeleza kwamba mpaka siku hizi, wako wengi ambao wakimegewa mafundisho yaliyomo ndani ya hati za Mtaguso wa pili wa Vatican hugwaya kwa mshangao huku wakidhani na kusema hiyo ni chachu mpya ambayo imechelewa kutufikia!!

CHIMBUKO LA UTUME WA WALEI NA HALMASHAURI YA WALEI

Ushiriki na ushirikishwaji wa walei katika uhai na utume wa kanisa siyo ruzuku bali ni wajibu na haki. Katika miaka iliyotangulia Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano huko Ulaya na maeneo ya ukatoliki wa kale Utume wa walei ulishamiri kama Aksio Katoliki (Catholic Action). Hapa na pale katika Bara la Afrika, wamisionari walianzisha mikakati ya utume wa walei kwa mtazamo na muundo wa Aksio Katoliki (Catholic Action).13 Jambo hili linashuhudiwa na tukio la Mkutano wa Kwanza wa Viongozi kuhusu Utume wa Walei Afrika ulijiri huko Kisubi, Uganda. Kwa msisitizo bayana, Mtaguso wa pili wa Vatikano unawataka wachungaji kutambua na kuenzi mchango wa walei katika utume na usitawi wa kanisa[8] Kwa mastahili ya kubatizwa, kushirikishwa Mwili wa Kristo na  Kristo. Kutokana na sababu hiyo, wanashirikishwa hadhi ya Kristo kuhani, nambue kuwa Kristo mbii na mfalme. Kwa hiyo, wanatakiwa kwa jinsi yao, kujihusisha na utume unaowapasa wakristo ndani ya kanisa na ulimwenguni kote 16 Kwa hiyo, tutawenyewe ndiye chimbuko na msingi wa utume wa waamini walei katika kanisa. Zaidi ya hayo, Roho Mtakatifu ambaye ni mpaji wa vipaji vyote ni chimbuko la utume wa kila mlei. Kutokana na mafungamano yake na Kristo na kuvuviwa na Roho Mtakatifu, kila mlei anao wajibu na haki ya kujihusisha na kushiriki kwa dhati katika utume wa kanisa.17

Katika uhalisia wa wa maisha yao, waamini walei wanaishi na kuwajibika katika mazingira ya kawaida ya maisha ya kila siku. Tunaweza kusema kwamba wanaishi usekulari, yaani hali ya kujihusisha na kushughulika ndani ya maisha ya kawaida au malimwengu. Katika hali hii, walei wamepewa Wito wa kuutafuta utakatifu kwa kujihusisha na mambo ya kawaida ya maisha na jamii. Kwa hiyo, ni Wito wa walei kuyatakatifuza malimwengu. Wanatakiwa kulitekeleza hilo kwa kujikita ndani yake kama chachu bora huku waking'aa fadhila za kimungu yaani Imani, matumaini na mapendo. Popote walipo wanatumwa kumwakisi Kristo aliye Nuru na anayewataka wao wenyewe wawe nuru ya ulimwengu (Mt.5:13-16). Mtaguso wa Pili wa Vatican unatufundisha kwamba kwa tabia na uhalisi Wake, utume wa walei unagusa njanja mbalimbali za maisha. Kwa uchache ieleweke kwamba katika kutekeleza utume wao ndani ya kanisa na katika jamii, walei wanapaswa..18

Kuinjilisha na kutakatifuza malimwengu. Kulea dhamiri kwa misingi ya maadili na tunu za kikristo. Kushirikiana na hierarkia kwa kuzingatia taaluma, weledi na mang'amuzi yao ili kutafiti, kuchambua na kuibua mipango sahihi itakayolisaidia kanisa kutekeleza utume wake vizuri zaidi. Kusitawisha wasifu na tabia ya kanisa karna jumuia (community) na kuufanya utume wake uzae matunda mengi na bora zaidi. Kutambua na kutii uongozi wa wenye daraja takatifu (hierarkia) ambao wana wajibu na madaraka ya kuidhinisha ushirikiano.

Sambamba na maelezo yaliyotangulia, ieleweke kwamba utume wa walei una msingi katika hulka, historia na jadi ya kanisa. Paulo Mtume anatufundisha kwamba: "Kwa nguvu ya neema niliyojaliwa ninawaambieni kila mmoja wenu: msijikadirie kupita kiasi kiwapasacho kujikadiria, bali jikadirieni kwa kiasi na kwa kadiri ya imani Mungu aliyowagawia kila mmoja wenu. Kwa maana kama tulivyo navyo viungo vingi katika mwili mmoja, lakini viungo vyote havina kazi moja, ndivyo Sisi tulio wengi ni mwili mmoja katika Kristo na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Basi tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mtu akiwa na kipaji cha unabii, usemi wake ulingane na imani. Mtu akiwa na kipaji cha utumishi, basi atumikie, na mwenye kipaji cha ualimu aelimishe. Mwenye kipaji cha faraja afariji. Mwenye kutoa kitu atoe kwa unyofu. Aliye msimamizi afanye bidii. Mwenye kufanya matendo ya huruma afanye kwa uchangamfu "19

Hakika, kulingana na fundisho hili hakuna hata mmoja asiye na fursa ya kuwa mshiriki hai katika utume wa kanisa, walei wakiwemo kikamilifu. Kwa hiyo, walei ni washiriki halali katika utume wa wokovu ambao kanisa limekabidhiwa na mwanzilishi wake yaani Bwana wetu Yesu Kristo. Ndivyo inavyopaswa kuwa kutokana na wito waliopewa kupitia sakramenti walizozipokea, hasa ubatizo na kipaimara. Kuendana na wito huo, waamini walei wameaminishwa jukumu au utume maalum, yaani hasa wajibu wa kuliwezesha kanisa kupenya, kuwepo na kuzaa matunda ya ufalme wa mbinguni katika mazingira ambayo kwa uhalisia wake ni wao tu wanaweza kujikita na kuwa chumvi na nuru ya ulimweng [9] Kwa njia hii, walei wanaweza kuitikia wito wa Kristu anayewataka wawe waenezaji wa ufalme wake wa ukweli, uhai,neema, haki, amani, uhuru, maendeleo bora ya watu na utakatifu popote dunian1.[10]

Kusudi walei washiriki vema katika utume mzima wa kanisa kadiri ya wito na karama zao, wanastahili kuwezeshwa kwa njia zifuatazo:[11] Kupewa ushirikiano wa hierarkia kwa kupatiwa miongozo na msaada wa kiroho; Kupewa mwelekezo sahihi ili utume uakisi usitawi wa kanisa lote. Kusaidiwa kuzingatia mafundisho sahihi na nidhamu ya kanisa. Kupatiwa malezi endelevu ili kumjenga mlei kiimani, kimaadili, kiroho na kitaaluma kadiri ya mazingira, msingi na majukumu ya kila mlei. Kupata uelewa na uwezo wa kupambanua na kukabili mambo mapya katika jamii, kanisa na ulimwengu. Kufundwa kuhusu tunu za kiutu na kikristu, hasa zile zinazohusu nidhamu ya maisha na mahusiano sahihi ya kiutu. Kuaminishwa kwa busara, baadhi ya majukumu ambayo kihalisi ni jukurnu la wachungaji. Kupata uelewa na msimamo wa kurnwona na kumtambua mwanadamu katika ukweli na uhalisia wake.

Kupatiwa mapadre waliothibitishwa kwa misingi ya upeo, maadalizi ya kitaaluma, nidhamu, ukomavu na mang'amuzi mapana ili wafanye kazi kwa karibu zaidi na walei . Kupata ushirikiano na msaada stahiki kutoka kwa watawa wa kike na kiume katika utume wao katika kanisa. Ili malengo hayo yafanikiwe, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vaticano walibaini umuhimu wa kuwahakikishia walei malezi stahiki katika nyanja zifuatazo. [12] Uinjilishaji na utakatifuzaji. Katika kipengele hiki, mkazo mkubwa umewekwa juu ya mbinu za mazungumzano. Kanisa na Upyaisho wa Malimwengu. Hapa, mkazo unawekwa katika kuwajenga walei kuelewa na kupambanua vema thamani na maana ya malimwengu, matumizi sahihi ya vitu, uongozi na uratibu wa taasisi, na umakini na uwajibikaji katika kushughulikia mafao ya wengi. Matendo ya upendo na huruma kama njia muhimu sana ya kutoa ushuhuda wa Kikristo. Mpaka hapa tumezungumza juu ya utume wa walei kwa ujumla. Ningependa kukumbusha kwamba, utume wa walei katika ujumla Wake, unamhusu mlei binafsi, vyama vya kitume, vuguvugu mbalimbali za imani (religious movements) na halmashauri ya walei katika ngazi zake mbalimbali. Ni muhimu tusiishie hapo, bali tujipe fursa ya kukitazama kwa namna ya pekee kipengele cha Halmashauri ya walei kwa mastahili yake chenyewe.

HALMASHAURI YA WALEI:

Maaskofu wa Baraza letu waliohudhuria Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, waliporejea baada ya hitimisho la Mtaguso wenyewe mnamo mwaka 1965, walidhamiria kuchambua, kusambaza na kutekeleza yale yaliyoibuliwa katika Mtaguso. Ilibidi wajipangie machakato wa kufanya hivyo. Ndiyo maana mwaka 1968 ukapangwa kuwa mwaka wa kuchambua na kushirikishana na wadau wote wa kanisa la Tanzania kwa njia ya semina na majadiliano. Mojawapo ya matokeo ya semina zile ni uamuzi wa kuundwa kwa kile ambacho awali kilijulikana kama Baraza la Walei. Huo ulikuwa ni uamuzi mzito na wa kihistoria ambao ulizindua zama mpya zilizoruhusu ushiriki wa hakika wa walei katika utume na uwajibikaji wa kanisa la Tanzania. Hata hivyo, ilibainika mapema sana kwamba jina lililotumika kubainisha utume huo wa walei lilikuwa na changamoto zake. Ikumbukwe kwamba jina huumba, hutoa dira, hujenga; lakini pia jina linaweza kupotosha na kusababisha mkanganyiko. Jina 'baraza la walei' lilibeba ndani yake hatari ya kuwafanya watu wadhani kwamba huo ni uongozi mbadala au kinzani na uongozi wa hierarkia, au kwamba waamini walei şaşa ni kanisa la peke yao. Kwa hiyo, ilibidi kufanya marekebisho ambayo yalipelekea kuamua kutumia jina la 'halmashauri ya walei' ambalo ndilo linalotumika hadi leo.

Ili kiweze kuwa na msimamo na mwelekeo sahihi na unaoeleweka, chombo hiki cha kitume kinachojulikana kama 'halmashauri ya walei', kina katiba. Pamoja na Mihimili mingine muhimu kama vile Neno la Mungu, Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Mkusanyo wa Sheria za Kanisa na Mkusanyo wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu Jamii, katiba ya halmashauri ya walei ni dira muhimu inayotakiwa kufahamika na kuzingatiwa ipasavyo na wadau wote. Vvombo hivyo kwa pamoja vinapaswa kufahamika kwa walei, wakleri na watawa ili diray dhima, ütendaji na mahusano yawe sawa na yenye tija kwa uhai wa kanisa lote. Kwa kuzingatia mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, [13] Katiba ya Halmashauri ya Walei inaweka bayana kwamba: "Halmashauri ya Walei ni chombo cha kitume kinachowaunganisha walei wote katika ngazi ya JNNK, Kanda, Vigango, Parokia, Jimbo au Taifa kutegemea ngazi husika. Ni chombo cha kitume kilichoundwa kwa ajili ya kushauri juu ya usitawi wa Utume wa Walei, kinachoendeshwa na Walei wenyewe waliochaguliwa kihalali chini ya ushauri na uongozi wa jumla wa viongozi wa Hierarkia "25

Ni muhimu sana kwa kila mhusika katika ngazi yoyote ya utume wa walei kuelewa na kuyazingatia maelezo hayo, kwani yanapozingatiwa inakuwepo nidhamu stahiki na utendaji usio na kuzozana kati ya wadau mbalimbali wa kanisa, inapaswa kueleweka bayana kwamba uwepo wa halmashauri ya walei si jambo la hiari bali ni hitaji la kisheria na la kichungaji. lli utendaji wa halmashauri ya walei uwe na ufanisi, kuna ulazima wa kujenga mtazamo sahihi na uelewa wa kutosha kuhusu kanisa. Jambo hili lisipozingatiwa muda, fursa na nguvu nyingi vyaweza kupotea katika malumbano au kukinzana kusiko na maana kati ya walei na hierarkia, kati ya walei na watawa, au hata kati ya walei wenyewe. Hilo hujidhihirisha pale makasisi wanapopuuza au kutoshirikisha walei. Kwa upande mwingine, mkwamo kama huo hutokea pia pale walei wanapodhani kwamba ushiriki na uwajibikaji wao unafuta madaraka na uwajibikaji wa makasisi. Kwa vyovyote vile, mambo hayo hulidhalilisha kanisa, kulidhoofisha, kukwamisha utume na kuwakwaza waamini na hata wafuatiliaji makini wasio wakristo. Kwa hiyo, wote tuwe makini. Katika yote, walei na wakleri watambue kwamba wameaminishwa uwakili ambao unawadai kushirikiana, kushirikishana na kukamilishana katika utendaji na ushuhuda unaowapasa. Kila mmoja akijijengea mtazamo na msimamo sahihi wa kiroho (Christian perception and spirituality), mlei na mkleri watatafuta kushughulikia usitawi wa kanisa na kuenea kwa Utawala wa Mungu.

UTUME WA WALEI NA FAMILIA: Uamuzi wa kuambatanisha mada ya familia na ile ya utume wa walei ni jambo linalobainisha mtazamo sahihi. Bila shaka, kwa kutazama juu juu, mtu anaweza kudhania kwamba usahihi huo unatokana na ukweli kwamba kwa kanisa la Tanzania, tunaadhimisha jubilee ya dhahabu ya utume wa walei sambamba na adhimisho la Mwaka wa Familia. Hata kama maadhimisho hayo mawili yasingeenda sambamba, bado ingebaki sahihi kuyatafakari pamoja. Kwa hakika, familia na walei ni mada mbili pacha na zinazoshabihiana katika kanisa. Kwa uhalisia wake, familia ni chimbuko la jamii na pia la kanisa. Kutokana na ukweli huo, familia inatambulika kuwa ni Kanisa la nyumbani. Harakati zote zinazolihusu kanisa na utume wake hazina budi kuanzia katika familia. Ndiyo kusema kwamba utume na uinjilishaji wote huanzia katika kanisa la nyumbni ambalo ni kitalu cha uhai na shule ya kwanza ya maisha.

Kwa mantiki hiyo Papa Yohane Paulo ll ametufundisha kwamba Familia ya Kikristu ni jumuia ya kwanza kabisa inayoitwa kueneza Injili, ikimsindikiza na kumlea mwanadamu katika hatua zote za kukua kwake ili afikie ukomavu wa kiutu na wa kikristu.27 Hatuwezi kutegemea kupata mafanikio katika nyanja nyingine zozote bila kuijali, kuilinda, kuitetea na kuisitawisha familia. Kwa hiyo, utume wa familia ni jukumu lisiloweza kuepukika. Katika kulichambua swala la utume wa familia, inatupasa kutafakari juu ya mazingira na changamoto zinazoikabili familia katika zama zetu hizi, ambapo licha ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika nyanja mbalimbali, hazikosekani changamoto. Ni vigumu kutafakari juu ya familia bila kugusia swala la ndoa. Tukumbuke kwamba ndoa kati ya mume na mkeni chimbuko la familia. Huu ni ukweli unaotokana na utashi wa Mungu ambaye amemwumba mwanadamu na kumbainisha kwa jinsia ya kiume na kike, na kuwataka wazae na kuongezeka.[14]

Kama chimbuko la familia, ndoa ya kikristo ni wito na utume. Ni wajibu wa kanisa kuwasaidia wanandoa na familia zao kuishi vema na kupata kukua, kukomaa na kukamilika katika wito wao huo. lli kanisa liweze kuutekeleza ipasavyo wajibu huo, linao wajibu wa kuyaelewa na kuyakabili ipasavyo mazingira yanayozikabili familia siku hizi. Yafuatayo ni kati ya mambo mazuri yanayozigusa familia katika zama hizi Kukua kwa dhana ya uhuru wa mtu kuchagua mume au mke kwa hiari yake.Kuimarika kwa utambuzi wa usawa kati ya mwanamume na mwanamke. Kuimarika kwa uelewa wa jamii kuhusu uhuru, haki za wanawake na utetezi wao. Kuimarika kwa mawasiliano na mshikamano kati ya watu wa jamii, marika na tamaduni mbalimbali. Kuboreka kwa huduma za afya na nyinginezo. Kwa upande mwingine, ikumbukwe kwamba wanandoa na familia wanakabiliwa na changamoto nzito na nyingi zikiwemo hizi zifuatazo: Mitazamo hasi kuhusu jinsia na ndoa.

Jambo hili linaenda sambamba na maswala ya baadhi kutetea ushoga na kudai kutambulika kwa ndoa kati ya watu wa jinsia moja. Jambo hili kwa bahati mbaya linabebwa, kutetewa na kugharimiwa na watu binafsi n ahata mashirika yenye uwezo mkubwa kiuchumi. Mambo yamifikia kiwango cha kuwepo kampeni na mashinikizo yanayolenga kunadi maelekeo hayo hasi. Kama wakristo na waafrika, hatuna budi kusimama kidete tukizingatia uadilifu, utakatifu wa ndoa na malezi yenye mwelekeo chanya. Kushamiri kwa ndoa za mseto. Hizi zina changamoto siyo tu zinazotokana na kukinzana kiimani lakini pia mtazamo kuhusu maana ya ndoa na malezi ya watoto. Kuongezeka kwa tatizo la talaka na ndoa nyingi kuvunjika. Hili linachangiwa na sababu nyingi kama vile ukomavu haba wa wanandoa kiutu, kisaikolojia, kijamii, kimaadili, kufungamana mno na malimwengu na kadhalika. Kukithiri kwa uchumba sugu na ndoa za majaribio.

Hili nalo linachangiwa na vitu kama umaskini, kutothubutu kujikita katika majukumu ya kudurnu (fear of serious and lasting commitments). Kuzorota kwa mtazamo na msimamo sahihi kuhusu utakatifu wa uhai. Hili linachangia kushamiri kwa vitendo vya matumizi ya vizuia mimba na utoaji mimba. Vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto ambavyo vinachukua sura ya: unyanyasaji, ukahaba, biashara haramu ya binadamu na hata utumwa mamboleo. Mambo haya na mengine yanayofanana nayo, yanalidai kanisa na wanakanisa kujizatiti ipasavyo ili kuweza kulinda, kutetea na kuinjilisha familia na mwanadamu kwa ujumla. Jukumu hili linawapasa walei, wakleri na watawa kushikamana ipasavyo. Wote kwa pamoja, wanalo jukumu la kichungaji la kuzisindikiza famia za kikristo kwa ukaribu, umakini na uwajibikaji wa hali ya juu, ili ziweze kutekeleza wito na wajibu wa kuwa jumuia ya uhai na upendo (Mdo.4:32). Kwa hiyo, Kanisa likitaka kuwa aminifu kwa Kristo ni lazima liweke msisitizo katika kuinjilisha na kutakatifuza familia. Hilo litafanyika kwa kuwajengea waamini shauku ya Neno la Mungu, katekesi endelevu, utamaduni wa kupenda sala, maisha ya sakramenti, ushiriki hai na makini katika maadhimisho ya liturjia, ushiriki hai katika jumuia kama kanisa la ujirani, utayari wa kujihusisha na matendo ya huruma na upendo na roho ya umisionari.

HITIMISHO: Ninapenda kuhitimisha kwa kuwapongeza walei wote wa kanisa Katoliki hapa Tanzania kwa kuadhimisha jubilee ya miaka 50, Imekuwa ni miaka ya kukua na kuwajibika kulikotukuka. Tunajiunga nanyi kumshukuru Mungu kwa matunda yaliyopatikana katika ngazi zote za uwepo na uwajibikaji wenu katika kanisa na jamii kwa ujumla. Baadhi ya matunda yaliyodhihirika katika miaka 50 ya utume wa walei katika kanisa la tanzania ni kama yafuatayo: Kuanzishwa na kusitawi kwa jumuiya ndogo ndogo za kikristo kama mkakati mahususi wa kuinjilisha. Ushiriki katika kuinjilisha na kutegemeza kanisa katika ndazi ya majimbo na baraza. Kuanzishwa kwa vyuo vikuu ya kanisa. Kuanzishwa kwa Benki ya Mkombozi. Kujengwa kwa kituo cha Bakanja. Kulea na kutegemeza miito mbalimbali katika kanisa.

Pamoja na mafanikio hayo, sote tutambue kwa unyofu kwamba yapo maeneo mbalimbali ambapo juhudi na ushiriki wa dhati zaidi vinatakiwa, ili kanisa lijibainishe zaidi na zaidi kama chumvi na nuru ya ulimwengu. Nitaje tu vipengele vichache kama vile: Kuimarisha familia kama kanisa la nyumbani katika zama hizi zenye changamoto lukuki. Kuimarsha jumuiya ndogondogo za Kikristo, hasa kwa kufanikisha ushiriki mzuri zaidi hasa wa wanaume na vijana. Kulea na kuimarisha moyo wa ushiriki, ukarimu na umiliki wa walei wote katika utume, mipango na mikakati ya kanisa. Kulea utayari wa kujitolea na kuwajibika ndani ya kanisa hasa bila kuhesabu au kujali masilahi binafsi kwa kukubali kukabidhiwa nyadhifa za uongozi katika ngazi mbalimbali za kanisa. Uthubutu wa kuishi Wito wa kila mmoja wa unabii kwa kutetea ukweli, haki, umoja, amani na masilahi ya wote bila kujihofia au kusukumwa na vigezo vya itikadi za vyama vya siasa, ukabila, matabaka ya kiuchumi, tofauti za kijinsia na hata matabaka ya wasomi na wasio wasomi.

Uthubutu wa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika jarnii na ngazi mbalimbali za siasa kwa msukumo wa dhamiri safi, nia ya kutumikia na kupania maendeleo ya wote na uzalendo unaotawaliwa na ukomavu, busara na ueledi 29. Kupania ukomavu na weledi unaotegemezwa na imani safi, upendo, ukarimu na mshikamano wa watoto wa Mungu, ili kuepuka misuguano na mivutano inayoleta vikwazo na kukwamisha usitawi wa kanisa.[15] Utayari wa kukuza, kushiriki na kutegemeza roho ya umisionari ili habari njema ya wokovu izidi kuenea. Katika hili, inatupasa sote kupambanua maeneo na mazingira yanayojikita na kujitokeza kuwa na tabia ya pembezoni mwa jamii na kanisa. Katika mazingira hayo ya pembezoni, wanapatikana watu waliosahauliwa pengine na jamii, serikali na kanisa.[16] Kanisa haliwezi kamwe kuvumilia kuwepo kwa watu waliotengwa au kusahauliwa, kwani agizo la Yesu kwa wafuasi wake ni: "Nendeni duniani kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe" (Mk.16:15). Kupania utakatifu kwa uelewa kwamba huo ni wito wa msingi wa kila mbatizwa (Mt.5:48).[17] Kila mwamini anaalikwa na kuhimizwa kuchuchumilia utakatifu kwa kukuza tunu zifuatazo:

Uelewa na ushiriki makini, wenye ukomavu na staha katika maadhimisho ya liturjia na ibada nyingine za kanisa. Katika zama hizi za saya$i na teknolojia, wengi wanaelekea kuburuzwa na vyombo vya mawasiliano kama vile simu. Ninawaalika wote kuwa makini ili £itawaliwe na mkanganyiko au utoto wa mtandaoni, au janga la kugeuza mtandao kuwa ni mungu wa uongo. Bahati mbaya, hilo lipo. Kukuza moyo wa sala na ibada binafsi na za pamoja. Kujitahidi kujijengea na kukuza mtazamo, uelewa na mwelekeo wa kiroho (spirituality) wa kila mlei.[18] Kusitawisha utamaduni na nidhamu ya kulisoma, kusali na kutafakari Neno la Mungu. Kulenga moyo na utayari wa uwajibikaji kwa njia ya kazi halali na adilifu, kusudi kupunguza ombwe la umaskini linalowasakama wengi na kwa baadhi likiandamana na tamaa ya kupata mafanikio kwa kutumia njia zisizo halali wala adilifu.

Kujali, kuheshimu na kutetea uhai wa mwanadamu katika awamu zote za uwepo wake, tangu kutungwa mimba hadi aitwapo na Mungu. Kuhuisha Tabia ya kujali, kutunza na kutumia mazingira kwa adabu, shukrani, ukarimu, mwono wa mbali na heshima kwake Muumba. Wapendwa, ninawaombea uvuvio wa Roho Mtakatifu ili awahuishe na kubidisha mnapoanza safari ya kuelekea jubilee ya miaka mia moja ya utume wa walei katika kanisa la Tanzania, Amecea, SECAM na ulimwengu mzima.

Askofu Mkuu Mwandamizi Thaddaeus Ruwa'ichi OFMCap., - Dar es Salaam.

[1] LG.II

 LG.12

[2] Mk.16:15-16; Mt.28:19-20; Lk.24:4648; Yn.20:21-23.

[3] DOWNEY, Michael (ed.): The New Dictionary of Catholic Spirituality.Bangalore, TPI, 1995, pg.590.

[4] LG.31

[5] Mdo.18:26, Rum.16:1-16.

[6] DWYER, Judith A. The New Dictionary of Catholic Social Teaching. Collegeville, The Liturgical Press,1994 pg.539. (Art. By Dennis P. McCann: The Role of the Laity) '"Prior to Vatican Il, ordinary parioshioners could be forgiven for assuming that the role of the laity was to 'pay, pray and obey."'

[7] Benedict XVI: Africae Munus Nr.128

13 CLEIRE, R. What is lay Apostolate. In: The African Enchiridion (Edited by Oseni Ogunu), Vol. l, Bologna, EMI, 2005. Article 21, pg.86 Catholic Action is an apostolate of the lait y. .. Inthis sense, Catholic Action is a universal apostolate. It ia not restricted to any category of lay people." 14 Ibid. pg.83

[8] LG.30

[9] L(3.33

[10] LG.36

[11] AA.24-25, 28-29.

[12] AA .31

[13] AA, Nr.20d "Walei ama kwa kujitolea kwa hiari ama kwa kualikwa kufanya kazi na kushirikiana moja kwa moja na utume wa hierarkia, wanatenda kazi chini ya uongozi mkuu wa Hierarkia yenyewe, ambayo yaweza kuidhinisha ushirikiano huo pia kwa njia ya agizo (mandatum) rasmi." 25 Rasimu ya Katiba ya Halmashauri ya Walei, 2018

[14] Mwa.1:27-28; 2:21-24.

[15] AA.23

[16] RICCARDI, Andrea: TO The Margins — Pope Francis and the Mission of the Church. New York, Orbis, 2018.

[17] Tazama pia: Law. 11:44; 19:2; Kumb. 18:3; Yn 3:3; Yak. 1:4; IPet. 1:16; Africae Munus NR.129.

[18] AA.4 "Lay spirituality Will take its particular character from the circumstances of one's state of life.

21 June 2019, 13:31