Jumapili ya IV ya Pasaka; Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 56 ya Kuombea Miito: Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande anasimikwa rasmi Jimbo kuu la Mwanza. Jumapili ya IV ya Pasaka; Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 56 ya Kuombea Miito: Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande anasimikwa rasmi Jimbo kuu la Mwanza. 

Askofu mkuu Renatus Nkwande, Jimbo kuu la Mwanza: 12 Mei 2019

Askofu mkuu mteule Nkwande, anatarajiwa kusimikwa rasmi Jumapili ya Kristo Yesu, Mchungaji mwema sanjari na maadhimisho ya Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani. Tukio hili linatanguliwa na Masifu ya Jioni, tarehe 11 Mei 2019 ambamo ataonesha hati za uteuzi wake, atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu, ataongoza masifu ya jioni, atakiri Kanuni ya imani na kula kiapo cha utiikwa Papa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu mteule Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, Ijumaa tarehe 10 Mei 2019 ameagwa rasmi na Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Bunda, tayari kuanza safari ya kuandika ukurasa mpya wa maisha na utume wake, Jimbo kuu la Mwanza. Askofu mkuu mteule Nkwande, anatarajiwa kusimikwa rasmi, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu, Mchungaji mwema sanjari na maadhimisho ya Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani. Tukio hili linatanguliwa na Masifu ya Jioni, Jumamosi, tarehe 11 Mei 2019 ambamo ataonesha hadharani hati za uteuzi wake, atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu, ataongoza masifu ya jioni, atakiri Kanuni ya Imani pamoja na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule alipadrishwa kunako mwaka 1995. Tarehe 27 Novemba 2010, akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bunda na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 20 Februari 2011 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, utume ambao ameutekeleza kwa muda wa miaka 7 kama Askofu na miaka 23 kama Padre. Jimbo kuu la Mwanza lilikuwa wazi, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumteua Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam hapo tarehe 21 juni 2018.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, alizaliwa kunako tarehe 12 Novemba, 1965, Parokia ya Sumve, Jimbo kuu la Mwanza. Alipata masomo yake ya sekondari, Seminari ya Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma na baadaye Nyegezi, Jimbo kuu la Mwanza. Kunako Mwaka 1987 alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, kwa ajili ya masomo ya Falsafa na baadaye mwaka 1989 aliendelea na masomo ya Taalimungu Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Alipadrishwa kunako tarehe 2 Julai 1995 akiwa ni Padre wa Jimbo kuu la Mwanza.

Tangu alipopadrishwa amefanya shughuli mbali mbali za kichungaji kama Paroko msaidizi, Gombera wa Seminari ndogo ya Nyegezi, Jimbo kuu la Mwanza na baadaye kunako mwaka 2002 hadi 2005 alikwenda Roma kwa masomo ya Sheria za Kanisa, kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana na hapo akajipatia shahada ya uzamili katika sheria, kanuni na taratibu za Kanisa. Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2011 alikuwa ni Mhazini mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza. Tangu mwaka 2008 hadi 2009 alikuwa ni Makamu wa Askofu, Jimbo kuu la Mwanza. Na baadaye mwaka 2009 aliteuliwa kuwa msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Mwanza kufuatia kifo cha Askofu mkuu Athony Mayala. 

Askofu Mkuu Nkwande
10 May 2019, 15:52