Tafuta

Vatican News
Askofu Mstaafu Gabriel Mmole wa Jimbo Katoliki Mtwara, Tanzania amefariki dunia, tarehe 15 Mei 2019 na atazikwa tarehe 21 Mei 2019 kwenye Kanisa kuu la Watakatifu wote, Mtwara. Askofu Mstaafu Gabriel Mmole wa Jimbo Katoliki Mtwara, Tanzania amefariki dunia, tarehe 15 Mei 2019 na atazikwa tarehe 21 Mei 2019 kwenye Kanisa kuu la Watakatifu wote, Mtwara.  (ANSA)

TANZIA: Askofu Gabriel Mmole amefariki dunia, kuzikwa 21 Mei 2019

Askofu Mstaafu Gabriel Mmole alizaliwa kunako mwaka 1939. Baada ya masomo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 14 Oktoba 1971. Kunako tarehe 12 Machi 1988, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara na kuwekwa wakfu tarehe 25 Mei 1988. Akang'utuka madarakani mwaka 2015 na amefariki dunia, 15 Mei 2019. Anazikwa 21 Mei.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasikitika kutangaza kifo cha Askofu mstaafu Gabriel Mmole wa Jimbo Katoliki Mtwara, kilichotokea alfajiri ya tarehe 15 Mei 2019 huko Mtwara baada ya kuugua kwa muda mrefu pamoja na uzee. Marehemu Askofu Gabrieli Mmole, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 tangu alipozaliwa kunako mwaka 1939 huko Mbwinji, Wilayani, Masasi na alikuwa ni kati ya Maaskofu wenye umri mkubwa nchini Tanzania!

Askofu Titus Josefu Mdoe wa Jimbo Katoliki la Mtwara anasema, maziko ya Askofu Gabrieli Mmole yatafanyika tarehe 21 Mei 2019 kwenye Kanisa kuu la Watakatifu wote, Jimbo Katoliki Mtwara. Askofu Mdoe anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwombea Marehemu Askofu Gabrieli Mmole, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuzipokea kazi zake njema alizozifanya kama Padre na Askofu kwa muda wa miaka 31 na apende kumpumzisha kwa amani, miongoni mwa watakatifu wake!

Askofu Gabriel Mmole alizaliwa kunako mwaka 1939. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 14 Oktoba 1971, wakati huo, likiitwa Jimbo la Ndanda, Tanzania. Kunako tarehe 12 Machi 1988, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara na kuwekwa wakfu tarehe 25 Mei 1988. Ibada hii ikaongozwa na Kardinali Laurean Rugambwa, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Baada ya kuwahudumia watu wa Mungu Jimbo Katoliki Mtwara, akiwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza, tarehe 15 Oktoba 2015 akang’atuka kutoka madarakani!

Jimbo Katoliki la Mtwara na familia ya Mungu nchini Tanzania katika ujumla wake, imempoteza Baba na mchungaji, aliyekuwa mpole na mnyenyekevu. Katika maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu alikazia sana katekesi makini: kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala kama chemchemi ya utakatifu wa maisha. Kutokana na changamoto za kichungaji, alitoa kipaumbele cha kwanza kwa elimu na hasa kwa kuwawezesha watawa waliokuwa wanahitimu darasa la saba kuendelea na masomo ya sekondari na leo hii, kuna watawa ambao wamebobea katika medani mbali mbali za maisha, matunda na juhudi za Askofu Gabriel Mmole. Alijisadaka pia katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, ili kujenga umoja, upendo na mshikamano wa kitanzania!

Askofu Mmole
15 May 2019, 16:33