Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Waamini wanatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, hadi miisho ya dunia! Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Waamini wanatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, hadi miisho ya dunia! 

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni

Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho. Kwa muda wa siku 40, Yesu Mfufuka aliwatokea wafuasi wake, akala na kunywa nao; akawafundisha juu ya Ufalme wa Mungu na utukufu wake uliokuwa bado umefunikwa na alama za kibinadamu! Leo , Amepaa mbinguni!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. - Dodoma.

Sherehe ya Kupaa Bwana mbinguni ni sherehe ambayo sote tunaitwa kutambua kuwa yule Kristo Yesu tunaye mwamini amepaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba, ametukuzwa na ana mamlaka yote na atakuja tena na ukuu na enzi kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Katika tendo hili la kupaa, Yesu alitoa tamko la utume - tena wafanye kwa uaminifu mpaka atakapokuja. Aliwahakikishia neema ya Mungu katika utumishi wao. (Mdo 1,8 -Mt 28,19-20 -Mk 16,15-18). Ushuhuda katika kueneza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia katika mataifa yote. Huu ndio ujumbe tena unaowekwa mbele yetu tunaposherehekea sikukuu ya kupaa Bwana. Ujumbe huo ni wa Bwana, ndiyo maana atuahidia Roho Mtakatifu. Peke yetu tutashindwa.

Kristo Yesu, amepaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Nasi tumekabidhiwa jukumu la kuendeleza utume  huu na kutangaza ufalme wa Mungu kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Leo tunaadhimisha sherehe ya kanisa, siku 40 baada ya sherehe ya Pasaka - kupaa mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo. Mhubiri mmoja asema hakuna awezaye kukaa peke yake mwanamke/mwanamme – kila mmoja anamhitaji mwingine, mwalimu ahitaji wanafunzi n.k. Hivi pia kwa mkristo, leo hii yupo Roho Mtakatifu na akiwepo utamu wa maisha ya kikristo huongezeka. Katika Mt. 1:23 tunaambiwa kuwa Mungu yu pamoja nasi. Leo tunasikia tamko hilo la Yesu.

Leo Yesu asema nipo pamoja nanyi. Ikumbukwe kuwa siku kuu ya kupaa siyo kumbukumbu ya Kristo kuondoka kati yetu bali ni adhimisho la kumbukumbu ya uwepo wa Kristo kati yetu. Kivipi? Uwepo huu unaoneshwa na kazi zifanywazo na watu wa Mungu - wale ambao daima wanamtii Roho mtakatifu. Tunaposoma habari ya Kupaa Bwana - katika Yoh. 3:13 tunaona kuwa, wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani Mwana wa Adamu. Katika Efe. 4:10 tunasoma, naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote ili avijaze vitu vyote. Katika Ebr. 4:14 tunasoma kuwa, basi iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia mbinguni Yesu, Mwana wa Mungu, tuyashike tena maungamo yetu.

Padre Raniero Cantalamesa anasema mbingu ikieleweka kama mahali pa pumziko, pa utimilifu wa milele ilifanyika mara tu alipofufuka na kupaa. Mbingu yetu ya kweli ni Kristo mfufuka tunayetumaini kukutana naye na pamoja naye tutakuwa mwili mmoja naye baada ya ufufuko wetu. Na tukisoma habari ya ufufuko na kupaa – katika Yoh. 20:17 tunaona kuwa, Yesu akamwambia (Mariamu) usinishike kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba, lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie ninapaa kwenda kwa Baba yangu, naye ni baba yenu, kwa Mungu wangu, naye ni Mungu wenu. Na  katika Lk. 24:51 tunsoma kuwa, ikawa katika kuwabariki alijitenga nao akachukuliwa juu mbinguni.

Kadiri ya Wainjili Mathayo na Marko -  Yesu alipaa mbinguni mwili na roho na tena hilo limetokea siku ile ile ya ufufuko wake, mara moja na hivyo tu. Katika Luka na Matendo – Yesu alipaa mbinguni pale Yerusalemu na hii ilifanyika siku 40 baada ya ufufuko na muda huo amewatokea mitume mara kadhaa. Lakini lengo la waandishi siyo uhakika katika mandishi bali katika ujumbe wa tukio hilo kuu. Adhimisho la sikuku hii ya leo laonesha tu mwisho wa muda/wakati ambao Yesu bado alihusiana kwa macho na wanafunzi wake. Tunachoambiwa ni kuwa atakuja tena siku ya mwisho – Yoh. 21:22 - Yesu akamwambia ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi?

Hakika masomo yetu ya leo, liturujia yetu ya leo yahimiza ufuasi katika ukweli, kwamba maana halisi ya maisha ya kikristo ipo katika Kristo mwenyewe. Mitume wanahimizwa wakaze mwendo na kuongoa wengi, wakibatiza na kufundisha. Nguvu yao ni Kristo na wao wenyewe. Kinachotokea ni kuwa Yesu aliye na nguvu ya Baba anatoa uwezo huo huo kwa wafuasi wake. Ufuasi ni mchakato ambao kila mwamini anaelimishwa na kuingizwa katika njia mpya, ni mchakato wa uinjilishaji. Huu ndio mwito uliotolewa na jukumu kuu walilopewa wafuasi wakati wa kupaa Bwana nao wakafanye aliyofanya Bwana, kuendeleza utume wake Bwana.

Huu ni wosia wakati wa Kupaa. Katika kupaa kwake Bwana, hupatikana nguvu kwao wote wamfuatao. Yeye atamani kubaki na watu wake ndio maana asema mimi nipo kati yenu. Hatuachi peke yetu. Yote asemayo yatuachia furaha na amani na maneno hayo bado yanabaki kati yetu. Hata leo tunahitaji uongozi wake Kristo. Siku kuu ya Kupaa Bwana ni sikukuu ambayo sote tunaitwa kutambua kuwa yule Kristo tumwaminiye amepaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba, ametukuzwa na ana mamlaka yote na atakuja tena na ukuu na enzi. Katika tendo hili la kupaa, Yesu alitoa tamko la utume - tena wafanye kwa uaminifu mpaka atakapokuja. Aliwahakikishia neema ya Mungu katika utumishi wao. (Mdo 1,8 -Mt 28,19-20 -Mk 16,15-18). Hili tamko la utume ni lipi?

Ushuhuda katika kueneza Habari Njema mpaka miisho ya dunia katika mataifa yote na kutangaza kwa kila kiumbe hii Habari Njema ya ufalme wake bila kuwa na mipaka ya utaifa au ukabila. Huu ndio ujumbe tena unaowekwa mbele yetu tunaposherehekea sikukuu ya kupaa Bwana. Ujumbe huo ni wa Bwana, ndiyo maana atuahidia Roho mtakatifu. Peke yetu tutashindwa. Sherehe hii yathibitisha ukamilifu wa upendo wa Mungu. Mungu amekamilisha utume wake hapa duniani. Ametufundisha juu ya ufalme wake, ametuaminisha sisi watu wake tuendeleze hilo jukumu, anatutuma sisi tuende sasa ulimwenguni lakini pamoja na Roho wake. Hakika ni uaminifu mkubwa. Hiyo ndiyo changamoto iliyopo mbele yetu leo – nasi tuende tukahubiri hiyo habari njema. Tumsifu Yesu Kristo.   

31 May 2019, 07:04