Tafuta

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeonesha nia ya kushirikiana na UNICEF kwa ajili ya kuwalinda, kuwatetea na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeonesha nia ya kushirikiana na UNICEF kwa ajili ya kuwalinda, kuwatetea na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. 

Baraza la Makanisa Ulimwenguni & UNICEF: Huduma kwa watoto!

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawaangalia kwa namna pekee watoto wakimbizi na wahamiaji. Hawa ni watoto ambao wako hatarini kutumbukizwa kwenye mtandao wa biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo pamoja na nyanyaso. Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za watoto hawa! Huduma kwa watoto!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, linaunga mkono juhudi zinazotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, ili kuhakikisha kwamba, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi walindwa na kutunzwa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki zao msingi zinalindwa na wote.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawaangalia kwa namna pekee watoto wakimbizi wasioambatana na wazazi wala walezi wao. Hawa ni watoto ambao wako hatarini kutumbukizwa kwenye mtandao wa biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo pamoja na nyanyaso za aina mbali mbali. Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za watoto hawa. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyoibuliwa na wajumbe walioshiriki hivi karibuni kwenye semina kuhusu wajibu na dhamana ya Makanisa katika ulinzi wa watoto wadogo.

Mosi ni kuhakikisha kwamba, haki msingi za watoto hawa zinaendelezwa na kudumishwa dhidi ya nyanyaso na mifumo yote ya kibaguzi. Pili, Watoto washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Tatu, ni kuhakikisha kwamba, Kanisa na Jamii inaunda mazingira yanayojikita katika misingi ya haki, amani na usalama kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto! Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na UNICEF linataka kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limechapisha Hati ijulikanayo kama “Churches’ Commitments to Children” yaani “Wajibu wa Makanisa katika Ulinzi wa Watoto”. Makanisa mahalia yanaweza kusaidia kuragibisha mchakato wa maboresho ya hali na maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, sehemu mbali mbali za dunia! Dhamana hii kwa sasa inapaswa kutafsiriwa katika matendo kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za watoto; kuendeleza mchakato wa haki na amani; kuanzisha miradi na huduma kwa ajili ya kuwasindikiza watoto wahamiaji.

Makanisa yaangalie jinsi ya kuanzisha ushirikiano na wanasiasa kwa ajili ya maboresho ya maisha na huduma kwa watoto; kwa kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya Makanisa haya katika kambi za wakimbizi sehemu mbali mbali za dunia. Katika mwelekeo huu wa majadiliano ya kiekumene, Wakristo wanaweza kupiga hatua moja mbele, kwa kuanzisha pia majadiliano ya kidini, kwa kushirikiana na waamini wa dini ya Kiislam kwa ajili ya huduma kwa watoto wadogo. Makanisa yanataka kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na haki za watoto wakimbizi na wahamiaji wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo!

Watoto
21 May 2019, 10:27