Tafuta

Vatican News
Patriaki Daniel anawahimiza waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili na utu wema! Patriaki Daniel anawahimiza waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili na utu wema!  (ANSA)

Hija ya Kitume Romania: Hotuba ya Patriaki Daniel: Ushuhuda!

Wakristo wanahamasishwa kutangaza na kushuhudia imani; kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Maadhimisho ya Liturujia Takatifu iwe ni sehemu ya mchakato wa kuunganisha maadhimisho haya na uhalisia wa maisha ya watu! Sala imwilishwe katika matendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Patriaki Daniel wa Kanisa la Kiorthodox la Romania, Ijumaa, tarehe 31 Mei 2019, amemkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Upatriaki wa Kanisa la Kiorthodox nchini humo kwa kukumbushia hija ya kitume, ya Mtakatifu Yohane Paulo II, miaka ishirini iliyopita! Wakati huo, Patriaki Teoctist na Mtakatifu Yohane Paulo II ni viongozi walionja makali ya utawala wa Kikomunisti, wakawa na ujasiri wa kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya imani ya Kanisa.

Patriaki Daniel anakaza kusema, ni ujasiri huu ulioisukuma Serikali kudumisha uhuru wa kidini na kuabudu, kiasi hata ch Sherehe ya Pasaka kuwa ni Siku kuu ya kitaifa. Hawa walikuwa ni viongozi waliosimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wameimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu na kufanikiwa kuwatangazia vijana upendo wa huruma ya Mungu, maisha na uzima wa milele. Viongozi hawa kwa sasa wanawahamasisha Wakristo wa nyakati hizi kutangaza na kushuhudia imani; kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kuwahamasisha waamini na watu wenye mapenzi mema, kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Maadhimisho ya Liturujia Takatifu iwe ni sehemu ya mchakato wa kuunganisha maadhimisho haya na uhalisia wa maisha ya watu! Sala inapaswa kumwilishwa katika huduma kwa maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Injili ya Kristo inawataka waamini kusimamia haki, upatanisho na mshikamano, ili upendo na baraka ya Kristo Yesu, uweze kuwafikia na kuwaambata wote, ili hatimaye, watu waweze kupata amani na furaha!

Patriaki Daniel
31 May 2019, 18:55