Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, kwa sasa hali ni tete sana nchini humo kwani watu wengi wamekata tamaa ya maisha! Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, kwa sasa hali ni tete sana nchini humo kwani watu wengi wamekata tamaa ya maisha! 

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya: Hali ni tete sana!

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya: hali ya wananchi wengi wa Kenya wamekata tamaa kutokana na umaskini; vijana wengi wakijinyonga; tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili zinaendelea kumong’onyoka pamoja na kupanuka kwa saratani ya rushwa. Utawala wa sheria bado ni kitendawili. Wafanyakazi wanaendelea kusubiri sheria ya marekebisho ya kodi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, katika Tamko lake Kuhusu Hali ya Nchi ya Kenya, linagusia: hali ya wananchi wengi wa Kenya kukata tamaa kutokana na umaskini; vijana wengi wakijinyonga; tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili zikiendelea kumong’onyoka pamoja na kupanuka kwa saratani ya rushwa nchini Kenya. Utawala wa sheria bado ni kitendawili nchini Kenya! Wafanyakazi wanaendelea kusubiri sheria ya marekebisho ya kodi pamoja na changamoto ya kukua kwa deni la taifa.

Katika kushughulikia, matatizo, kero na changamoto zote hizi, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linavitaka vyombo vya sheria kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Kenya! Maaskofu wanasema, Mama Kanisa anapoendelea kusherehekea Fumbo la Pasaka, wanapenda kuwatuma ujumbe wa matumaini kwa wale wote waliokata tamaa katika maisha, kiasi hata cha kuthubutu kutema zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haya ni matokeo ya saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma; uchu wa madaraka na utajiri wa haraka haraka; mambo yanayoendelea kuwadidimiza wananchi wa Kenya katika medani mbali mbali za maisha.

Kuna baadhi ya wanasiasa wanaokumbatia madaraka kwa ajili ya mafao binafsi na wala si kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani kwao tunu hizi si mali kitu! Inasikitisha kuona watu wanakufa kwa baa la njaa nchini Kenya, wakati ambapo “vigunia vya fedha ya dharura” iliyotengwa na Serikali vinayeyuka na kupotea katika mazingira tatanishi! Maaskofu wanasikitishwa sana na wimbi kubwa la vijana nchini Kenya kuamua kujinyonga hadi kufa, hali ambayo imeanza kuzoeleka katika vyombo vya mawasiliano ya jamii! Lakini hii si sawa, kuna mambo ambayo yanawapelekea vijana wa kizazi kipya hata kuamua kufanya maamuzi machungu kama haya katika maisha yao.

Ukweli wa mambo lazima usemwe, watu wamekata tamaa na wengi wanakabiliwa na ugonjwa wa sonona. Vijana wengi hawana fursa za ajira na baadhi yao wamekosa malezi na majiundo makini, kiasi hata cha kutumbukia katika upweke hasi unaowazamisha katika utamaduni wa kifo! Vijana wengi wameshindwa kupata mifano bora ya kuigwa kutoka katika jamii na matokeo yake ni: machafuko, kinzani na mahangaiko ya wananchi wa Kenya katika ujumla wao! Utu, heshima, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga, ili kuliokoa Taifa la Kenya linalokwenda mrama!

Maaskofu wanaendelea kudadavua hali halisi ya maisha ya wananchi wa Kenya kwa kusema kwamba, kwa sasa kuna mmong’onyoko mkubwa wa tunu msingi za maisha ya: kiroho, kiutu na kimaadili. Matokeo yake ni mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, rushwa na ufisadi wa mali ya umma; uchoyo, ubinafsi na uchu wa fedha na utajiri wa haraka haraka. Utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu ni mambo yanayoonekana kupitwa na wakati, lakini hizi ndizo tunu zinazowaunganisha watu na kukoleza mafungamano ya kijamii, tayari watu kusimamia: utu, heshima, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma, vinawameng’enyua sana wananchi wa Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka wananchi kusimama kidete ili kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa; kwa kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unatekelezwa na vyombo vyote vinavyohusika, ili kweli haki iweze kutendeka. Watu wanaokula rushwa pamoja na mafisadi, wanaonekana kuwa juu ya Sheria, wakati ambapo wananchi wengi wanatumbukia katika ombwe la umaskini wa hali na kipato. Maaskofu wanasema, rushwa na ufisadi vipigwe vita kuanzia kwenye familia, jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na katika medani mbali mbali za maisha kwa kukemea na kukataa kutoa wala kupokea rushwa kwani ni adui wa haki. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo, furaha, haki na amani.

Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wawe mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia uaminifu na uadilifu; ukweli na uwazi katika maisha na utendaji wa shughuli zao. Umefika wakati wa kukuza na kudumisha dhamiri nyofu, ili kutambua mabaya yanayopaswa kuachwa na wema, unaopaswa kukumbatiwa na kuendelezwa. Ugawaji wa madaraka na nafasi za kazi uzingatie kanuni maadili na sheria za kazi. Kumbe, kuna haja ya kuondokana na uchoyo na ubinafsi unaoendelea kuota mizizi katika akili na nyoyo za wananchi wa Kenya; kwa kujikita katika ukweli na uaminifu, utu na heshima ya binadamu.

Ukabila, upendeleo, udini na umajimbo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati hayana mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Kenya. Migomo mbali mbali inayofanywa na makundi ya kijamii inahitaji kupewa suluhu ya kudumu, kwa kudumisha haki, amani na maridhiano ndani ya jamii. Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, rushwa na ufisadi wa mali ya umma, vinaendelea kusababisha majanga mengi kwa taifa, kwani, deni la taifa limeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Watu wanajiuliza, Je, deni hili litalipwa na nani? Wakati fedha inaingia mifukoni mwa watu binafsi?

Ulipaji wa deni la taifa, utaendelea kukwamisha mchakato wa huduma na maendeleo fungamani nchini Kenya! Wafanyakazi wanasikitishwa na kodi kubwa wanayotozwa kiasi hata cha kushindwa kumudu mahitaji msingi katika familia zao. Umefika wakati wa kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unapewa kipaumbele, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sheria ishike mkondo wake, wale wote watakaotiwa hatiani, washughulikiwe kikamilifu. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupambana na saratani ya rushwa, hadi kieleweke! Wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na mshikamano wa kitaifa. Huu ni wakati wa kutafuta mema na wala si mabaya, ili wapate kuishi na Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja nao daima!

Maaskofu Katoliki Kenya
18 May 2019, 16:26