Tafuta

Vatican News
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linawataka vijana kubaki Afrika kwani kwenda ughaibuni kama wahamiaji na wakimbizi ni hatari kwa maisha yao! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linawataka vijana kubaki Afrika kwani kwenda ughaibuni kama wahamiaji na wakimbizi ni hatari kwa maisha yao! 

Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi: Vijana Bakini Afrika!

Kuna umati mkubwa wa vijana wanaokimbia:vita, umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi, wanatafuta fursa za ajira na kazi pamoja na kuwa na hamu ya kuboresha maisha yao! Vijana hawa huko njiani wanakumbana na kifo kinachowakodolea macho. Kumbe, Kanisa linapaswa kuwa ni Sakramenti ya matumaini, kwa vijana wa kizazi kipya! Ughaibuni, mambo ni tete sana vijana! Msithubutu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, RECOWA-CERAO limehitimisha mkutano wake wa mwaka uliozinduliwa tarehe 13 Mei 2019 na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye katika hotuba yake elekezi alisema, mkutano mkuu wa Pili wa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Afrika Magharibi, uliofanyika kunako mwaka 2016 ulikazia zaidi: Upatanisho, maendeleo na familia kama changamoto za uinjilishaji Afrika Magharibi.

Leo hii, anasema kuna haja ya kuongeza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kama sehemu ya uinjilishaji, ili kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu sanjari na uporaji wa rasilimali na utajiri wa Afrika ya Magharibi unaofanywa na makampuni makubwa ya kigeni, wakati kuna maelfu ya watu wanaoendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini, machafuko na vita! Mkutano huu wa tatu, umekuwa ukiongozwa na kauli mbiu “Uinjilishaji mpya na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, Familia ya Mungu Afrika Magharibi” umehitimishwa rasmi tarehe 20 Mei 2019, huko Ouagadougou, nchini Burkina Faso.

Kwa masikitiko makubwa Maaskofu kutoka Afrika Magharibi wanasema, wanafuatilia kwa hofu na mashaka makubwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Afrika linaloelekea Barani Ulaya. Kuna umati mkubwa wa vijana wanaokimbia:vita, umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi, wanatafuta fursa za ajira na kazi pamoja na kuwa na hamu ya kuboresha maisha yao! Vijana hawa huko njiani wanakumbana na kifo kinachowakodolea macho. Kumbe, Kanisa linapaswa kuwa ni Sakramenti ya matumaini, kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kuwashirikisha kwa ukamilifu zaidi katika maisha na utume wa Kanisa! Vijana wanapaswa kuelewesha hatari, changamoto na matatizo wanayoweza kukumbana nayo kama wahamiaji na wakimbizi.

Kwanza kabisa, wanaweza kutumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo! Haya ni mambo yanayodhalilisha utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi. Ujinga, umaskini, magonjwa, vita, ukosefu wa fursa za ajira na kazi, kinzani pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kati ya matatizo makubwa yanayoikabili familia ya Mungu Barani Afrika katika ujumla wake. Maaskofu wanakiri kwa hakika kwamba, nchi nyingi Barani Afrika, haziwezi kuzima kiu ya furaha na ndoto ya matumaini ya maisha bora zaidi! Lakini, changamoto hizi, zisiwafanye vijana wa kizazi kipya kuamua kufanya maamuzi magumu kwa kuamua kukimbilia ughaibuni kama wakimbizi na wahamiaji!

Bado kuna fursa ya kuligeuza Bara la Afrika kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Huko ughaibuni, vijana wanateseka sana. Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linakaza kusema, kuna haja ya kushikamana ili kupambana kwa dhati kabisa na mambo yote yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Umefika wakati kwa Bara la Afrika kuvalia njuga Saratani ya rushwa na ufisadi; mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Kuna haja ya kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu Barani Afrika. Vitendo vya kigaidi vinatishia pia ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na mafungamano ya kijamii Barani Afrika.

Maaskofu Afrika
25 May 2019, 13:45