Liturujia ya Neno la Mungu: Jumapili IV Kipindi cha Pasaka: Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani Liturujia ya Neno la Mungu: Jumapili IV Kipindi cha Pasaka: Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani 

Jumapili ya Yesu Mchungaji Mwema, Siku 56 Miito Duniani 2019

Leo tunatafakari masomo ya dominika ya 4 ya Pasaka mwaka C wa Kanisa, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema. Ni Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu.” Vijana wanapaswa kuthubutu kuacha yote ili kuweza kushiriki katika mradi mkubwa wa Mungu katika huduma kwa Mungu na jirani zao!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari masomo ya dominika ya 4 ya Pasaka mwaka C wa Kanisa, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema. Ni Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu.” Vijana wanapaswa kuthubutu kuacha yote ili kuweza kushiriki katika mradi mkubwa wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Vijana wathubutu kusadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao, kwani inalipa sana!

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mdo. 13:14, 43-52) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Katika somo hili, Paulo yupo katika safari yake ya kwanza ya kitume, safari inayomfikisha mahala panapoitwa Antiokia ya Pisidia. Kazi yake ya kitume inakuwa ni ya mafanikio na watu wengi wanamwongokea Kristo. Hata hivyo mafanikio haya yanaharibiwa na baadhi ya Wayahudi. Hawa wanaanza kuyapinga na kuyapotosha mafundisho ya Paulo na wanaishawishi jamii nzima kuachana na mafundisho hayo. Ndipo Paulo anawaambia “ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza, lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni twawageukia mataifa”.

Hapo Paulo anaanza kujikita kiutume kwa watu wa mataifa - watu wasio wayahudi, nao wanalipokea Neno na kuliamini. Somo hili, katika hatua ya mwanzo, linatueleza mojawapo ya sababu ya injili kuwafikia watu wa mataifa. Na sababu hii ni kuwa Wayahudi hawakuwa tayari kuipokea. Zaidi ya hayo, pasipo kuonesha utofauti wa kitaifa au wa kikabila kati ya wayahudi na watu wa mataifa mengine, somo hili linaonesha utofauti wa utayari wa kupokea neno la Mungu iwe ni kwa wayahudi au  kwa watu wa mataifa. Wote wanaitwa kuiitikia injili.

Somo la pili (Ufu 7:9. 14-17 ) ni kutoka kitabu cha Ufunuo na linahusu maono ya wateule wa Mungu. Wateule hawa ni wengi mno wa idadi isiyohesabika na ni wa kila taifa, kabila na lugha. Watu wote bila kujali utaifa, ukabila wala lugha wana nafasi sawa mbele ya mpango wa wokovu wa Mungu. Nao wamevishwa mavazi meupe  na wana matwi ya mitende mikononi mwao. Matawi ya mitende ni alama ya ushindi. Kwa wayahudi huwakumbusha namna walivyosherehekea sikukuu ya vibanda na namna walivyomkaribisha Yesu alipokuwa akiingia Yerusalemu. Mavazi meupe ni ishara ya utakaso, ishara ya usafi wa maisha.

Wamefikia utakaso huo na kuishiriki furaha ya ushindi kutoka katika “dhiki ile iliyo kuu”. Kristo mwenyewe alikwisha tabiri kuwa siku za mwisho zitakuwa ni siku za dhiki na taabu kubwa. Katika Mk 13:19 anasema siku hizo zitakuwa na dhiki ambayo haijawahi kutokea tangu mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu. Maono haya yanapowataja wateule waliotoka katika dhiki hii ni maono yanayolenga kuwaimarisha watu wasiiogope dhiki ya siku za mwisho na zaidi ya hapo maono haya yanalenga kuwaimarisha waikabili vema wakijua kuwa baada ya dhiki hiyo kuna utakaso na furaha ya ushindi.

Maono yanaongeza kuwa mavazi hayo meupe ni mavazi yaliyooshwa katika damu ya mwanakondoo. Katika kitabu cha Ufunuo, mwanakondoo ni alama ya Kristo na damu ni alama inayoomanisha maisha na hapo hapo humaanisha pia kifo. Damu ya mwanakondoo ni maisha na kifo cha Kristo, ni Kristo katika ujumla wake. Kumbe wateule hawa wameupata utakaso na ushindi kwa nguvu ya damu ya Kristo na kwa gharama ya damu ya Kristo. Ni Kristo aliyewapa ushindi. Kanisa limeona pia katika damu iliyotoka ubavuni mwa Kristo alama ya sakramenti ambazo Kristo ameliachia.

Mojawapo ya Sakramenti hizo ipo sakramenti inayomtakasa mwanadamu kutoka uchafu wowote wa dhambi na kuifanya roho yake kuwa nyeupe. Hii ni sakramenti ya kitubio. Ni hapa tunapoona pia maono haya kuwa ni maono yanayoongelea mapambano na ushindi wa mwanadamu katika kila hatua ya maisha yake. Ni sakramenti ya kitubio inayompatia mwanadamu ushindi dhidi ya mapambano yake ya kila siku dhidi ya dhambi.

Injili (Yoh. 10:27-30) Injili ya leo ni kutoka sura ya 10 ya injili kadiri ya mwinjili Yohane. Katika sura hii ya 10 Kristo anajitambulisha kuwa ndiye mchungaji mwema. Katika sehemu ya sura hii ambayo ndiyo injili ya leo, Kristo anaeleza uhusiano alilonao na kondoo wake, yaani wafuasi wake na uhusiano alionao na Baba yake. Anasema kondoo wake huisikia sauti yake naye anawajua nao humfuata. Ni uhusiano unaohusisha jitihada za wote wawili, Kristo na mfuasi. Jitihada ya mfuasi ni kumsikiliza Kristo na kumfuata, ndiyo kuishikilia imani na kuambatana nayo katika maisha yake. Kwa mfuasi huyu anayemsikiliza na kumfuata Kristo huingia naye katika mahusiano ya ndani na ya pekee, mahusiano ya kumjua.

Kumjua huku si kule kwa juu juu bali ni kumjua katika undani wake hasa, kumjua kunakolenga kuiinua hali yake na kuuinua ubinadamu wake mzima. Matokeo ya uhusiano huu kati ya Yesu  na mfuasi humpa mfuasi uzima wa milele kwani katika safari ya maisha yake mfuasi huyu hatapotea. Kristo anaeleza pia uhusiano wake na Baba kuwa ni uhusiano wa umoja. Yeye na Baba ni wamoja. Injili ya leo inauelezea upendo wa Kristo mchungaji mwema. Huu ni upendo unaoingia katika maisha ya mfuasi, upendo unaoanzisha mahusiano binafsi na mfuasi na upendo unaomuokoa mfuasi kwa kumuingiza katika uzima wa kimungu ulio uzima wa milele.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii ya nne ya Pasaka ni dominika ambayo pia inafahamika kama dominika ya Mchungaji Mwema na siku 56 ya Kuombea Miito Mitakatifu Duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa siku hii ya kuombea miito anawaalika waamini wote na kwa namna ya pekee vijana kuwa na ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu. Anawakumbusha kuwa mwito wa Mwenyezi Mungu kamwe hauingilii uhuru binafsi wa mwanadamu unaompa mzigo usiobebeka bali wito ni hatua yake ya mapendo ambayo kwayo anamshirikisha mwanadamu na kumwalika kuingia katika mpango wake mkubwa wa wokovu wa wanadamu.

Anaongeza kuwa kila mmoja anaitwa kwa namna yake na kwamba katika kuufuata wito inapasa kutokubaki katika ulimwengu wa ndoto na matarajio hewa na kusisitiza kuwa hawapaswi kuwa viziwi kwa mwito wa Mungu na tena wasiogope kuyaachilia maisha yao kuwa “wavuvi wa watu” wakijitolea nafsi zao ndani ya kanisa kwa ajili ya huduma aminifu kwa injili na kuwatumikia watu. Katika dominika hii ya miito tuliombee Kanisa liendelee kuiakisi sura ya Kristo mchungaji mwema na kwa njia ya watumishi wake liendelee kuwa alama hai ya ule upendo wa Kristo unaookoa.

Siku ya Kuombea Miito 2019
10 May 2019, 16:16