Tafuta

Vatican News
Uhuru wa kuabudu na kidini ni sehemu ya haki msingi za binadamu, lakini waathirika wakuu ni Wakristo sehemu mbali mbali za dunia! Uhuru wa kuabudu na kidini ni sehemu ya haki msingi za binadamu, lakini waathirika wakuu ni Wakristo sehemu mbali mbali za dunia!  (ANSA)

Uhuru wa kuabudu & Uhuru wa kidini: Wahanga wakuu ni Wakristo!

Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Takwimu zinaonesha kwamba, wahanga wakuu wa madhulumu ya kidini ni Wakristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uhuru wa kuabudu na kidini ni nguzo ya haki msingi za binadamu; ni kiiini cha Habari Njema ya Wokovu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Uhuru wa kuabudu na kidini unaweza kusaidia kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Hii ni chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na kwamba, ukweli na uwazi ni kanuni msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kuna baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaotaka kuzima uhuru wa kuabudu au kung’oa kabisa uhuru wa kidini kutoka katika masuala ya kisiasa na matokeo yake ni kuibuka kwa kasi kubwa chuki dhidi ya imani, dhuluma na nyanyaso za kidini. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuunganisha sauti zao ili kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu; kwa kujikita katika kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wajenge madaraja ya majadiliano ya kidini kwa kuheshimiana, kwani tofauti zao msingi ni kadiri ya mapenzi ya Mungu na kamwe, zisiwe ni sababu ya chokochoko, uhasama na chuki za kidini, ambazo zimekuwa ni sababu kubwa ya maafa na majanga katika maisha ya watu wengi duniani! 

Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Wahanga wakuu wa madhulumu ya kidini ni Wakristo; kwani kuna watu ambao wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko, kuna idadi kubwa ya Wakristo wanaouwawa pengine kuliko hata ilivyokuwa kwenye Kanisa la mwanzo! Lakini, jambo la kushangaza vifo vya Wakristo hawa si habari tena!

Mauaji kwa kisingizio cha udini ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kuhakikisha kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii, vinawajibika barabara kufichua maovu haya yanayoendelea kujificha katika jamii. Ni katika muktadha wa uhuru wa kuabudu na kidini, Kardinali Vincent Gerard Nichols, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Westminster ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles kwa kushirikiana na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani, wamemwomba Bwana Philip Mounstephen, Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Uingereza, kuhakikisha kwamba, Serikali ya Uingereza inasaidia kuwalinda Wakristo wanaoteswa, kunyanyaswa na kubaguliwa sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuhakikisha kwamba, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu unalindwa na kuheshimiwa na Serikali husika kama sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu.

Hivi karibuni, Serikali ya Uingereza imezindua uchunguzi na upembuzi yakinifu mintarafu dhuluma na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Uchunguzi huu unafanyika katika kipindi cha miezi mitano ili kuangailia jinsi ya kuwasaidia waathirika wa nyanyaso na dhuluma za kidini. Uchunguzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililotolewa na Umoja wa Mataifa, lakini zaidi sana ni uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini pamoja na uhuru wa mtu kutoa mawazo yake. Taarifa ya uchunguzi na upembuzi huu itatolewa na kuchapishwa rasmi, mwezi Juni, 2019. Viongozi hawa wa kidini wanasema kuna haja ya Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mwelekeo mpana zaidi kuhusu uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu mambo ambayo yanapaswa pia kuingizwa katika sera na siasa za mambo ya nchi za nje kwa Serikali ya Uingereza.

Mambo kama misaada; ulinzi na usalama, biashara; wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa yanapaswa kubainishwa, kuingizwa na kuratibiwa barabara kama sehemu msingi ya sera na siasa ya mambo ya nchi za nje ya Uingereza. Wakristo ni sehemu muhimu sana ya mahusiano na mafungamano ya kijamii duniani, lakini wamekuwa ni wahanga wakuu wa nyanyaso na dhuluma kwa misingi ya uhuru wa kidini na kuabudu. Kuna baadhi ya waamini wa dini nyingine kama Jumuiya ya Yazidi kutoka Iraq pia wanateseka na kunyanyasika kutokana na kuongezeka kwa dhana ya ukanimungu inayofanywa na baadhi ya watu wanaotaka kutuliza dhamiri zao zinazoteseka, kwa kuengua uwepo wa Mungu katika maisha yao! Viongozi wa Makanisa wanasema, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu.

Uhuru wa Kidini: Uingereza
24 April 2019, 10:57