Tafuta

Vatican News
Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC katika ujumbe wa Pentekoste kwa Mwaka 2019 linawataka Wakristo kuwa ni mashuhuda wa ukweli na upendo katika maisha yao! Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC katika ujumbe wa Pentekoste kwa Mwaka 2019 linawataka Wakristo kuwa ni mashuhuda wa ukweli na upendo katika maisha yao!  (ANSA)

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Ujumbe wa Pentekoste 2019

Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia ukweli. Huu ni ukweli unaoganga na kuponya; ukweli wa upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Mitume wa Yesu walikuwa ni watu wa kawaida, wasiokuwa na elimu wala na maarifa, lakini walikuwa na nguvu na ujasiri waliokirimiwa na Roho Mtakatifu. Ulimwengu unawahitaji mashuhuda wa upendo na ukweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., katika Ujumbe wake kwa Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2019 linasema, Pentekoste ni Siku kuu, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume na kuwakirimia Mapaji yake saba. Ni sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa. Mitume waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, wakawa na nguvu na ujasiri wa kutoka kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Mwinjili Luka anasema, Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. (Mdo. 2:18).

Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia ukweli na kwamba, hakuna mtu au kikundi chenye hati miliki ya ukweli unaowafumbata wote; ukweli unaoganga na kuponya. Huu ndio ukweli wa upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Mitume wa Yesu walikuwa ni watu wa kawaida, wasiokuwa na elimu wala na maarifa, lakini walikuwa na nguvu na ujasiri waliokirimiwa na Roho Mtakatifu. Ulimwengu unawahitaji mashuhuda wa ukweli, watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ili kufikia azma hii, kuna haya ya toba na wongofu wa ndani linasema Baraza la Makanisa Ulimwengu, ili kukazia fadhila ya upendo kati ya watu. Ukweli hauna budi kutafutwa na kudumishwa, kwa kuzingatia utakatifu wa maisha ya watu; utu, heshima na haki zao msingi. Ukweli unadumishwa kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kama amana na utajiri wa kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuitunza na kuiendeleza. Ukweli uwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata haki na kudumisha amani.

Baraza la Makanisa linasema, Sherehe ya Pentekoste ni kumbu kumbu ya kuzaliwa kwa Kanisa linalowaunganisha watu wote wa dunia katika lugha ya upendo. Huu ndio mwanzo wa Jumuiya ya ukweli inayotumwa kujitosa kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Hii ni huduma inayofumbatwa katika Injili ya upendo. Upendo unavunjilia mbali maamuzi mbele; sera za chuki na uhasama zinazotaka kuwagawa na kuwasambaratisha watu.

Upendo unaheshimu na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kukuza uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini: Upendo ni kinyume kabisa cha vitendo vya kigaidi vinavyotishia: usalama, maisha na mafungamano ya kijamii. Dhana ya upendo, haki na amani ni chachu ya kuganga na kuponya madonda ya kashfa ya uchoyo, ubinafsi na dharau kwa wengine. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa sababu pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika nyoyo zao na Roho Mtakatifu waliopewa wao!

Katika maisha na utume wa Kanisa, waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia ukweli kuhusu: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kulinda na kuendeleza uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; kwa kukazia maendeleo fungamani ya binadamu; kwa kuheshimu mazingira nyumba ya wote pamoja na kuwa na uelewa sahihi mintarafu mpango wa Mungu kuhusu haki na amani. Kwa njia ya Roho Mtakatifu Kanisa litaendelea kushikamana ili kutafuta, kutangaza, kushuhudia na kuishi ukweli! Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawatakia Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema amani na utulivu katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste.

WCC: Pentekoste 2019
07 June 2019, 12:12