Mahujaji kutoka Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kati ya mahujaji walioshiriki katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 22 Mei 2019 Mahujaji kutoka Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kati ya mahujaji walioshiriki katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 22 Mei 2019 

Mahujaji wa Chama cha Wanawake Tanzania wakutana na Papa, Roma!

Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Jumatano tarehe 22 Mei 2019 wamehudhuria kwenye Katekesi ya Papa Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahojiano na Radio Vatican Mama Oliver Luena, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa amesema, kundi la WAWATA lilikuwa na jumla ya wanawake 57, kati yao kulikuwepo pia Mapadre wawili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anakumbusha kwamba, maisha ya binadamu ni hija na kuwa mwanadamu mwenyewe ni mhujaji hapa duniani. Ni mtu anayesafiri kwenda nyumbani kwa Baba. Hija inapaswa kuwa ni nyenzo ya toba na wongofu wa ndani; huruma na mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu, ili kuwa vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia! Hija inahitaji maandalizi, sadaka na majitoleo, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa walimwengu!

Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Chama cha WAWATA kinajishughulisha na shughuli zote za kuwaendeleza wanawake kiroho na kimwili ili waweze kutoa mchango wao kikamilifu katika kujiendeleza kulistawisha kanisa na jamii kwa ujumla katika nyanja za kiroho, matendo ya huruma, uchumi na maendeleo endelevu.

WAWATA inaongozwa na dhamira kuu: Kwa Upendo wa Kristo Tutumikie na Kuwajibika. Muundo wa WAWATA umeanzia katika Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, Vigango, Dekania, Parokia, Jimbo hadi Taifa kama ulivyo muundo wa Kanisa Katoliki Tanzania na kila mwanamke Mkatoliki ni mwanachama wa WAWATA. Kimataifa WAWATA ni mwanachama wa Shirikisho la Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO-World Union of Catholic Women Organization) lililoanzishwa kunako mwaka 1910 na makao yake makuu yako Paris, nchini Ufaransa. Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Jumatano tarehe 22 Mei 2019 wamehudhuria kwenye Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican Mama Oliver Luena, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa amesema, kundi la WAWATA lilikuwa na jumla ya wanawake 57, kati yao kulikuwepo pia Mapadre wawili. Tangu walipoondoka kutoka Dar es Salaam tayari wametembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno, wakatembelea mahali apozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila na Loyola, mahali alipozaliwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Muasisi wa Shirika la Wayesuit. Mambo makuu waliobaki nayo kutoka Fatima, Ureno ni: kuhusu muhimu wa maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani, changamoto endelevu katika kuutafuta na kuambata utakatifu wa maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu.

Kutoka Ureno, WAWATA wakaenda hadi kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa na huko wamejifunza kwamba, Madhabahu ni daraja la kuwakutanisha watu katika maisha ya kiroho! Waamini wengi wameweza kung’amua miito ya maisha na utume wao kwa kutembelea madhabahu ya Bikira Maria. Hapa pia ni mahali pa toba na wongofu wa ndani; mahali pa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani; ni mahali pa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu!

Mahujaji hawa wametembelea Assisi mahali alikozaliwa Mtakatifu Francisko wa Assisi ambaye anakumbukwa kwa mambo makuu matatu: huduma kwa maskini, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja umuhimu wa kulinda na kudumisha amani ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mahujaji kutoka Tanzania, kamwe hawawezi kufika Italia bila ya kwenda kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Rita wa Cascia. Amana na utajiri wa maisha yake ya kiroho umejikita katika: Wito wa utakatifu wa maisha kwa Wakristo wote; umuhimu wa kusamehe na kusahau pamoja na kupenda Msalaba, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa: Hekima, huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Mtakatifu Rita wa Cascia anakumbukwa na wengi kama mwombezi wa mambo yaliyoshindikana.

Mahujaji kutoka Tanzania wametembelea “San Giovanni Rotondo” na huko wamejifunza kutoka kwa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina kwamba, Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Lakini, Mama Kanisa anao watoto wake ambao wanaogelea katika lindi la dhambi! Papa Francisko anasema, Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina alilipenda Kanisa, kiasi hata akapewa neema ya kusamehe na kusahau! Haiwezekani kuendelea kuishi ndani ya Kanisa kwa kulishutumu kila kukicha kama anavyofanya Shetani, Ibilisi!

Baba Mtakatifu anawataka waamini wawe na ujasiri wa kuonesha udhaifu na mapungufu ya Kanisa, lakini pia walipende na kuliheshimu Kanisa. Makosa yarekebishwe kwa toba na wongofu wa ndani ili Kanisa lisonge mbele! Wakiwa mjini Roma, WAWATA wametembelea na kusali kwenye Makanisa makuu yaliyoko Jimbo kuu la Roma. Kwa kweli ni hii ni hija ambayo imekuwa na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio makuu yaliyotolewa na Shirikisho la Wanawake Wakatoliki Duniani kwa Mwaka 2018-2022 yaani: Kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia; Utunzaji bora wa Mazingira nyumba ya wote; Malezi na majiundo makini kwa watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi na hatimaye, umuhimu wa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha!

WAWATA: Roma
23 May 2019, 16:29