Tafuta

Vatican News
JUMA KUU: Alhamisi Kuu: Ekaristi takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na Huduma ya upendo inayofumbatwa katika unyenyekevu! JUMA KUU: Alhamisi Kuu: Ekaristi takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na Huduma ya upendo inayofumbatwa katika unyenyekevu!  (AFP or licensors)

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja ya Upadre na Upendo

Alhamisi kuu: Kutangazwa kwa amri ya mapendo na huduma inayomwilishwa katika unyenyekevu. Pia tunaadhimisha kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi. Yesu anawalisha mitume kwa kuwapa chakula cha mbinguni. Na jambo la tatu, Yesu anaweka Sakaramenti ya Daraja Takatifu, ili kuendeleza sadaka hii. Anampatia mwanadamu nafasi ya kuadhimisha Ekarisiti Takatifu na kutoa huduma.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Tangu zamani za kale Waisraeli walitolea sadaka za wanyama na mazao kama alama ya shukrani. Hata wakati Waisraeli walipotoka utumwani Misri ibada ya pasaka na sikukuu ya mkate isiyochachwa ikaunganishwa na kuadhimishwa sasa kama sadaka moja ya ibada ya wokovu, ikifanyika sasa kukumbuka walipotoka utumwani Misri. Tangu zama hizo hata leo bado wanadhimisha ibada hii. Wakati wa Kristo, Mwanakondoo wa Mungu amejidhabihu msalabani akajitoa kama chakula katika karamu ya mwisho katika juma la pasaka ya waisaraeli. Tunaadhimisha ibada hiyo kila mwaka katika juma kuu.

Kristo Yesu ameiletea dunia yote wokovu kwa karamu yake na msalaba wake. Kadiri ya imani yetu, tendo lile lile la karamu na msalaba linaendelezwa na Kristo katika Misa takatifu iliyo Karamu na Sadaka ile ile ya Kristo. Karamu (chakula cha) ya Bwana maana yake ni Ekaristi takatifu. Karamu hii ni ukumbusho wa karamu ya mwisho ya Bwana pamoja na mitume wake alipoweka Ekaristi Takatifu. Mapokeo fulani ya Kiyahudi yalieleza neno “Pasaka” “Pass over” kwa maana ya kuvuka, yaani kuvuka bahari ya Shamu - Kut. 14. Kristo na sisi pamoja naye tutauvuka ulimwengu huu wa dhambi na kwenda kwa Baba katika nchi ya ahadi – Kut. 21. Kristo ameshatuvusha, hivyo ni juhudi na bidii yetu kubaki pamoja naye ili tufike tuendako.

Ili tufike kwa Baba yahitajika juhudi binafsi, juhudi ya jamii inayoamini - walipo wawili au watatu kwa jina langu nami nipo kati yao. Lakini zaidi sana yahitajika neema ya Mungu ili tuweze kufika kwake. Katika adhimisho hili la Ekaristi Takatifu siku ya alhamisi kuu; Tunaadhimisha kutangazwa kwa amri ya mapendo na huduma. Mungu anaonesha unyenyekevu anaosha miguu yetu sisi wadhambi. Anatufundisha kupendana. Pia tunaadhimisha kuwekwa kwa sakramenti ya ekaristi. Yesu anawalisha mitume kwa kuwapa chakula cha mbinguni.  Na jambo la tatu, Yesu anaweka Sakaramenti ya Daraja Takatifu, lengo likiwa ni kuendeleza hicho alichofanya yeye. Anampatia mwanadamu nafasi ya kuadhimisha Ekarisiti Takatifu na kutoa huduma.

Kwa hakika Padre ni Kristo mwingine ‘Alter christus’. Katika Sala ya Ekaristi ya pili, Padre anayeadhimisha misa takatifu anasoma sala hii ‘tunakushukuru Ee Mungu kwa kutujalia kusimama mbele yako na kukutumikia’. Padre ni mtumishi wa Mungu anayetoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu. Padre ni zawadi kwa Mungu ya watu kwa Mungu – Ebr. 5:1-3. Mtakatifu Francisko wa Assisi alikuwa na heshima kubwa sana kwa padre kiasi kwamba alisema maneno haya ‘nikikutana na Malaika na padre, namsalimu kwanza Padre. Sababu aliyotoa ni kuwa Malaika ni rafiki wa Mungu ila Padre ni mhudumu wa Mungu. Hata katika Maandiko Matakatifu heshima kwa mitume (Padre) inatamkwa wazi na Yesu mwenyewe – Lk. 10:1 ‘mwenye kuwasikiliza ninyi anisikiliza mimi. Mwenye kuwakataa ninyi anikataa mimi. Na mwenye kunikataa mimi amkataa yeye aliyenituma’.

Katika somo la kwanza tunaona jinsi walivyokula mlo wa kifamilia – mlo uliliwa wakati uitwao mtakatifu katika mwaka wao – waliadhimisha maandiko ya torati na maswali yaliyoulizwa na watoto kwa baba zao yalitoa majibu ya uwepo wao na makusudio ya Mungu kwao – historia ya ukombozi wao ilirudiwa kwa watoto wa familia. Katika Injili twaona Yesu anafanya hivyo hivyo na anapoulizwa na Yohani anatoa majibu – ila alitoa maana ya mpya ya Pasaka. Katika adhimisho hilo, Yesu anaweka ukurasa mpya – anatangaza namna mpya ya kumwabudu Mungu na ulimwengu wote utapata huo uhuru na anawapa mitume uwezo wa kufanya hivyo hivyo.

Ndugu zangu, neno Ekaristi lamaanisha shukrani – hukumbusha ukombozi wa Waisraeli toka utumwani na ni shukrani kwa Mungu kwa kumkomboa mwanadamu. Hapa unatangazwa mwaka mpya na namna mpya ya kuishi na kumtukuza mwenyezi Mungu – angalia hapo juu yale mambo matatu aliyoyaweka Yesu. Ndiyo maana Mtume Paulo anawashangaza katika somo la pili kwani walikosa upendo kati yao. Badala ya kula pamoja kwa upendo wanajitenga kimakundi – mtume anasema wamepoteza imani.

Tukumbuke kuwa pasipo Ekaristi hakuna kanisa na pasipo Padre hakuna Ekaristi. Adhimisho la Ekaristi ni kumbukumbu ya ukombozi wetu na maisha ya sadaka ya mkombozi wetu. Adhmisho hili linagusa maisha yetu yote. Si historia tu ya kukumbuka bali ni historia ya kuishi. Mwinjili Luka 22:19 anasema ‘fanyeni kwa kunikumbuka mimi’. Tunapoadhimisha ekaristi takatifu tunamshukuru Mungu Baba kwa upendo wake kwetu. Katika Ekaristi wokovu wetu unakamilishwa. Tunamshukuru Mungu Baba Mwenyezi kwa upendo wake kwetu. KKK. N. 1409 tunasoma kuwa EKARISTI NI KUMBUKUMBU YA PASAKA YA KRISTO, yaani ya kazi ya wokovu iliyotekelezwa kwa maisha, kifo na ufufuko wa kristo, kazi inayofanywa iwepo kwa tendo la Kiliturujia. Tumsifu Yesu Kristo

17 April 2019, 08:58