Tafuta

Vatican News
Roho Mtakatifu ni zawadi ya Baba kwa njia ya Mwana: Roho Mtakatifu atawafundisha na kuwakumbusha yale yote Kristo Yesu aliyoyafundisha! Roho Mtakatifu ni zawadi ya Baba kwa njia ya Mwana: Roho Mtakatifu atawafundisha na kuwakumbusha yale yote Kristo Yesu aliyoyafundisha! 

Jumapili ya VI ya Pasaka: Ahadi ya Yesu: Roho Mtakatifu: Atawafundisha na Kuwakumbusha!

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VI ya Pasaka: Hapa Kristo anakamilisha ufunuo wa Utatu Mtakatifu kwamba katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu, Mungu Baba nafsi ya kwanza ndiye muumbaji, Mungu mwana nafsi ya pili, ndiye Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu nafsi ya tatu ndiye anayeliongoza, kulisimamia, kuliimarisha na kulitakatifuza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 6 ya pasaka. Bwana wetu Yesu Kristu kabla ya kupaa kwenda mbinguni, siku alipowatokea kwa mara ya mwisho mitume wake baada ya kufufuka, aliwapatia wosia wa kupendana kama yeye alivyowapenda na kuwaahidi msaidizi ndiye Roho Mtakatifu. Katika Injili ya leo ilivyoandikwa na Yohane, Yn. 14: 23-29 Yesu anasema: Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu.Amani nawaachieni; amani yangu nawapa, msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga, nitawatumia Msaidizi, huyo ni Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

Hapa Kristo anakamilisha ufunuo wa Utatu Mtakatifu kwamba katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu, Mungu Baba nafsi ya kwanza ndiye muumbaji, Mungu mwana nafsi ya pili, ndiye Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu nafsi ya tatu ndiye anayeliongoza, kulisimamia, kuliimarisha na kulitakatifuza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki la mitume. Kanisa Katoliki ni moja maana yake Mwanzilishi ni mmoja ndiye Yesu Kristo nafsi ya pili ya utatu mtakatifu, Kiongozi wake mkuu duniani ni mmoja ndiye Baba Mtakatifu khalifa wa Mtume Petro ambaye Kristo alilijenga Kanisa juu yake na wala milango ya kuzimu haitalishinda, mafundisho yake ya kiimani, kimaadili, kilitrujia yote ni mamoja.

Alama hii ya umoja wa Kanisa inajidhihirisha wazi tangu nyakati za Mitume. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume linadhihirisha hili. Kulipotokea malumbano na majadiliano kama kuwapokea wapagani katika Kanisa ni lazima wafuate sheria, mila na desturi za kiyahudi, yaani watahiriwa kama desturi ya Musa, namna tatizo hili lilivyotatuliwa inadhihirisha umoja wa Kanisa tangu mwanzo wake wakati wa mitume. Kwanza wahusika wa tatizo walijadiliana wao wenyewe na “wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swala hilo”.

Habari ya jambo hili ilijadiliwa na Maamuzi yaliyotolewa Yerusalemu na Mitume na Wazee wakaandika hivi; Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa, kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo mtafanya vema. Wasalamu. Maamuzi yaliyotolewa na wazee na mitume Yerusalemu yaliliongoza Kanisa zima pote ulimwenguni. Ndivyo ilivyo hata sasa ambapo Makao Makuu ya Kanisa yakiwa Vatican, ikitokea shida yoyote ya kiimani au kimaadili itajadiliwa pamoja na maamuzi yanayotolewa yanaliongoza Kanisa zima. Ndiyo maana Kanisa limebaki imara hata sasa.

Roho Mtakatifu ndiye anayeliongoza kwa njia ya Baba Mtakatifu, ndiyo maana anaitwa Baba Mtakatifu kwa maana anayoyasimamia ni matakatifu naye anaongozwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu katika maamuzi ya mafundisho msingi ya kiimani na kimaadili. Kanisa ni Takatifu: Yohane katika somo la pili anasema, “Akanionyesha ule mji mtakatifu Yerusalemu”. Yerusalemu ni mfano wa Kanisa. Kanisa ni Takatifu kwasababu: Mwanzilishi wake ni Mtakatifu, Yesu Kristu, linahudumia vitakatifu, linawafanya watu kuwa watakatifu kwa njia ya Neno la Mungu na Sakramenti zake. Mafundisho yake yanaongozwa na Roho Mtakatifu ndiye anayelifundisha kupitia kwa Baba Mtakatifu khalifa wa mtume Petro.

Kanisa ni Katoliki: Tunaweza kusema Kanisa kumbakumba. Kanisa ni kwa ajili ya wokovu wa watu wote kama wimbo wa katikati unavyotuambia “Miisho yote ya Dunia itamcha yeye”, itamwabudu Mungu. Kumcha na kumwabudu Mungu kunaanzia hapa duniani na ukamilifu wake ni Mbinguni. Somo la pili la kitabu cha ufunuo linasema wazi; tunapswa kumtengenezea Mungu makao katika roho zetu. Kwa sababu “tangu sasa watu wamwabuduo Mungu, watamwabudu katika Roho na katika ukweli” (Yn 4:24). Na huko mbinguni ni roho tupu, nami sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Mungu Mwenyezi na Mwanakondoo, ndio hekalu lake.

Kanisa ni la Mitume. Imani na misingi ya mafundisho ya Kanisa Katoliki imejengwa juu ya mitume waliopokea Mafundisho na Imani hiyo moja kwa moja toka kwa Yesu Kristu. Uongozi wa Kanisa nao unafuata mtiririko huo kutoka enzi za Mitume mpaka sasa. Katika somo la pili la kitabu cha Ufunuo Yohane amesema; naliona mji mzuri, safi kama bilauri; una ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi yaliandikwa majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-kondoo akidhihirisha kuwa Kanisa alilolianzisha Yesu aliwakabidhi mitume wake, nasi tumelipokea kutoka kwa mitume.

Historia inatufundisha kuwa kuanzia karne ya 16 upinzani wa imani na mafundisho tuliyopokea toka kwa mitume ulizidi, kukatokea na kuibuka kwa madhehebu mbalimbali ya upinzani yaani waprotestanti kama jina lao lilivyo. Kimsingi chanzo chake ni kupinga mafundisho na hasa mamlaka ya Baba Mtakatifu Khalfa wa mtume Petro. Nyakati zetu kumekuwa na ongezeko kubwa la mgawanyiko huu ambapo wanaibuka mitume, manabii wakitangaza na kuhubiri Injili ya mafanikio. Swali la kujiuliza, Je, katika mgawanyiko huu, imani ya mitume tuliyorithi inaendelea kulindwa na madhehebu yanayozidi kumeguka? Je, Roho Mtakatifu, msaidizi aliyetuahidi Yesu atatufundisha ndivyo anavyotufundisha?

Kwa nini mgawanyiko huu? Uchu wa madaraka/uongozi, upinzani dhidi ya mafundisho ya kimaadili, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotuelekeza kwenye utakatifu kwa kuubeba msalaba alioufia na kutukombolea Yesu Kristo Mkombozi wetu ni moja ya vyanzo vya mgawanyiko na upinzani huu ndiyo maana wengi wanaoanzisha madhehebu haya wanatangaza Injili ya mafanikio wakiukataa Msalaba. Pili matatizo ya kijamii kama magonjwa, umaskini, kuvunjika kwa ndoa, kushuka kwa mizani na kupotea kwa dira ya maadili, kukata tamaa, manyanyaso, kukosa ajira, kutafuta utajiri au umaarufu kwa njia zisizo halali nayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kushamiri kwa Injili ya mafanikio, Pasaka bila Ijumaa kuu yaani utakatifu bila msalaba.

Mtume Paulo anatuonya juu ya injili ya mafanikio katika barua yake ya kwanza kwa Timoteo (1Tim.6:9-10) akisema; lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka haraka huanguka kwenye majaribu na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu, zenye kudhuru, zinazowazamisha katika uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda madaraka na fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha amani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi mno. Tufanye nini ili kujiepusha na janga hili? Kanisa Katoliki, linasisitiza waamini tushike maafundisho ya imani na maadili yanayotolewa na mamlaka funzi ya Kanisa pia tusiishi katika upweke wa kidini bali tuishi kijumuiya ili kusaidiana katika kutatua matatizo yanayotukabili kupitia jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, kwani ni njia ya kutuepusha na majanga ya kimaisha.

Tuisikilize sauti ya Yesu akituambia; “angalieni mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu wakisema, mimi ni Kristo, nao watawadanganya wengi” Mt 24:4-5, “jihadharini na manabii wa uwongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali” Mt 7:15-20. Haya yote yanawezekana tukiwa na sikio sikivu la kumsikiliza Roho Mtakatifu Kiongozi wetu anayetukumbusha yote aliyotufundisha Yesu kupitia kwa mitume. Tumsifu Yesu Kristo. 

Jumapili ya Sita ya Pasaka
21 May 2019, 13:45