Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VI ya Pasaka: Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, Roho Mtakatifu na Zawadi ya amani inayowajibisha! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VI ya Pasaka: Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, Roho Mtakatifu na Zawadi ya amani inayowajibisha! 

Jumapili VI ya Pasaka: Dhana ya Sinodi; Roho Mtakatifu & Amani!

Wosia wa Yesu: Jambo la kwanza ni upendo, la pili ni zawadi ya Roho Mtakatifu na la tatu ni amani. Leo anakazia kuonesha uhusiano uliopo kati ya upendo na kulishika Neno la Mungu. Dira, misingi na mwongozo wa upendo ndilo Neno la Mungu na Yohane anafundisha kwamba, Mungu ni upendo. Upendo uliojijenga juu ya Neno la Mungu ni upendo unaomuunganisha mtu na Mungu.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari masomo ya dominika ya 6 ya Pasaka mwaka C wa Kanisa. Wosia wa Yesu katika Injili ya dominika hii ni katika mambo matatu. Jambo la kwanza ni upendo, la pili ni zawadi ya Roho Mtakatifu na la tatu ni amani. Kwa mara ya kwanza katika historia, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inaanza kujitokeza!

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mdo. 15:1-2, 22-29) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Kanisa la mwanzo linazidi kukua na kusambaa nje ya mipaka ya uyahudi. Linavyozidi kusambaa hivyo, linatokea tatizo. Hili ni kanisa lililozaliwa katika mazingira ya kiyahudi. Waamini wa mwanzo walikuwa ni wayahudi na walikuwa na tamaduni zao za kiyahudi na desturi ambazo wote walizishika. Sasa nje ya mipaka ya Uyahudi, Je wasio wayahudi wanapaswa kwanza kushika tamaduni za kiyahudi ili wawe wakristo kamili au wanaweza kuwa wakristo bila kushika tamaduni za kiyahudi? Unakua mvutano mkubwa unataka kupelekea kuligawa Kanisa.

 

Somo letu la kwanza leo linahusu mvutano huu na linatuonesha namna ambavyo Kanisa hilo la mwanzo liliutatua. Baada ya kushindwa kufikia uamuzi, Paulo, Barnaba na wawakilishi wa jumuiya wanaenda Yerusalem kwa mitume kulizungumzia suala hilo na kutafuta ufumbuzi katika umoja wa urika wa mitume chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Hii ndiyo ilikuwa Sinodi ya kwanza. Matokeo yake ni kuwa Mitume waliona kuwa wasio wayahudi kulazimika kushika kwanza tamaduni za kiyahudi ndipo wawe wakristo kamili ni kuwatwisha mzigo usio wa lazima. Waliweka tofauti kati ya yale mambo yanayowabana wayahudi pekee na yale yanayowabana watu wote. Hivyo wakajikita katika yale yanayowabana watu wote, yale aliyokuwa ameagiza Mwenyewzi Mungu hata kabla ya kumwita Abrahamu: kujiepusha na vitu vilivyotolewa sadaka ya sanamu na ya damu yaani ushirikina; wajiepushe na nyama zilizosongolewa na kujiepusha na kila aina ya uasherati.

Somo la pili (Ufu 21:10-14, 22-23 ) ni kutoka kitabu cha Ufunuo.  Ni mwendelezo wa maono ya Yohana, maono ambayo katika somo la dominika hii yanatufikisha Yerusalemu mpya, mahala wanapoelekea watu wote. Yerusalemu anayoiona ni mji unaoshuka kutoka mbinguni, sio mji uliojengwa na wanadamu kama miji mingine. Wenyewe ni zawadi kutoka juu. Umezungukwa na utukufu wa Mungu maana yake uko karibu kabisa na Mungu, upo ndani ya eneo la utukufu wa Mungu na ni kwa sababu hii unakuwa na thamani kubwa kama ya kito au madini yenye thamani nyingi.

Yohane anaona pia kuwa katika mji huu vipimo vyake, milango ya kuuingia, idadi ya majina yaliyoandikwa na misingi ya ukuta wa mji vyote vina namba kumi na mbili. Ni namba inayowakilisha makabila 12 ya Israeli na pia idadi ya mitume 12 wa Yesu. Hapa Yohane anaona ukaribu wa pekee uliopo kati ya mji huu na taifa la Isreeli na kati ya mji huu na mitume. Ni kuanza na taifa la Israeli Mwenyezi Mungu ameamua kuwakomboa na  kuwakusanya watu kwake kwa njia ya Kanisa ambalo mitume ndio msingi wake. Mwisho wa maono haya, Yohane haoni hekalu.

Katika Yerusalemu mpya hekalu halipo kwa sababu Mungu Mwenyewe yupo na  kinapokuwapo kitu halisi basi kile ambacho ni alama tu hakina nafasi. Lakini tunapoliangalia hekalu kama kitovu cha ibada za Agano la Kale, ibada ambazo hazina nafasi katika Agano Jipya, maono haya yanaashiria hatima ya hekalu. Yanaonesha mwisho wa muundo wa ibada za kale zilizokuwa ni alama tu na mwanzo wa Ibada za Agano Jipya ambazo ni uwepo halisi  wa Kristo ambaye kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake zinaadhimishwa ibada za mafumbo ya wokovu alioupatia ulimwengu.

Injili (Yoh. 14:23-39) Injili ya dominika hii, kadiri ya mwinjili Yohane ni sehemu ya maneno ya mwishomwisho ya Yesu na wanafunzi wake kabla ya kuingia katika mateso. Yesu anawaandaa wanafunzi wake katika kuanza maisha mapya wao peke yao kwa maana ya kwamba muda si mrefu ujao hatakuwa nao tena kama alivyokuwa nao hapa duniani. Ni kama anawapa wosia, na wosia wa Yesu katika Injili ya dominika hii ni katika mambo matatu. Jambo la kwanza ni Upendo, la pili ni Zawadi ya Roho Mtakatifu na la tatu ni Amani.

Alikwishawafundisha kirefu sana juu ya upendo na tena akawapa kama amri mpya. Leo anakazia kuonesha uhusiano uliopo kati ya upendo na kulishika Neno la Mungu. Upendo sio tu kufuata vionjo binafsi bali upendo unahitaji kuongozwa, unahitaji kupewa dira na kuwekewa misingi. Dira, misingi na mwongozo wa upendo ndilo Neno la Mungu. Anayependa hushika Neno la Mungu kwa kuwa, kama anavyofundisha Yohane, Mungu ni upendo. Upendo uliojijenga juu ya Neno la Mungu ni upendo unaomuunganisha mtu na Mungu.

Pili Yesu anapoondoka anawaambia wanafunzi wake wasifadhaike na wasiwe na woga kwa sababu atawaletea Roho Mtakatifu atakayekuwa kwao Msaidizi. Atawafundisha na kuwakumbusha yote. Maisha waliyoishi mitume pamoja na Kristo na uwepo wa Kristo katika maisha ya muumini ndio wokovu wenyewe. Roho Mtakatifu kuwakumbusha ni kuweka hai daima, sio kumbukumbu tu, bali uwepo wa Kristo katika maisha yao.  Mwisho anawaachia amani, amani yake ambayo si kama ile amani ya kiulimwengu bali ile amani ya kweli iliyotangazwa na malaika pale alipozaliwa – “utukufu kwa Mungu juu na Amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema”.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii yamegusia mambo ya msingi katika maisha ya jumuiya na katika upya wa maisha ya mwamini ndani ya Kristo Mfufuka. Katika mgogoro uliolikumba Kanisa la mwanzo tunaziona pia jumuiya zetu katika migogoro mbalimbali iwe mikubwa au midogo. Tunaziona pia familia zetu ndani ya migogoro mbalimbali. Tunaalikwa leo kutambua nguvu ya mazungumzano na mijadala ya pamoja katika utatuzi wa migogoro ndani ya familia, ndani ya jumiuya na kanisa kwa ujumla. Na tena katika mazungumzano hayo tunaoneshwa nafasi ya pekee waliyonayo wazee. Ndani ya Kanisa tunayo hierakia ambayo kwa msaada wa Roho Mtakatifu hulinda na kudhihirisha umoja wa Kanisa. Tujibidiishe kuiheshimu kama kuheshimu makusudio ya Mungu mwenyewe kwa Kanisa lake.

Masomo ya leo yanatualika pia kujikinga dhidi ya kutengeneza madaraja au matabaka katika jumuiya zetu na hasa ndani ya Kanisa. Tunaalikwa kuulinda ukristo usihodhiwe na ukabila au ueneo bali uongozwe daima na misingi aliyoiweka Kristo mwenyewe. Tuzilinde taasisi za Kanisa, tuilinde mifumo ya Kanisa tangu upokeaji wa miito, huduma na utumishi ili ziendelee kuudhihirisha ukatoliki. Mwisho tunaalikwa kuendelea kujisimika katika upendo, kujenga amani na kuutambua uwepo wa  Roho Mtakatifu ambaye Kristo anamtuma ndani yetu ili kutuimarisha, kutufundisha na kuweka hai uwepo wa Kristo katika maisha yetu.

Kiturujia 6 Pasaka

 

24 May 2019, 15:09