Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika linawaalika wananchi wenye sifa za kupiga kura kujitokeza kwa wingi; wadumishe, haki, amani, maridhiano na umoja wa Kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika linawaalika wananchi wenye sifa za kupiga kura kujitokeza kwa wingi; wadumishe, haki, amani, maridhiano na umoja wa Kitaifa. 

SACBC: Uchaguzi Mkuu Afrika ya Kusini: Haki, Amani na Ukweli!

Askofu Sithembele Sipuka, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, SACBC anasema, Afrika ya Kusini, Jumatano tarehe 8 Mei 2019 inafanya uchaguzi mkuu wa sita. Wananchi wote wa Afrika ya Kusini wenye haki ya kupiga kura wanapaswa kujitokeza bila kukosa kwa sababu huu ni wajibu wao wa kikatiba, kimaadili na maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, SACBC, lililoanzishwa kunako Mwaka 1947 linaundwa na Nchi za Afrika ya Kusini, Bostwana na Swaziland. Askofu Sithembele Sipuka, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika anasema, Afrika ya Kusini, Jumatano tarehe 8 Mei 2019 inafanya uchaguzi mkuu wa sita. Wananchi wote wa Afrika ya Kusini wenye haki ya kupiga kura wanapaswa kujitokeza bila kukosa kwa sababu huu ni wajibu wao wa kikatiba, kimaadili na maisha ya kiroho.

Askofu Sipuka anasema kuna wananchi wengi wa Afrika ya Kusini waliopoteza maisha yao, kwa kudai demokrasia ya kweli nchini humo. Kumbe, kila mwananchi anapaswa kuhakikisha kwamba, anawajibika barabara kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu, ili kweli uchaguzi huu, uweze kuwa wa: haki, kweli na huru. Wananchi wajenge mazingira yatakayosaidia kukuza na kudumisha umoja wa kitaifa, maridhiano, haki na amani, ili watu waweze kupiga kura pasi na wasi wasi na hivyo kuwachagua viongozi wanaowapenda.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, linapenda kulaani wale wote wanaotaka kuvuruga uchaguzi mkuu kwa mafao yao binafsi, kwa kutaka kufanya vurugu na ghasia waache mara moja. Kila mwananchi awajibike kujenga na kudumisha amani, maridhiano, umoja na upatanisho. Amani ikisha kutoweka, ni vigumu sana kuweza kurejeshwa tena. Maaskofu wanawataka wanasiasa pamoja na wapambe wao, kujenga ustaarabu na kuhakikisha kwamba, wanafuata: sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi mkuu nchini Afrika ya Kusini. Waamini waendelee kusindikiza zoezi hili kwa njia ya sala zao!

Afrika ya Kusini
07 May 2019, 09:30