Tafuta

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Tanzania, tarehe 15 Mei 2019 ina sherehekea Miaka 30 ya Huduma katika: Kutibu, Kuelimisha na Kufariji! Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Tanzania, tarehe 15 Mei 2019 ina sherehekea Miaka 30 ya Huduma katika: Kutibu, Kuelimisha na Kufariji! 

Hospitali ya Mt. Gaspar, Itigi: Tibu, Elimisha & Fariji! Miaka 30 ya Huduma kwa watoto & maskini

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, ilifunguliwa rasmi tarehe 15 Mei 1989 na Mzee Ali Hassan Mwinyi. Mwaka 2010 Serikali ya Tanzania ikaipandisha hadhi na kuwa ni Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa. Hospitali ina jumla ya vitanda 320; watumishi 297 na wodi kuu nne. Inaongozwa na kauli mbiu "Tibu, Elimisha na Fariji". Kipaumbele cha kwanza ni watoto na maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. wakisukumwa na kauli mbiu ya: Elimisha, Tibu na Fariji walianza rasmi kutoa huduma za afya Itigi, Manyoni, Singida nchini Tanzania 15 Septemba 1987. Lengo kuu likiwa ni kutoa huduma kwa maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Itigi ya wakati huo si Itigi ya Mwaka 2019! Nia hii njema ilizidi kukuwa na baada ya miaka miwili huduma hii ilipanuka na hivyo kufunguliwa rasmi kwa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar na Mzee Ali Hassan Mwinyi tarehe 15 Mei 1989.

Miaka 30 ya uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, imeendelea kupanuka na kukua katika shughuli na huduma zake na Mwezi Novemba Mwaka 2010 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuipandisha hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya mkoa. Hospitali ina jumla ya vitanda 320. Katika wodi kuu nne ambazo ni:-Wodi ya magonjwa mchanganyiko (Medical ward), Wodi ya Upasuaji (Surgical ward), Wodi ya Uzazi na Magonjwa ya Kike (Obstetrics & Gynaecology), Wodi ya watoto chini ya miaka 12 (Paediatrics ward) na Wodi maalum na ya magonjwa ya mlipuko ((Privates & Isolation).

Kwa hivi sasa Hospitali ina jumla ya watumishi 297 kati yao 50 tu ndio wanalipwa ruzuku na Serikali. Hospitali inao madaktari bingwa 5. Ili kuboresha zaidi huduma ya tiba kwa wagonjwa, kwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, ikaanzisha Chuo cha Uuguzi cha Mtakatifu Gaspar, kwa kuongozwa na kauli mbiu mbiu “Tufanye mengi, vizuri na kwa haraka”. Tarehe 9 Mei 2019, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, imezindua maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa tiba bure pamoja na kuwapatia wananchi nafasi ya kufanya uchunguzi wa magonjwa mbali mbali.

Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 15 Mei 2019 kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar inayomilikiwa na kuendeshwa na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, ni kipindi muafaka cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini!

Huu ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini. Huu ni muda muafaka wa kuendelea kujikita zaidi katika: kuelimisha, Kutibu na Kufariji, Kauli mbiu inayoongoza huduma za tiba zinazotolewa Hospitalini hapo! Matarajio kwa siku za mbeleni: Ushirikiano uliopo kati ya Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaendelezwa na kuzidi kukua ili kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia hata wale wasiokuwa na kipato kikubwa.

Hospitali inapania kutoa huduma zote za kibingwa kwa watoto kwa kuwa wanayo makubaliano na Hospitali ya “Bambino Gesù” inayomilikiwa na kuongozwa na Vatican, ambayo ni hospitali maalumu kwa magonjwa ya watoto tu. Ushirikiano na Hospitali ya Bambino Gesù ulianza kunako mwaka 2008, ushirikiano ambao umesaidia ujenzi na maboresho ya wodi ya watoto; msaada wa huduma ya tiba kimataifa pamoja na ujenzi wa chumba cha upasuaji kwa ajili ya watoto. Ushirikiano kati ya Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi pamoja na Hospitali ya Bambino Gesù, umepyaishwa na kuimarishwa zaidi tangu Mama Mariella Enock, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù alipotembelea na kujionea mwenyewe jinsi ambavyo Hospitali hii inatangaza na kushuhudia Injili ya huruma na huduma kwa wagonjwa na maskini, hususan watoto wadogo ambao wamepewa kipaumbele cha pekee!

Hospitali Itigi 30 Years
14 May 2019, 10:09