Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili V ya Kipindi cha Pasaka: Upendo ni Amri na Utambulisho wa Wafuasi wa Kristo! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili V ya Kipindi cha Pasaka: Upendo ni Amri na Utambulisho wa Wafuasi wa Kristo! 

Jumapili ya V ya Pasaka: Upendo ni Amri & Utambulisho wa Kikristo

Upendo ni amri ya Mungu tena ni amri iliyo kuu na sio ombi. Upendo ni kitambulisho cha wafuasi wa Kristo, mkipendana watu watawatambua kuwa mu-wafuasi wangu. Ni katika kuuishi upendo ndipo tunaweza kuurithi ufalme wa mbingu. Tusipowapenda wengine hasa adui zetu na kuwaombea ili waishi maisha marefu wapate kuongoka hatutaingia katika ufalme wa mbinguni. Neno hilo!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya pasaka. Upendo ni amri ya Mungu tena ni amri iliyo kuu na sio ombi. Upendo ni kitambulisho cha wafuasi wa Kristo, mkipendana watu watawatambua kuwa mu-wafuasi wangu. Ni katika kuuishi upendo ndipo tunaweza kuurithi ufalme wa mbingu. Tusipowapenda wengine hasa adui zetu na kuwaombea ili waishi maisha marefu wapate kuongoka hatutaingia katika ufalme wa mbinguni. Tukubali, tusikubali, tukatae, tusikatae habari ndiyo hiyo.

Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha matendo ya mitume linatueleza jinsi Paulo na Barnaba walihubiri kwa ujasiri na upendo mkuu katika Asia ndogo wakiwaimarisha wamini na kuwaonya wakae imara katika Imani, walipokuwa wanadhulumiwa na kuteswa akisema; imewapasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi (Mdo 14:22). Somo hili pia linatufundisha kuwa wazee wa kanisa huchaguliwa na roho mtakatifu anayejidhihirisha kwa njia ya kusali, kuomba na kufunga, na kisha kuchaguliwa wanawekewa mikono ishara ya kumpokea roho huyo ili awaongoze. Kumbe mamlaka ya uongozi sio ya kujitwalia, kujichukulia, kujivika na kujitangaza. Hili ni fundisho, onyo na angalisho kwa wanaowakimbilia wachungaji feki wanaoibuka katika nyakati zetu wakitangaza injili ya mafanikio. Paulo ametuambia; mbinguni tutaingia kwa njia ya dhiki nyingi na imani imara kwa Kristo na sio kwa mafanikio ya mambo ya ulimwengu huu.

Utabiri wa Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya; “mimi nitaumba mbingu mpya na dunia mpya, na ya kale yote hayatakumbukwa,” (Isa 65:17), huko watu watapata raha na furaha; huzuni na masikitiko vitapotea kabisa, wala hakutakuwa na kifo (Isa 35:10), Yohane anauona ukitimia baada ya hukumu ya mwisho, katika somo la pili kutoka kitabu cha Ufunuo, ya kuwa taabu zote zitakwisha, na viumbe vyote vitafanywa upya. Mungu atafanya maskani yake pamoja na watu wake, atafuta kila chozi katika macho yao. Wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Tazama, yote yanafanyika kuwa mapya kwa nguvu ya upendo wa Kristo alipokufa msalabani.

Upendo ni wosia aliotuachia Yesu Kristo kupitia kwa mitume wake katika karamu ya mwisho, siku ya alhamsi kuu akisema; Amri mpya nawapa, Mpendane kama vile mimi nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi. Wosia huu unakuwa ndio mwongozo wa maisha yao na ishara ya kuwatambulisha kuwa wao kweli ni wanafunzi wa Yesu. Kumbe upendo ni kitambulisho cha ufuasi wetu kwa Kristo. Wanafunzi wa kweli wa Kristo hujulikana kwa kushika amri hii mpya ya mapendo. Maneno nakupenda, kupenda, kupendwa, wapendwa, mapendo, mapenzi au upendo sio misamiati migeni.

Haya ni maneno ambayo tunayatumia katika maisha na mahusiano yetu ya kila siku, kwa nafasi mbalimbali na katika uelewa tofauti kwa lengo la kufikishiana ujumbe tarajiwa, tukielekeza hisia zetu kwa mtu fulani au kwa kitu chochote kile tunachokihitaji, kinachotupendeza, kinachotufurahisha, kinachotufaa au kile ambacho tunafaidika nacho. Lakini yawezakuwa hatuelewi tofauti na uzito wa upendo kati ya mtu na kitu au kati ya kitu kimoja na kingine. Kwa mfano; mmoja anaweza kusema nampenda Mungu, Yesu, Bikira Maria, na akasema nampenda baba, mama, kaka, mke, mwanangu na akatumia neno hilo hilo akisema napenda juisi, soda, pombe, nyama, maziwa, nguo au nampenda paka, twiga, ng’ombe, mbuzi au hata jiwe.

Swali la kujiuliza, Je, tutofautishe vipi upendo wetu kwa Mungu, kwa mama, baba, kwa rafiki, kwa mke au kwa mume? Ni katika maana gani na uzito upi tunalitumia neno upendo? Je, unavyompenda baba ni sawa sawa na unavyompenda paka au unavyopenda maziwa? Tunatofautisha vipi kati ya kumpenda mtu na kitu? Je, mipaka yetu iko wapi kati ya kumpenda mtu na kitu au Mungu na watu? Wayunani wanazo ngazi au aina kuu tatu za upendo na namna za kuuelezea. Upendo wa Mungu (agape) usiohesabu mabaya ndio unamfanya mtu kuutoa uhai wake kwa wengine, upendo wa kifamilia (filia) ni upendo kwa ndugu, jamaa na marafiki na upendo wa kimahusiano ya kimwili kati ya mume na mke (eros), ndio unaowaelekeza kwenye ndoa licha ya kuwa nyatika zetu upendo huu umechukua nafasi ya starehe zaidi nje ya malengo ya Mungu ya kushiriki uumbaji.

 

Swali lingine la kujiuliza ni kwa nini Yesu anaiita hii amri mpya wakati amri hii ya mapendo ilikuwepo tangu zamani katika Agano la Kale ikiwahimiza waisraeli; Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwanguvu zako zote na kwa akili zako zote. Ikapewa sifa ya amri ya kwanza na pili ni kama hii mpende jirani yako kama unavyojipenda? (Kumb 6:5, Wal 19:18). Kwa Wayahudi jirani ni yule myahudi mwenzao tu tena asiyekuwa na matatizo. Myahudi aliyekuwa na matatizo hasa magonjwa waliyosadiki yanatokana na laana ya dhambi hakuthaminika wala hakupendwa ndio maana wengine walitengwa na jamii hasa wakoma.

Yesu anaposema hii ni amri mpya anasisitiza; pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi. Maana yake Yeye Kristo awe mfano na kipimo cha mapendo kamili upendo unadai kujisadaka na kutoa uhai kwa ajili ya wengine. Hakuna upendo mkubwa zaidi ya huu, kuutoa uhai kwa ajili ya wengine. Upendo huu hauna vipimo wala vigezo bali unampenda mtu kwa kuwa na mtu au binadamu kwa kuwa ni binadamu bila kuangalia ni undugu, ukabila, mafanikio, utajiri, uwezo kiakili au wenye sifa zinazotuvutia. Mtume Paulo anasema ni upendo unaovumilia daima, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali ukweli. (1Kor. 4-6).

Upya wa amri hii ni kutokuwa na mipaka na matabaka. Hakuna kinachoweza kuuzuia. Ndiyo maana mtume Paulo anauliza, “nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo?” (Rum. 8:35), anajibu, hakuna kiwezacho kututenga na upendo wa Kristo: wala kifo, wala uhai, wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni, wala yanayotokea sasa, wala yatakayo tokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa, (Rum. 8:38-39) Hivyo mapendo halisi na ya kweli hayachagui wala hayana ubaguzi. Mtume Yohane anatuasa; Yeye asiyependa akaa katika mauti, na kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji; nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukaao ndani yake.” (1Yoh 3:14-15) 

Upendo wa kweli utatufikisha Mbinguni. Ujio wa Kristo haukuwa kwa ajili ya kufanya maisha yetu hapa duniani yawe rahisi. Ujumbe wa injili aliutoa Yesu sio injili ya utajiri wa mali na madaraja na ufahari. Bali ni kuubeba msabala na kumfuata. Inahitaji upendo kuwa na nguvu ya kuubeba msalaba. Taabu tuzipatazo katika kuuishi wosia wa Kristo wa kupendana, visitukatishe tamaa bali vituimarishe. Upendo ni neno rahisi kulitaja lakini ni vigumu kuliishi. Upendo unagharimu. Paulo katika somo la kwanza amesema, “imetupasa kuingia katika ufalme wa Mbinguni kwa kupitia njia ya dhiki kubwa.” Upendo si lelemama. Ulimgharimu Kristo maisha yake. Ndiyo maana alisema, “hakuna upendo ulio mkuu zaidi ya ule wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili rafiki zake. Je, kuna dhiki yoyote iliyo kubwa zaidi ya kutoa uhai? Yohane katika somo la Pili ametuasa akisema; tujipe moyo hata kama tunaishi upendo kwa dhiki, dhiki yetu haitapotea bure. Utafika wakati Mungu atakapofuta kila chozi katika macho yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Jumapili 5 ya Pasaka
16 May 2019, 17:41