Masista wa MSOLA katika kipindi cha Miaka 150 wamekuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji na utamadunisho Barani Afrika. Masista wa MSOLA katika kipindi cha Miaka 150 wamekuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji na utamadunisho Barani Afrika. 

Masista wa MSOLA: Mchakato wa Uinjilishaji Barani Afrika!

MSOLA ni Shirika lililoanzishwa Barani Afrika ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na uwepo wake kati ya Waafrika popote walipo. Kutokana na asili ya Shirika hili huko nchini Algeria, watawa wanabeba dhamana ya umisionari na majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Bara la Afrika.

Na Sr. Juliana Kalomba & Sr. Angela Kapitingana, MSOLA, - Roma.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amekutana na kuzungumza na Shirikisho la Mama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawataka watawa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na uaminifu kwa karama za waanzilishi wa Mashirika yao! Watawa katika maisha na utume wao, wawe ni wapanzi wa Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa katika maisha kutokana na sababu mbali mbali. Shirika la Masista Wamisionari wa Mama Yetu wa Afrika, wanaadhimisha uaminifu wa  Mungu wa miaka mia moja hamsini tangu Shirika  lianzishwe. Hawa ni watawa wanaojulikana na wengi kama “White Sisters”.

Utangulizi: Masista Wamisionari wa Mama Yetu wa Afrika ni tunda la zawadi aliyoipokea Kardinali Charles Lavigerie mnamo   mwaka 1869. Kardinali Charles Lavigerie akiwa Algeria, Afrika Kaskazini alikutwa na changamoto ya watoto yatima wengi kutokana na kipindupindu. Swali la msingi lilikuwa “ni nani atayewatunza”? Licha ya kwamba alikwisha anzisha Shirika la Mapadre, kwa haraka sana aligundua kuwa Uinjilishaji wao bila msaada wa watawa wa kike hauwezi kufanikiwa. Hili lilimfanya aandike karama na mwongozo wa Shirika la kitawa la kike hata kabla hajapata wasicaha wa kuishi lengo lake. Tarehe 8 Septemba 1869 waliwasili mabinti nane toka Britany nchini Ufaransa na ndipo MSOLA walizaliwa wakihimizwa kuwa Mitume waliotayari kujitoa kwa ajili ya wengine kwa moyo na sadaka ya umisionari katika Kristo Yesu.Kutoka Algeria, Shirika lilienea katika sehemu mbalimbali za Afrika, Tanzania ikiwemo nchi ambayo MSOLA walifika mwaka 1894 na kujituma sana katika mchakato wa uinjilishaji wa kina, ili kuendeleza upendo wa Kristo.

Karama: Jina la Masista Wamisionari wa Bikira Maria Mama Yetu wa Afrika linaeleza kwa kifupi karama yake katika Kanisa. Shirika limeanzishwa katika Bara la Afrika kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na uwepo wake kati ya Waafrika popote walipo Barani Afrika na duniani katika ujumla wake. Kutokana na asili ya Shirika hili huko nchini Algeria, watawa wanabeba dhamana ya umisionari na wajibu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Bara la Afrika. Masista Wamisionari wa Mama Yetu wa Afrika huishi katika Jumuiya za Kimataifa zenye mila na desturi mbalimbali. Moja ya kipengele cha karama ni kuwa na uthubutu wa kuanzisha mchakato wa uinjilishaji kwa kusoma alama za nyakati na mazingira ya watu wanaowahudumia. Kardinali Lavigerie, alihimiza sana kuwa “Wamisionari dhidi ya yote watakuwa wanzilishi lakini utume wa kudumu itafanywa na Waafrika wenyewe watapokuwa wamekwisha kuwa Wakristo na Mitume”.

Kwa mantiki hii Shirika limeweza kuanzisha mashirika ya kitawa ya kike yapatayo 21 Barani Afrika. Na nchini Tanzania, Shirika lilikuwa kati ya waasisi wa kwanza kushiriki kuanzisha shule, hospitali, vyuo vya ualimu, maarifa ya nyumbani na shughuli za maendeleo fungamani kwa ajili ya kuwaletea wanawake ukomnbozi. Kardinali Lavigerie pia alijikita sana katika kukomesha biashara ya utumwa na aliwahimiza watawa kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu kwani sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maeneo ya Utume wetu: Masista Wamisionari wa Mama yetu wa Afrika wapo katika nchi 15 za Bara la Afrika na Ulaya. Afrika Mashariki, wanafanya utume katika Majimbo Makuu ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza nchini Tanzania. Nyumba yetu ya malezi ipo katika Parokia ya Loruvani, Jimbo kuu la Arusha. Mpaka sasa kuna watawa saba wazalendo kutoka Tanzania wakiwa wanafanya utume wao nchini: Italia, Ghana, Malawi, Burkina-Faso, Poland na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo.

Utume wa MSOLA katika Ulimwengu Mamboleo! Masista Wamisionari wa Mama Yetu wa Afrika wanaishi na kujikita sana katika shughuli mbalimbali, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati. Kwa wakati huu wanaendelea kujikita zaidi katika huduma miongoni mwa wakimbizi, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarihi; pamoja na huduma kwa watu wasio na makazi maalumu. Wanaendelea kupambana na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; wanakazia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Wamekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam pamoja na dini za Asili Barani Afrika.

Utume huu unatekelezwa kwa kupitia vitengo vya elimu, afya, na kazi za ustawi wa jamii. Mungu ni mwaminifu na wana MSOLA wanamushukuru Mungu kwa kuwaongoza na kulinda karama ya shirika kwa miaka mia moja na hamsini. Ni Neno jema Kumshukuru Bwana. Kwa hakika “Mungu ni mwaminifu, yeye aliyetuita kuishi katika ushirikiano na mwanaye Yesu Kristo, bwana wetu” (1Wakorintho1:9). Kwa wale wasichana wanaotaka kuthubutu kujisadaka kwa ajili ya Mungu na huduma kwa jirani zao, wanakaribishwa kwa mikono miwili. Ikumbukwe kwamba, Masista wa MSOLA wamekuwa ni waasisi wa Mashirika 21 ya kitawa Barani Afrika. Nchini Tanzania wameanzisha Mashirika 4 ya kitawa. Haya ni: Shirika la Masista wa Malkia wa Mitume, Jimbo Kuu la Mbeya, Mabinti wa Maria, Malkia wa Afrika, Jimbo Katoliki la Sumbawanga pamoja na Masista wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Jimbo Katoliki la Bukoba.

Msola 2019

 

13 May 2019, 10:07