Tafuta

Vatican News
Kardinali Crescenzio Sepe: Bahari ya Mediterrania imekuwa ni kaburi la maskini mamboleo wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi! Kardinali Crescenzio Sepe: Bahari ya Mediterrania imekuwa ni kaburi la maskini mamboleo wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi! 

Bahari ya Mediterrania imekuwa ni kaburi la maskini mamboleo!

Bahari ya Mediterrania imekuwa ni kaburi la maskini, wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kuna haja ya kuwaandaa waamini watakaoweza kusikiliza na kujibu kilio cha maskini mamboleo. Ni fursa ya kujenga na kudumisha mshikamano wa huduma ya upendo; kwa kulinda na kutetea: maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Crescenzio Sepe, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Napoli, Italia, anapenda kuchukua fursa hii, kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko Jimboni Napoli, Ijumaa, tarehe 21 Juni 2019 ili kushiriki katika kongamano la kitaalimungu, baada ya kuchapishwa kwa Katiba ya Kitume: “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli”. Kongamano limeandaliwa na Kitivo cha Taalimungu, Chuo Kikuu cha Kusini mwa Italia, Kitengo cha San Luigi. Hii ni changamoto kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli, unaowawezesha hasa wanawake kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Si kawaida sana kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kushiriki katika makongamano.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa ndugu zake Wayesuit, ili kusaidia mchakato wa kutangaza na kushuhudia Ukweli unaobubujika kutoka katika Injili, tayari kuumwilisha katika maisha ya: Kijamii, kitamaduni, kisiasa na kidini. Lengo ni kuendeleza mahusiano na mafungamano kati ya: Taalimungu na Shughuli za Kichungaji; Kati ya Maisha na Imani; changamoto kubwa iliyovaliwa njuga na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hati ya “Optatam Totius” yaani “Upyaisho wa Kanisa lote unaotamaniwa: Malezi ya Waseminari” unakazia pamoja na mambo mengine: Malezi  na makuzi ya wito wa Kipadre; Marekebisho ya Masomo ya Kikanisa; Mwongozo wa Malezi mahususi kuhusu shughuli za kichungaji; majiundo na malezi endelevu baada ya kupewa Daraja Takatifu!

Lengo ni kuwawezesha viongozi wa Kanisa kuwa na utambuzi mpana katika maisha ya kiroho, kiakili na katika shughuli za kichungaji. Neno la Mungu halina budi kupewa kipaumbele cha kwanza katika malezi na makuzi ya Kipadre; Ushiriki mkamilifu wa Liturujia na Mafumbo ya Kanisa pamoja na kukuza ari na moyo wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha maskini wa nyakati hizi! Kardinali Crescenzio Sepe, anasema, Ukanda wa Bahari ya Mediterrania una utajiri mkubwa, lakini kwa miaka ya hivi karibuni, Bahari ya Mediterrania imekuwa ni kaburi la maskini, wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Ni watu wanaokimbia vita, umaskini, dhuluma, nyanyaso na ukosefu wa fursa za ajira.

Hii ni changamoto inayofanyiwa kazi, ili kuwaandaa majandokasisi, watakaoweza kusikiliza na kujibu kilio cha maskini katika ulimwengu mamboleo. Ni fursa ya kujenga na kudumisha mshikamano wa huduma ya upendo; kwa kulinda na kutetea: maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani na matumaini duniani; kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kubomolea mbali kuta za utengano zinazojengwa kutokana na maamuzi mbele. Ukanda wa Mediterrania unapaswa kuwa ni Jukwaa la majadiliano, haki, amani na udugu wa kibinadamu. Bahari ya Mediterrania ni mali na utajiri wa wote ndiyo maana inaitwa “Mare nostrum”, changamoto na mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpya wa maisha unaothamini na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Napoli, inamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchagua Napoli, kuwa ni mahali pa tafakari ya kina kuhusu Furaha ya Ukweli katika maisha ya Kikristo. Kongamano linahudhuriwa na watu wachache, lakini Jimbo kuu la Napoli, ni kitovu cha habari katika siku hizi mbili! Hii ni mara ya tatu kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Jimbo kuu la Napoli!

Papa: Napoli 2019
20 June 2019, 10:41