Tafuta

Vatican News
Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili III ya Kipindi cha Pasaka: Uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani; Ukulu wa Mtume Petro, Ekaristi takatifu katika maisha na utume wa kanisa! Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili III ya Kipindi cha Pasaka: Uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani; Ukulu wa Mtume Petro, Ekaristi takatifu katika maisha na utume wa kanisa!  (ANSA)

Liturujia Neno la Mungu: Jumapili ya III ya Pasaka: Petro Mtume!

Liturujia ya Neno la Mungu inakazia dhamana ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Chimbuko na muundo wa Kanisa unaosimikwa katika msingi wa Mitume. Kanisa linajengwa kwa njia ya Fumbo la Ekaristi, uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake! Madhulumu na mateso ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

 

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari masomo ya dominika ya 3 ya Pasaka mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu inakazia dhamana ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyetesa, akafa na kufufuka kwa wafu! Chimbuko na muundo wa Kanisa unaosimikwa katika msingi wa Mitume. Kanisa linajengwa kwa njia ya Fumbo la Ekaristi, uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake!

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mdo. 5:27b-32, 43-52) ni kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume. Tupo katika jumuiya changa ya Kikristo, jumuiya ambayo imejijenga juu ya nguvu ya ufufuko wa Kristo na ambayo kwa bidii zote inatangaza na kushuhudia kuwa Kristo amefufuka, Kristo yule ambaye wayahudi walimuua kwa kumtundika msalabani sasa amefufuka. Kwa mahubiri na ushuhuda huu mitume wanaingia katika mgogoro na Baraza la wayahudi. Katika somo hili la leo Baraza linawaita na kuwakanya wasiendelee kufundisha kwa jina la Kristo kwa sababu kwa kufanya hivyo wanalitangazia Baraza hatia ya kumuua Yesu.

Kuhani Mkuu anawaambia “msifundishe kwa jina hili…mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu?” Na kwa kweli hawawezi kukwepa ukweli huo kwa sababu ni Baraza hilo hilo lililopeleka mashtaka dhidi ya Yesu na kuhimiza auwawe. Petro , kwa jina la mitume na la jumuiya nzima anawaambia “imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu”. Anachokitangaza Petro ni kwamba mitume hawawezi kuacha kutekeleza wajibu wao wa kitume kwa ajili ya kulinda heshima au matakwa ya watawala hasa katika mazingira ambayo matakwa hayo yanamaanisha kuunyamazisha utume wenyewe. Katika somo hili, yanaanza kuonekana wazi mamlaka ya Petro kama kiongozi wa wa jumuiya ya waamini na hivi kiongozi wa Kanisa na kiongozi wa urika wa mitume. Mitume wanapohojiwa, ni Petro anayesimama kwa jina lao na la Kanisa kujibu. Sauti anayoitoa inakuwa ndiyo sauti ya mitume wote na sauti ya kanisa zima.

Somo la pili (Ufu 5:11-14 ) ni kutoka kitabu cha Ufunuo. Ni sehemu ya maono ya Yohane kuhusu kiti cha enzi cha Mungu na liturujia ya mbinguni. Anaona na kusikia sauti ya malaika ikiungana na ile ya wanaotajwa kuwa ni wenye uhai na sauti ya wazee, yaani makundi mbalimbali ya watu. Hawa wote idadi yao  ni elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, kumaanisha kuwa ni idadi kubwa isiyoweza kuhesabika. Wote wakimwimbia utenzi mwanakondoo aliyechinjwa. Ni nani huyu mwanakondoo aliyechinjwa? Katika kitabu hiki cha Ufunuo, mwanakondoo ni alama ya Kristo. Ni alama inayokumbushia yule mwanakondoo ambaye siku ya kukombolewa wayahudi kutoka Misri alichinjwa na damu yake kupakwa katika miimo ya milango yao.

Ni alama ambayo pia inakumbushia yule mtumishi wa Bwana anayemzungumzia Nabii Isaya, mtumishi ambaye alipelekwa kujitoa sadaka kama mwanakondoo anayepelekwa machinjioni (Is 53:7) na zaidi sana yule mwanakondoo aliyetambulishwa na Yohane Mbatizaji kuwa ndiye aondoaye dhambi ya ulimwengu ( Yn 1, 29.36). Hapa Yohane analiona kanisa lililokombolewa na mwanakondoo. Na sasa linamwimbia utenzi mwanakondoo kwa ukombozi aliowaletea. Anaona pia kuwa utenzi huu wa ushindi unaoanza kuimbwa na kanisa lililokombolewa unaimbwa pia na kila kiumbe kilichoko mbinguni. Ukombozi na ushindi wa mwanakondoo unakuwa ni furaha kwa viumbe vya duniani vilivyokombolewa na hata viumbe vya mbinguni.

Maono haya ya Yohane yana kitu kingine cha ziada. Picha hii ambapo makundi mbalimbali ya watu katika idadi kubwa yanatamka kwa sauti utenzi wa sifa, ilikuwa ni mojawapo ya heshima aliyokuwa anapewa Kaizari, mkuu wa dola ya kirumi. Yohana katika maono yake anasema anayestahili heshima hiyo ni mwanakondoo aliyeshinda. Jumuiya ya kikristo na kanisa kwa ujumla linaanza kujitambulisha kama taasisi maalumu na ya pekee isiyojihusisha na ibada za watawala wa wakati huo isipokuwa kwa Mungu pekee.

Injili (Yoh. 21:1-19) Katika injili ya leo, Yesu Kristo Mfufuka anawatokea Mitume kando ya bahari ya Tiberia na anajidhihirisha kwao katika muujiza wa uvuvi wa samaki wengi. Na hii inakuwa ni mara ya tatu Kristo Mfufuka kuwatokea Mitume wake. Injili hii inaleta muhtasari wa mapokeo ya jumuiya ya mwinjili Yohane, mapokeo ambayo yanaelezea chimbuko la muundo wa Kanisa na utume wake ambao umejisimika juu ya Kristo Mfufuka. La kwanza ni ukhalifa wa Mtume Petro. Ni Petro anayetoa wazo la kwenda kuvua samaki na mitume wengine aliokuwa nao wanafuata. Uvuvi ambao unafanikiwa tu pale Mitume wanaposikiliza na kufuata maelekezo ya Yesu mwenyewe. Tendo lenyewe la kuvua samaki ni alama ya kazi nzima ya uinjilishaji na wongofu wa wa mataifa yote. Na namba 153 ya samaki waliowapata ina tafsiri nyingi lakini zote zinaoenesha mataifa yote ya wana wa Mungu wanaohitaji kuokolewa.

Ukhalifa wa Petro anauthibitisha Yesu mwenyewe anapomwambia mara tatu, chunga kondoo wangu. Alama ya pili ni Ekaristi Takatifu. Jumuiya ya mwinjili Yohane na Kanisa zima kwa ujumla ni jumuiya inayojijenga katika adhimisho la kila juma la Ekaristi. Hapa Ekaristi inaoneshwa kwa alama ya mkate na samaki ambavyo ni Yesu mwenyewe alivitoa na kuwaita wanafunzi wake kufungua kinywa. Mapokeo yanasisitiza na kuendeleza tendo hilo hilo kwa adhimisho la kila wiki la Ekaristi. Alama ya tatu ni mateso au madhulumu ya Kanisa na watumishi wake.

Yesu anamwambia Petro kuwa alipokuwa kijana aliweza kujifunga mkanda na kwenda alipotaka lakini wakati utafika atakapokuwa mzee, mtu mwingine atamfunga mkanda na kumpeleka asikotaka yeye. Jumuiya ya Mwinjili Yohane ambayo katika kipindi hicho ilikuwa inapitia wakati mgumu wa migogoro dhidi ya dola ya kirumi iliyaona mateso yao hayo kama kitu kilichotabiriwa na Kristo mwenyewe. Kwa njia ya Petro, kanisa zima linatabiriwa kuteseka, lenyewe, watumishi wake na waamini wake. Ni utabiri huu uliowapa daima nguvu na tumaini hai bila kukata tamaa katika mateso na madhulumu mengi ya wakati wao.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika dominika hii ya tatu ya Pasaka tunapoendelea kumshangilia na kumshuhudia Kristo Mfufuka, tunaalikwa kutafakari juu ya utambulisho wetu kama Kanisa. Sisi ni jumuiya ya watu waliokombolewa kwa damu ya mwanakondoo, yaani Yesu Kristo Bwana wetu kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Kumbe tunaye Kristo kama msingi wa utambulisho wetu. Kwa sababu hiyo utume wa Kanisa ni kumhubiri na kumshuhudia Kristo. Huku ndiko kutangaza na kushuhudia Habari Njema, Habari ambayo inapaswa kuwafikia watu wote na katika hali zao zote za maisha. Tunatafakari pia utambulisho wetu kama Kanisa katika mshikamano na uongozi aliousimika Kristo mwenyewe, yaani uhalifa wa mtume Petro unaoonekana katika uongozi na utumishi wa Baba Mtakatifu. Utii kwa mamlaka ya kitume ya Baba Mtakatifu ni sehemu msingi ya utambulisho wetu kama Kanisa.

Mwisho tunaalikwa kuutafakari utambulisho wetu katika mahusiano na katika utendaji kazi wa Kanisa na mamlaka ya watawala wa kidunia. Jibu la Petro kwa baraza la kiyahudi kuwa imetupasa kumtii Mungu kuliko kuwatii wanadamu linatualika kuulinda utume wa Kanisa usichafuliwe na matakwa ya kisiasa ya watawala wa kidunia.

Liturujia J3 Pasaka
04 May 2019, 08:10