Tafuta

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo wake wa karibu miongoni mwao! Familia ya Mungu Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo wake wa karibu miongoni mwao! 

Papa Francisko Camerino: Jipe moyo! Inuka! Anakuita!

Kwa uwepo wa Papa Francisko miongoni mwao, wameyasikia tena maneno ya Yesu akisema “Jipe moyo; inuka, anakuita”. Huu ni ujasiri wa kusimama tena baada ya kuelemewa na machungu ya tetemeko la ardhi pamoja na kutambua kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwasahau watoto wake. Huu ni wakati wa kusimama na kuanza kutembea kwa kujikita katika upya wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Francesco Massara wa Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche, Italia, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 16 Juni 2019 wakati wa Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, kutembelea Jimboni humo amesema kwamba, watu wa Jimboni mwake ni wakarimu na wachapakazi; ni watu walioguswa na kutikiswa sana katika maisha na imani, lakini bado wana ujasiri wa kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo kama ilivyokuwa kwa mwa wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu aliyepaaza sauti yake na kusema, “Mwana wa Daudi, Yesu, Unirehemu” (Mk. 10:46-52).

Licha ya “wapambe nuksi” kutaka kumfunga mdomo, lakini Bartimayo akapaaza sauti kiasi cha kumfikia Kristo Yesu na watu wakamwambia “Jipe moyo; inuka, anakuita”. Eneo hili limesheheni utajiri wa historia, ukarimu, uhuru pamoja na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, lakini tetemeko la ardhi, limewatumbukiza wananchi hawa katika upofu, kiasi cha kuwaondolea amani na utulivu wa ndani. Tetemeko la ardhi limewajengea huzuni na uchungu moyoni kwa kuwapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao bila kusahau mali na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu. Wanatamani kusimama tena, ili kuendelea na safari ya maisha!

Tetemeko la ardhi limesababisha maafa makubwa, limewajeruhi watu na kuwaondolea matumaini na hasa zaidi kutokana na kusuasua kwa ujenzi na ukarabati wa majengo na miundo mbinu iliyoharibiwa, hali ambayo inawakatisha watu wengi tamaa ya maisha, kiasi cha kudhani kwamba, wamepokwa maisha ya mbeleni! Kanisa hili ambalo limeguswa, limejaribiwa na kutikiswa vibaya, bado halijakata tamaa kama ilivyokuwa kwa mwana wa Timayo, Bartimayo yule mwombaji kipofu! Kanisa bado linaendelea kupaaza sauti ya kilio cha mateso, ili kuwajengea matumaini watu wa Mungu, waweze kusimama tena katika imani, kwa kutambua uwepo wa neema ya Mungu, inayowasindikiza licha ya giza nene ambalo limeufunika uzoefu wao.

Kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao, wameyasikia tena maneno ya Kristo Yesu akisema “Jipe moyo; inuka, anakuita”. Huu ni ujasiri wa kusimama tena baada ya kuelemewa na machungu ya tetemeko la ardhi pamoja na kutambua kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwasahau watoto wake. Huu ni wakati wa kusimama tena na kuanza kutembea kifua mbele kwa kujikita katika upya wa maisha, tayari kuyashughulikia maisha yao kwa utu na heshima kama watoto wa Mungu, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake. Askofu mkuu Francesco Massara anasema, Mwenyezi Mungu daima anaendelea kuwaita waja wake wanaopaswa kutikia na kujibu pendo lake linalowaletea wongofu na upya wa maisha, ili kuambata umoja katika imani na upendo unaomwilishwa katika matendo, kielelezo makini cha imani tendaji.

Neno lake la faraja limekuwa ni mwanga angavu ambalo limewasaidia kumtafakari Mungu na maana ya maisha. Familia ya Mungu Jimboni humu linamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwepo wa Baba Mtakatifu kielelezo cha: huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika mchakato wa uinjilishaji na ushuhuda wa imani. Kwa hakika wanashuhudia kwamba, wanapendwa na wamefarijika sana kwa uwepo wake na kwamba, wanaendelea kumsindikiza katika sala na sadaka zao, ili aendelee kutekeleza vyema dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Askofu mkuu Camerino
16 June 2019, 16:24