Chama cha Kitume cha Kutetea Maisha na Familia kutoka Kanisa Katoliki nchini Canada, kinawataka waamini kusimama kidete kutetea na kuendeleza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Chama cha Kitume cha Kutetea Maisha na Familia kutoka Kanisa Katoliki nchini Canada, kinawataka waamini kusimama kidete kutetea na kuendeleza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. 

Simameni kidete kulinda uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baada ya kuruhusu sera za utoaji mimba, sasa Canada imepitisha pia sheria inayoruhusu kifo laini au “Eutanasia” pamoja na watu kusaidiwa kujinyonga hadi kufa! Hii ni kufuru dhidi ya Injili ya uhai, zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kana kwamba, haya hayatoshi, Serikali ya Canada inaendelea kuandaa mbinu mkakati unaojulikana kama “Medical Aid in Dying” (MAID). Utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Kitume cha Kutetea Maisha na Familia kutoka Kanisa Katoliki nchini Canada, “COLF”, kinaandaa maandamano makubwa kwa ajili ya kutetea maisha, yatakayofanyika kitaifa, mjini Ottawa, Alhamisi tarehe 9 Mei 2019. Hii pia ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu kupitishwa kwa sheria ya utoaji mimba nchini Canada. Nchi nyingine ambazo zinaruhusu utoaji mimba kisheria ni pamoja na China, Korea ya Kaskazini pamoja na Vietnam. Chama hiki cha kitume kinasikitika kusema kwamba, utamaduni wa kifo umeanza kuingia kwa nguvu sana nchini Canada.

Baada ya kuruhusu sera za utoaji mimba, sasa Canada imepitisha pia sheria inayoruhusu kifo laini au “Eutanasia” pamoja na watu kusaidiwa kujinyonga hadi kufa! Hii ni kufuru dhidi ya Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kana kwamba, haya hayatoshi, Serikali ya Canada inaendelea kuandaa mbinu mkakati unaojulikana kama “Medical Aid in Dying” (MAID) yaani Huduma ya Kitabibu kwa Ajili ya Kifo. Walengwa ni watoto wanaozaliwa wakiwa na ulemavu, wagonjwa wa akili pamoja na wagonjwa wanaosumbuliwa kwa muda mrefu!

Hawa ni watu ambao hawana tena uwezo wa kufanya maamuzi juu ya hatima ya maisha yao, bali kuna watu wanaoweza kuwaamria. Huu ni utamaduni wa kifo. Watu wanasahau kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Zawadi hii inapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa na wote. Kazi ya uumbaji ni kielelezo kikubwa cha upendo wa Mungu unaotakatifuza na kuokoa. Wakristo wanapaswa kumwilisha fadhila ya matumaini katika maisha yao. Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ameshinda dhambi na kifo.

Fumbo la Pasaka linawawajibisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete dhidi ya sera na utamaduni wa kifo, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai! Dhambi na ubaya vitaendelea kushamiri ulimwenguni, ikiwa kama watu wema na watakatifu, hawatajitokeza kupambana na hali hii, kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Wasimame kuwatetea watoto ambao bado hawajazaliwa; wawasaidie wanawake wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha pamoja na kuwahudumia kwa imani, upendo na matumaini watu wanaoteseka na wale ambao wako kufani!

Chama cha Kitume cha Kutetea Maisha na Familia kutoka Kanisa Katoliki nchini Canada kinasema, kitaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge ndani ya jamii, ili haki, utu na heshima ya binadamu viweze kurejeshwa tena nchini Canada, kwa kutetea zawadi ya maisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Wakati wa maandamano haya, waamini wanakumbushwa maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II anayesema kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu kwa sababu ni zawadi kutoka kwa Mungu, mwenye upendo usiokuwa na kifani!

Injili ya Uhai
07 May 2019, 09:59