Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka: Kanisa linatafakari kwa kina ungamo la Mtakatifu Petro kuhusu upendo na ukuu wake kwa ajili ya Kanisa! Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka: Kanisa linatafakari kwa kina ungamo la Mtakatifu Petro kuhusu upendo na ukuu wake kwa ajili ya Kanisa! 

Jumapili ya Tatu ya Pasaka: Ungamo la Mtume Petro! Upendo!

Kwa neno hili la Yesu yaeleweka kuwa Petro anakabidhiwa rasmi mamlaka ya uongozi. Anamkabidhi uongozi wa Kanisa aliomwahidia alipomwambia ‘wewe ni mwamba na juu ya mwamba huu nitajenga Kanisa langu’ – Mt. 16:18-19. Yesu anabaki mwaminifu hata kama mwanadamu anakosa uaminifu – Mt. 26:35. Maswali matatu ya Yesu kwa Petro, yanabatilisha majibu ya kumkana Yesu!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Kardinali Heenan wa London alikuwa ameelekezwa na daktari wake kupumzika na akaamua kwenda sehemu za mashambani huko Hertfordshire. Huku akiwa bado hajafika sehemu yake mpya ya mapumziko akapokea barua toka kwa mkristo mmoja aliyekuwa amekasirishwa na baadhi ya maamuzi mbalimbali ya mabadiliko yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mkristo huyo alikuwa ameamua kuachana na Kanisa Katoliki na kwenye barua aliandika wazi kuwa anaamini barua hii haitasema cho chote kwa Kardinali kwa vile hamfahamu na pia kondoo mmoja tu kuondoka isingekuwa shida. Kumbe, Kardinali akajibu ile barua kwa upole na unyenyekevu mkubwa ‘mimi ni mchungaji na wewe ni mmoja wa kondoo wangu’. Nitarudi mara moja London ili kwa pamoja tuongee na kujadili hatima ya hali yako.

Ndugu wapendwa, baada ya kutafakarishwa na wito wa huruma ya Mungu dominika iliyopita, leo tunaalikwa kutafakari sana mahusiano yetu na Mwenyezi Mungu. Tunaona katika ibada ya huruma ya Mungu kuwa habari ya uelewa juu ya kifo na ufufuko wake Kristo umekuwa ni sababu ya imani ya watu wote – Mk. 15:39, makaburi yakafunuka – Mt. 27:52-53 na hata kwa kufa kwake sisi tumepata roho wake Mungu – Yoh. 19:30. Hivyo tendo la ufufuko wa Yesu siyo tendo la ushujaa. Baada ya ufufuko, Yesu anawatakia amani na kuwatuma waende. Katika Ebr. 3:1 tunasoma neno hili – kwa hiyo ndugu watakatifu wenye kuushiriki mwito wa mbinguni mtafakarini sana mtume na kuhani mkuu wa maungano yetu Yesu aliyetumwa kwe ulimwengu. Ufufuko wahitimisha utume wake sasa. Naye aweza kuwapeleka mitume wake, wale aliowachagua yeye ili wapate kuendeleza kazi hiyo ya upendo wa Mungu kwetu.

Pia karibu sana na roho ya ufufuko ni maneno ya Yesu, pokeeni Roho Mtakatifu. Yoh. 16:7 – lakini mimi nawaambia iliyo kweli, yawafaa ninyi mimi niondoke kwa maana mimi nisipoondoka huyo msaidizi hatakuja kwenu bali mimi nikienda zangu nitampeleka kwenu. Baadaye tunaona katika hotuba yake siku ya Pentekoste, Mtakatifu Petro anaonesha wazi kuufahamu mpango huu wa Mungu. Anaunganisha vizuri kabisa ufufuko wa Bwana na kupeleka Roho Mtakatifu. Anasema akiwa ametukuzwa na Baba, Yesu alipokea Roho aliyeahidiwa kutoka kwa Baba halafu akamtuma roho huyo kwetu – Mdo. 2:33. Hakika ni mapenzi yake Baba kuwa ametupatia ukombozi na kwa njia hii kwetu ni fumbo kuu la upendo. Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanatupenda upeo kiasi cha kujitoa kwetu.

Fumbo hili la upendo ni kwa ajili yetu. Ufufuko wa Kristo ni ufunguo wa mlango unaoruhusu ujio huu wa neema na upendo wa Mungu kwetu. Kama tukikubali maisha yake ina maana pia twakubali  upendo wake ndiyo maana ya ufufuko kwetu. Huu ndiyo upendo unaotusukuma sote na kwa namna ya pekee unamsukuma Petro kutoa maisha yake yote kwa ajili ya Bwana wake Yesu Kristo. Tukirudi katika Liturujia yetu dominika hii tunaona kuwa somo la kwanza linatanguliza tafsiri ya kile kilichopo katika somo la injili, ukamilifu wa kilichosemwa na Yesu. Somo la pili laongelea kuhusu ushindi wa mwisho, wale walio wake Mungu wanasherehekea ushindi.

Katika sehemu hii ya Injili ya leo toka Yohane twaona mara ya tatu na ya mwisho ya tokeo la Yesu kama ilivyorekodiwa naye Yohane. Somo linatuonesha kuwa Yesu hakufufuka tu kwa maana ya maneno bali hakika alifufuka kimwili pia. Ushuhuda wa mitume uko wazi - tulikula na kunywa pamoja naye baada ya ufufuko wake. Petro anasisitiza hili katika somo la kwanza. Katika Injili, Yesu anaongea na Petro na inafuata kula samaki na mitume. Halafu yanafuata maswali matatu na majibu matatu na hitimisho tatu – lisha kondoo wangu

Kwa neno hili la Yesu yaeleweka kuwa Petro anakabidhiwa rasmi mamlaka ya uongozi. Anamkabidhi uongozi wa Kanisa aliomwahidia alipomwambia ‘wewe ni mwamba na juu ya mwamba huu nitajenga kanisa langu’ – Mt. 16:18-19. Yesu anabaki mwaminifu hata kama mwanadamu anakosa uaminifu – Mt. 26:35. Maswali matatu ya Yesu kwa Petro, yanabatilisha majibu matatu ya Petro dhidi ya ufahamu wake kwa Yesu. Watu wengi husema hapa ndio Petro anapata uongofu. Wengine huita ungamo la Petro. Ungamo hili la Petro laweza kufananishwa na ungamo la yule  baba mwenye mtoto aliyepagawa na shetani katika Mk. 9:24 - hapo baba wa kijana alilia kwa sauti kubwa, Nasadiki. Saidia kutokuamini kwangu. Anachosema Petro ni kuwa ndiyo Bwana nakupenda, ongeza upendo wangu kwako.

Daima Mungu humpatia mwanadamu nafasi zaidi ya moja. Changamoto hii inampatia Petro nafasi ya kuanza upya. Tangu hapo anachukua nafasi ya Yesu katika ulimwengu. Anaondoka Galilaya na kwenda ulimwenguni kutangaza habari njema. Mwishoni anathibisha ahadi yake ya uaminifu kwa Kristo kwa kutoa maisha yake kwa Kristo. Ukuu wa Yesu wa kusamehe na kumpa mwanadamu nafasi, unampatia nafasi hata mvovu kuongoka. Mazungumzo kati ya Yesu na Petro, hubadilisha maisha ya kila mmoja wetu. Mt. Agostino akitafakari sehemu hii anasema kuwa kwa kumwuliza Petro maswali, Yesu pia atuuliza kila mmoja wetu swali lile lile – je wanipenda?

Ndugu wapendwa, ukristo siyo mkusanyiko wa Maandiko mazuri bali ni swala la ufungamano wa ndani. Ni swala la mahusiano na Kristo. Kabla ya ufufuko wake aliwafundisha watu kumwamini na kumsadiki Mungu. Tumeona pia hili dominika ya pili kwamba kiini cha ibada ya huruma kwa Mungu ni kumwamini na kumsadiki zaidi Yesu. Kabla ya hapa Yesu hakuongea kuhusu kumpenda. Swala la upendo amelisema baada ya mateso, kifo na ufufuko wake. Upendo kwa Kristo huonekana kwa kuwapenda wengine. Hana haja na faida ya upendo huo. Anachotaka yeye ni kondoo wake wafaidike. Sababu na chanzo cha upendo huo ni Mungu Baba. Mama Teresa anasema – tunda la upendo ni huduma na tunda la huduma ni amani. Yesu atualika tumpende na tukifanya hivyo tutawapenda wengine. Tumsifu Yesu Kristo.!

03 May 2019, 15:44