Tafuta

Vatican News
Askofu mstaafu Emmanuel Alex Mapunda wa Jimbo Katoliki Mbinga amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83! Fumbo la Pasaka, liwsaidie waamini kukipoea kifo kwa imani! Askofu mstaafu Emmanuel Alex Mapunda wa Jimbo Katoliki Mbinga amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83! Fumbo la Pasaka, liwsaidie waamini kukipoea kifo kwa imani!  (Vatican Media)

TANZIA: Askofu Emmanuel Alex Mapunda afariki dunia! Mazishi 24 Mei 2019

Askofu mstaafu Emmanuel Alex Mapunda alizaliwa mwaka 1935. Alipadrishwa tarehe 8 Agosti 1965 Kumbe, amefariki dunia akiwa amelitumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 53, kwa hakika si haba! Tarehe 22 Desemba 1986 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbinga, Tanzania na kuwekwa wakfu tarehe 6 Januari 1987 na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Maisha ya mwanadamu yana mwanzo na utimilifu wake. Tafakari ya kina kuhusu kifo katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, iwasaidie waamini kukipokea kifo kadiri ya mafundisho ya Kanisa. Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ndani mwake, waamini wanachota tumaini lao moja, yaani kwa kutoka katika maisha ya hapa duniani ili kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kanisa linafundisha kwamba, kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti.

Huu ni  utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kwa maji na Roho Mtakatifu kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kwa kufanana kamili na “sura ya Mwana” kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme wa Mungu, uliotangulizwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, hata kama analazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wamepata kutoka kwa Kristo Yesu tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Waamini wanasikitika sana kwa sababu wanajua kwamba, iko siku watakufa, lakini wanatulizwa na mafundisho ya Kanisa kwamba, uzima wa waamini hauondolewi ila unageuza tu. Nayo makao ya hapa duniani yakisha bomolewa, wanapata makao ya milele mbinguni!

Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Askofu Mstaafu Emmanuel Alex Mapunda wa Jimbo Katoliki Mbinga, nchini Tanzania aliyefariki dunia, Alhamisi, tarehe 16 Mei 2019 akiwa njiani kwenda Dar es Salaam kwa matibabu zaidi. Marehemu Askofu Emmanuel Alex Mapunda alizaliwa tarehe 10 Desemba 1935 huko Parangu. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83. Alipadrishwa tarehe 8 Agosti 1965, akiwa Padre wa Jimbo kuu la Songea. Kumbe, amefariki dunia akiwa amelitumia Kanisa kama Padre kwa miaka 53, kwa hakika si haba! Baba Mapunda nenda kapumzike kwa amani!

Tarehe 22 Desemba 1986 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbinga, Tanzania na kuwekwa wakfu tarehe 6 Januari 1987 na Mtakatifu Yohane Paulo II kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, hadi raha! Tarehe 12 Machi 2011 akang’atuka kutoka madarakani baada ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Mbinga kwa muda wa miaka 32! Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuzipokea kazi za Mtumishi wake Askofu Mstaafu Emmanuel Alex Mapunda na amstahilishe maisha na uzima wa milele miongoni mwa wateule wake!

Askofu E Mapunda.

 

17 May 2019, 16:57