Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Siku ya Wafanyakazi 2019: dumisheni Rasilimali watu katika uzalishaji na huduma! Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Siku ya Wafanyakazi 2019: dumisheni Rasilimali watu katika uzalishaji na huduma! 

Siku ya Wafanyakazi Duniani 2019: CEI: Dumisheni Rasilimali Watu

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI: Linasema, kati ya changamoto kubwa zinazowaandama wafanyakazi nchini Italia ni maendeleo makubwa ya teknolojia, uhaba wa fursa za kazi; umuhimu wa kuwahusisha watu wasiokuwa na ajira katika maisha ya kijamii, ili nao waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya jamii. Ujumbe huu unaongozwa na kauli mbiu “Rasilimali watu katika huduma ya kazi”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wafanyakazi Duniani, inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo Mei Mosi, iwe ni fursa ya kutambua kwamba, kazi ni utimilifu wa utu, heshima na maisha ya binadamu. Hii ni nafasi ya kukuza na kudumisha: uhuru na ushiriki mkamilifu wa wafanyakazi katika mchakato wa uzalishaji mali na utoaji wa huduma kwa kuhamasisha kipaji cha ugunduzi na kuimarisha sheria za kazi, utawala bora na usalama kazini. Siku kuu ya Wafanyakazi imewekwa chini ya ulinzi wa Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi na mtu mwenye haki. Siku kuu hii kadiri ya Mapokeo ya Kanisa ilianzishwa kunako mwaka 1955 na Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili.

Mababa wa Kanisa daima wamekuwa wakikazia tunu msingi za kazi, ili mtu asiwe mzigo kwa wengine, lakini afanye kazi hivyo kwamba aweze kuishi na hatimaye, kujitosheleza kwa mahitaji yake msingi. Kazi ni wajibu na inaheshimu vipaji na karama ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake. Kazi ni sehemu ya ukombozi na mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa katika kazi, changamoto na mwaliko wa kuheshimu kazi na waswahili wanasema, chezea mshahara na wala si kazi! Jamii ijifunze pia kuwaheshimu na kuwaenzi wafanyakazi. Licha ya changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa wafanyakazi, lakini watambue kwamba, kama wazazi na walezi wanawajibika barabara katika malezi na makuzi ya watoto wao. Wazazi wawafundishe watoto wao umuhimu wa kuthamini kazi na wawe tayari kufanya kazi halali ili kujipatia riziki yao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika ujumbe wake kwa Siku ya Wafanyakazi Duniani, 2019 linasema, kati ya changamoto kubwa zinazowaandama wafanyakazi nchini Italia ni maendeleo makubwa ya teknolojia, uhaba wa fursa za kazi; umuhimu wa kuwahusisha watu wasiokuwa na ajira katika maisha ya kijamii, ili nao waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya jamii. Ujumbe huu unaongozwa na kauli mbiu “Rasilimali watu katika huduma ya kazi”. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yameiwezesha familia ya Mungu nchini Italia kuzalisha bidhaa na huduma, kiasi cha kuchangia ukuaji wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia katika nyanja mbali mbali, kiasi cha kuwawezesha walaji kuwa na uchaguzi mpana zaidi katika bidhaa na huduma bora inayotolewa sokoni.

Lakini, upande mwingine wa medali hii wanasema Maaskofu Katoliki wa Italia, ni ukosefu wa mgawanyo sawa wa rasilimali za nchi ili kutoa fursa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa maendeleo ya sayansi na teknolojia kujisikia tena kuwa ni sehemu ya mafungamano ya kijamii. Maendeleo haya pia yamekuwa ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, kiasi hata wakati mwingine, fursa za kazi na ajira, zinayeyuka kama ndoto ya mchana na kuwaacha wananchi wengi wakiogelea katika dimbwi kubwa la umaskini na hali ya kukata tamaa! Kila mwaka wananchi wasiokuwa na fursa za ajira nchini Italia wanaongezeka maradufu. Matokeo yake ni kuongezeka kwa umaskini, utu na heshima ya wafanyakazi ni mambo yanayoendelea kuporomoka kila kukicha! Hali hii inawaacha watu wengi wakiwa wamekata tamaa na hivyo kushindwa kuwekeza zaidi katika leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linakaza kusema, ili kuweza kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; kuna haja ya kushirikiana na kushikamana, ili maendeleo ya sayansi na teknolojia yaende sanjari na maboresho ya rasilimali watu, kwa kuwajengea wafanyakazi uwezo mpana zaidi wa kufikiri na kutenda, daima wakiongoza mageuzi ya teknolojia na kamwe wasiburuzwe na mabadiliko haya, kiasi cha kujikuta hawana ajira, kwa mashine kuchukua nafasi zao. Katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani nchini Italia, Maaskofu wanaendelea kukazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii katika maeneo ya kazi; kudumisha ujirani mwema kama kikolezo cha uzalishaji na utoaji wa huduma bila kusahau mwingiliano wa kijamii kati ya wafanyakazi wenyewe!

Kumbe, sera na mikakati ya kazi inapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa mafunzo na elimu kazini ili kuendeleza maboresho ya uzalishaji na huduma inayotolewa kwa watu wa Mungu. Pili ni kuhakikisha kwamba, mchakato wa umoja, ushirikiano na mafungamano kati ya wafanyakazi na viongozi wao yana boreshwa; wafanyakazi wanalipwa stahiki zao barabara na kwa jinsi hii, rasilimali watu inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika mfumo mzima wa uzalishaji na utoaji huduma. Ikiwa kama mambo haya yatazingatiwa, kwa hakika kutakuwepo na maboresho makubwa ya rasilimali watu na hivyo kuongeza: weledi, tija na ubora wa bidhaa na huduma inayotolewa. Cheche za maboresho haya zitajionesha hata katika maisha ya kawaida na tunu msingi za maisha ya kiroho.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani linasema, changamoto pevu kwa sasa hivi nchini Italia ni kuhakikisha kwamba, “maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanashirikishwa kikamilifu katika maisha ya kijamii na kamwe wasisukumizwe pembezoni mwa jamii. Wajengewe matumaini, ukarimu na kupewa fursa za kuweza kujiongeza katika maisha kadiri ya nafasi na uwezo wao. Hakuna sababu ya kujifungia katika woga na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko, bali watambue na kuthamini kwamba, jirani zao ni watu wanaopaswa kuthaminiwa na wala si kutwezwa na kubezwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linahitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, amana na dhamana ya jamii makini ni kuhakikisha kwamba ustawi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii, yawe ni kikolezo cha mshikamano na mafungamano ya kijamii, kwa ajili ya mafao ya wengi. Kwa njia hii, familia ya Mungu nchini Italia, itaweza kushinda changamoto ya kuporomoka kwa utu na heshima ya wafanyakazi katika nyakazi hizi na zile zijazo!

Mtakatifu Yosefu

 

01 May 2019, 15:59