Tafuta

Marehemu Askofu Emmanuel Alex Mapunda atakumbukwa sana kama Baba, Mwalimu na Mlezi wa miito aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia haki na ukweli! Marehemu Askofu Emmanuel Alex Mapunda atakumbukwa sana kama Baba, Mwalimu na Mlezi wa miito aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia haki na ukweli! 

Askofu Emmanuel Mapunda alikuwa: Baba, Jalimu na Mlezi!

Marehemu Askofu Emmanuel Alex Mapunda alikuwa ni Baba, Jalimu na Mlezi ambaye ameacha pengo kubwa sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania. Huu ndio muhtasari wa maisha na utume wake kama: Padre na Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Mbinga. Haya yamesemwa na Askofu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi, Alhamisi, tarehe 23 Mei 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Marehemu Askofu Emmanuel Alex Mapunda aliyefariki dunia tarehe 16 Mei 2019 akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, amezikwa kwa heshima zote Jimboni Mbinga alikohudumia kama mchungaji mkuu kwa muda wa miaka 32. Waamini wa Jimbo kuu la Songea na vitongoji vyake, walipata nafasi ya kusali na kumwombea, akiwa njiani kuelekea Jimboni Mbinga, ili kupumzishwa kwenye usingizi wa amani.

Marehemu Askofu Emmanuel Alex Mapunda alikuwa ni Baba, Mwalimu na Mlezi ambaye ameacha pengo kubwa sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania. Huu ndio muhtasari wa maisha na utume wake kama: Padre na Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Mbinga. Haya yamesemwa na Askofu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi, Alhamisi, tarehe 23 Mei 2019, kwenye Kanisa la Abasia ya Peramiho, Jimbo kuu la Songea. Askofu Nyongani anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kumuenzi Marehemu Askofu Mapunda aliyejisadaka katika kufundisha, kutangaza na kushuhudia ukweli na haki kwa ajili ya watu wa Mungu.

Marehemu Askofu Emmanuel Mapunda alikuwa ni Baba na mlezi na historia nzima ya maisha yake imefumbatwa katika tunu hizi msingi hadi mauti yalipomfika. Alikuwa ni nguzo ya malezi na majiundo makini kwa waseminari, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa la Mungu linapata wakleri waliofundwa na kufundika barabara ili kupata mapadre watakaojisadaka bila yakujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Kanisa linawahitaji mapadre: wema, watakatifu na wachamungu; wanaoweza kutambua changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zilizoko katika maisha, tayari kuzifanyia kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu wanaowahudumia kwa moyo, akili na nguvu zao zote!

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican Mama Oliver Luena, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa katika salam zake za rambi rambi anasema, Marehemu Askofu Emmanuel Mapunda, alikuwa ni Baba mnyenyekevu, mkimya na wala hakupenda makuu. Lakini, katika undani wake, alikuwa ni chemchemi ya busara na hekima iliyomwezesha kusongesha mbele maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Mbinga. Aliwahamasisha sana WAWATA kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, ili kusaidia malezi na majiundo ya familia, kwani wao ni walimu na makatekista wa kwanza!

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Askofu Emmanuel Alex Mapunda alizaliwa tarehe 10 Desemba 1935 huko Parangu. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83. Alipadrishwa tarehe 8 Agosti 1965, akiwa Padre wa Jimbo kuu la Songea. Kumbe, amefariki dunia akiwa amelitumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 53. Tarehe 22 Desemba 1986 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Mbinga lililomegwa kutoka Jimbo kuu la Songea. Askofu Mapunda akawekwa wakfu tarehe 6 Januari 1987 na Mtakatifu Yohane Paulo II kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 12 Machi 2011 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akaridhia ombi lake la  kutaka kung’atuka kutoka madarakani baada ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Mbinga kwa muda wa miaka 32!

Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuzipokea kazi za Mtumishi wake Askofu Mstaafu Emmanuel Alex Mapunda na amstahilishe maisha na uzima wa milele miongoni mwa wateule wake! Kwa ufupi, maisha na utume wake kama Padre: Mara baada ya kupadirishwa, Padre Emmanuel Mapunda alitumwa kuwa Paroko Msaidizi, Parokia ya Matogoro, ambako alifanya utume huo toka Januari hadi Agosti 1966; na baada ya hapo alitumwa kuwa Mlezi na Mkufunzi wa Seminari Ndogo ya Hanga na akahudumia hadi mwishoni mwa 1967; wakati huo Seminari hiyo ilikuwa chini ya Jimbo la Songea. Toka mwaka 1968 hadi 1969, alitumwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Songea na akaongezewa jukumu la kufundisha Dini katika Shule za Sekondari mjini Songea.

Mwaka 1970 Padre Emmanuel Mapunda alitumwa kwa mara ya kwanza Seminari Kuu Peramiho kuwa Kiongozi wa maisha ya Kiroho. Utume huo ulikatishwa alipotumwa masomoni Roma, na baada ya kurejea toka masomoni, mwaka 1973 alitumwa tena Seminari Kuu, Peramiho, kuwa Mlezi na Mkufunzi. Kuanzia mwaka 1976, pamoja na majukumu mengine, aliihudumia Seminari Kuu kama Gombera Msaidizi wa Seminari hiyo hadi mwaka 1980 kabla ya kwenda tena masomoni Roma. Baada ya kuhitimu masomo yake na kurejea Jimboni, mwaka 1983 alirudishwa tena kwa mara ya tatu Seminarini Peramiho mwaka 1983 kuwa Mlezi na Mkufunzi hadi mwaka 1986.

Katika awamu hiyo ya tatu ya kuhudumia Seminari Kuu Peramiho, alipewa tena dhamana na utume wa kuongoza kama Gombera kuanzia Desemba 1985 hadi Desemba 1986 alipoteuliwa kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mbinga. Mwaka 2013, kama Askofu Mstaafu wa Jimbo la Mbinga, alirudi tena kwa mara ya nne kuwa Mlezi na Mkufunzi katika Seminari Kuu ya Peramiho, kila wiki, akitokea Parokiani Nangombo, makazi yake baada ya kustaafu hadi umauti ulipomkuta.

Askofu Mapunda
24 May 2019, 14:37