Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka: Utii kwa Mungu kuliko kwa mwanadamu! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka: Utii kwa Mungu kuliko kwa mwanadamu! 

Jumapili ya Tatu ya Pasaka: Utii kwa Mwenyezi Mungu

Injili inatoa misingi ya mamlaka na ukuu wa Khalifa wa Mtume Petro. Mamlaka haya aliyakabidhiwa na Kristo mwenyewe. Tendo hili lilifanyika Yesu alipowatokea mara ya tatu wakivua samaki baada ya kufufuka kwake. Petro anakabidhiwa Kanisa baaada ya kuulizwa swali mara tatu, Simoni wa Yohane wanipenda, ili kumdhihirishia kuwa amesamehewa kosa lake la kumkana mara tatu!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 3 ya pasaka. Habari hii ni ya kweli: Licha ya kuwa kilikuwepo, kipo na kitaendelea kuwepo, kila kukicha kinamkuta ambaye mda wake umefika na kila mmoja wetu lazima kimpate mda wake ukifika, lakini bado kinabaki kuwa ni fumbo na kinatisha kuliko vitu vyote. Hiki si kingine bali ni kifo. Kifo kinatisha na kuogopesha, kila kikitokea kinaleta majonzi, huzuni, simanzi na masikitiko. Lakini maiti inatisha na kuogopesha zaidi ya kifo na ikitokea maiti imepiga chafya tunapatwa na kizungumkuti. Ikitokea maiti imezinduka au aliyezikwa akatokea panakuwa hapatoshi tunajawa na hofu na mashaka zaidi.

Hivi ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kawaida. Kwa mitume wa Yesu, ni kinyume kabisa. Kila walipomwona Kristo mfufuka walijaa furaha wakawa na ujasiri wa kutangaza habari zake. Hii ni kwa sababu kwa kifo na ufufuko wake ameshinda dhambi na mauti, kifo hakimtawali tena. Leo amewatokea mara ya tatu wanafunzi wake wakiwa ziwani wakivua samaki. Mwinjili Yohane anasema, wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. Ujasiri waliokuwa nao mitume baada ya ufufuko wa Kristo ulivyojidhihirisha katika somo la kwanza kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume unashangaza na kutuacha na maswali.

Iweje Mitume ambao walimkimbia Yesu alipokamatwa, walikamkana kwa kudai hawamjui, wakasimama mbali pale Karvari, tena baada ya kifo chake walionekana kukata tamaa na kujifichaficha, wakajifungia milango kwa hofu ya Wayahudi leo hii wanaonekana imara na kumshuhudia kwa nguvu zao zote?  Hii ni kwa sababu Jumapili iliyopita Yesu mfufuka alipowatokea na kujidhihirisha kwao kwa mara ya pili aliwavuvia na kuwajaza Roho Mtakatifu akiwaambia pokeeni Roho mtakatifu wowote mtakao waondolea dhambi wameondolewa na mtakao wafungia wamefungiwa na kisha akawaangiza na kuwatuma wakaihubiri habari njema ni Roho huyo huyo ndiye aliyewapa nguvu na ujasiri wa kutangaza habari za ufufuko wake Yesu na za mafundisho yake bila woga, wakianzia na Yerusalemu. Hawaogopi tena, hawana shaka wala wasiwasi wako vifua mbele wakisema; Mungu akiwa upande wetu ni nani wa kumwogopa?

Mafundisho yao ya kijasiri yanawatia uoga wale walioshinikiza kuuawa kwa Yesu, kwa sababu watu wengi waliamini kufufuka kwake na kwamba anafanya kazi katika nafsi za Mitume. Viongozi na wakuu wa wayahudi wanajaa mashaka na hofu nyingi kwamba watu wangeweza kulipiza kisasi kwa kosa lao la kumuuua Kristo ambaye kimsingi hakuwa na kosa lolote. Hivyo wanatumia nguvu kuwanyamazisha bila mafanikio. Ndiyo maana tumesikia Kuhani Mkuu akiwaonya Mitume akiwambia: “Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina la mtu huyu? Tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu” Nguvu na ushawishi wa Yesu Kristo unatambulikana sasa zaidi baada ya kuwa amefufuka kutoka wafu.

Hata hivyo, viongozi wa dini ya Kiyahudi hawataki kukubaliana na ukweli huo na ndio maana bado wanawazuia Mitume kuinjilisha. Msimamo wa Mitume unabaki ule ule; Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio. Hata walipopigwa na kuamuriwa kuacha kumtangaza Kristo, mitume walifurahi sana kwa kuwa waliaibishwa kwa ajili ya Kristo. Sisi leo furaha yetu iko wapi?

Pamoja na vitisho vingi habari za Yesu Kristo mfufuka zinaenea sehemu mbalimbali za Uyahudi na nje ya Uyahudi kama moto wa kiangazi kwa kauli mbiu ya mitume imetupasa kumtii Mungu kwanza kuliko mwanadamu.” Mitume sasa wanakumbuka mafundisho ya Kristo aliposema “Chakula changu ni kuyafanya mapenzi ya Baba yangu”.  Huu ndio ulikuwa msimamo wa Yesu Kristo mwenyewe na hivyo katika utume wake. Msimamo huu ndio uliomfanya aonekana mchochezi, mvunja sheria, mwana mapinduzi. Je, sisi katika orodha ya vipaumbele vyetu Mungu ana nafasi ya ngapi? Kati ya mali, starehe, madaraka Mungu yuko sehemu ipi?

Injili inatoa misingi ya mamlaka na ukuu wa Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtume Petro. Mamlaka haya aliyakabidhiwa na Kristo mwenyewe. Tendo hili lilifanyika Yesu alipowatokea mara ya tatu wakivua samaki baada ya kufufuka kwake. Petro anakabidhiwa Kanisa baaada ya kuulizwa swali mara tatu, Simoni wa Yohane wanipenda, ili kumdhihirishia kuwa amesamehewa kosa lake la kumkana mara tatu kabla jogoo hakuwika. Baada ya Petro kujibu kwa mfadhaiko mara ya tatu Bwana wewe wajua kuwa na kupenda, Kristo akampa mamlaka ya kuliongoza kanisa lake alilolianzisha yeye mwenyewe kwa kumpa madaraka na mamlaka kamili juu ya Kanisa. Mamlaka na madaraka haya anayapokea kila Baba Mtakatifu, Khalifa wa Petro anapochaguliwa kadiri ya mapokeo ya Kanisa.

Waamini wote kwa Sakramenti ya ubatizo, tulipewa jukumu la kumhubiri Kristo kwa maneno na matendo yetu. Tunapaswa kuwa jasiri wa kusimama katika imani yetu na kuilinda, kuipigania wakati wote na ikiwezekana hata kwa gharama ya maisha yetu. Maelfu ya wafiadini wako mbinguni kwa kuwa waliifia imani yao kwa Kristo. Hawakuwa watu wa pekeee tofauti na sisi. Si kusema hawakupenda maisha ya hapa duniani. La! Ila imani yao na upendo mkubwa kwa Kristo ndio uliowafanya waone maisha ya duniani si kitu. Kwa Ubatizo na kwa Kipaimara tumepokea kutoka kwa Roho Mtakatifu paji la UIMARA. Tutumie paji hili kuilinda imani yetu Kwa Kristo kwani anastahili yeye Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri, hekima na nguvu, heshima na utukufu. Barak ana heshima, utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, hata milele na milele. Amina. Tumsifu Yesu Kristo.

Jumapili 3 ya Pasaka

 

03 May 2019, 16:34