Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu: Sherehe ya Pasaka: Kiini cha Imani ya Kanisa Tafakari ya Neno la Mungu: Sherehe ya Pasaka: Kiini cha Imani ya Kanisa 

PASAKA YA BWANA 2019: Fumbo la Pasaka, kiini cha imani ya Kanisa

Akasulubiwa pia kwa ajili yetu sisi; akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akafa, akazikwa. Akafufuka siku ya tatu ilivyoandikwa. Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Kwa njia ya mateso, kifo, ufufuko kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni, mwanadamu amekombolewa kutoka katika dhambi na mauti!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, jumapili ya Pasaka. Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana tuishangilie na tuifurahie. Ni siku ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku ya Jumapili, siku ya tatu baada ya kifo chake. Kwa Wayahudi ni siku ya kwanza ya juma. Hii ni kwasababu siku za Kiyahudi zilianza jioni na kuisha jioni. Wayahudi hawakuhesabu siku kwa kuanzia saa sita ya usiku hadi saa sita ya usiku kama nyakati zetu. Ilipofika saa ya machweo yaani jua lilipoanza kuzama siku iliisha na mara siku mpya ilianza. Yesu alizikwa siku ya Ijumaa, akashinda siku nzima, siku ya Jumamosi hadi mapambazuko ya siku ya Jumapili. Hizo ni siku tatu. Tunazihesabu tatu, siyo kadiri ya masaa 24, bali kadiri ya majina ya siku jinsi walivyohesabu wayahudi.

Kihistoria tarehe ya kuadhimisha sherehe ya Pasaka hubadilika kila mwaka. Tarehe ya Pasaka kwa makanisa ya Mashariki inatofautiana na ya makanisa ya Magharibi kwa sababu namna ya kuhesabu siku 14 za mwezi wa Nisan zinatofautiana (Katekisimu ya Kanisa Katoliki Na. 1170). Papa Viktori I, (189 – 198) aliamuru kufuata desturi ya Kirumi ya kuadhimisha Pasaka siku ya Jumapili baada ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa Kiyahudi wa Nisan ambapo huwa ni siku ya Pasaka ya Wayahudi – ‘Passover’, ili kuepuka Pasaka kuangukia katikati ya Juma. Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki huadhimisha mapema zaidi siku ya pasaka. 

Tofauti hizi ni kwa sababu, kwa makanisa ya mashariki, kalenda iliyopitishwa na Mtaguso wa Nikea wa mwaka 325, haikurekebishwa kwa kadri ya marekebisho ya mwaka 1582, yaliyofanywa na Papa Gregori VIII na hivyo ni mara chache sana siku ya Pasaka huweza kuangukia katika tarehe sawa na ile ya upande wa Magharibi. Lakini kawaida pasaka inaangukia ndani ya kipindi cha siku 35 kati ya tarehe 22 Machi na 25 Aprili, lakini siku inabaki ni siku ya kwanza ya juma yaani jumapili. Hivyo Jumapili ni siku ya kwanza ya juma, siku ya ufufuko, ni siku ya uumbaji mpya tunaporudishiwa sura na mfano wa Mungu tulioupoteza kwa dhambi ya asili. Pasaka ni sikukuu ya sikukuu, sherehe ya sherehe ni Dominika Kuu. Mtakatifu Atanasi anaiita Pasaka Dominika Kuu. Sio tena Sherehe ya Pasaka, ya Wayahudi, waliyokumbuka kutolewa kwao utumwani Misri bali ni siku ya kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na nguvu za shetani.

Kadiri ya desturi ya Wayahudi, mwili wa mtu aliyekufa akazikwa alipaswa kupakwa mafuta kwa siku tatu, baada ya kuzikwa, kwa sababu, waliamini kwamba roho ya mtu aliyekufa hubaki karibu na mwili kwa siku tatu na siku ya nne huenda kwa Mungu. Kwa sababu hiyo, waliupaka mwili mafuta kwa siku tatu. Yesu alikufa siku ya Ijumaa na hivyo alipakwa mafuta mara ya kwanza kabla ya kuzikwa. Siku iliyofuata ilikuwa ni sabato, pia ilikuwa ni sikukuu kubwa ya Pasaka ya Wayahudi, hivyo hawakumpaka Yesu mafuta, kwa sababu, siku hiyo hawakuruhusiwa kufanya kazi yeyote. Baada ya sabato ilifuata Jumapili, siku ya kwanza ya juma ambayo ndiyo siku ya tatu baada ya Yesu kufa. Wanawake walienda kuupaka mwili wa Yesu mafuta mapema asubuhi. Walikuta kaburi liko wazi, na Yesu amekwishafufuka, sasa ni mzima. Huu ni ukweli usiopingika.

Ufufuko wa Yesu Kristo ni ukweli mkuu wa imani yetu. Ndio hasa kilele na msingi wa imani yetu. Nasadiki isingekuwa na maana kama Kristo asingefufuka; kwani Fumbo la Umwilisho wa Bwana wetu Yesu Kristo kuchukua mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu mwilini mwa mama Bikira Maria, kusingekuwa na maana kwani kuchukua mimba na kuzaa kwa viumbe hai ni kitu cha kawaida. Kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo siku ya Noeli kusingekuwa na maana kwani kuzaliwa ni kawaida katika maisha yetu. Kuhubiri kusingekuwa na maana kwani hata manabii kabla yake walifanya hivyo hata sasa katika nyakati zetu bado mahubiri yanaendelea.

Kuteswa kwake kwa kupigwa mijeledi, kuvikwa taji la miiba, kutemewa mate, kutundikwa juu ya msalaba, kufa na kuzikwa kusingekuwa na maana kwani haya yalikuwepo kabla ya yeye kufanyiwa hivyo na baada yake yameendelea kufanyika. Hivyo ufufuko wake ni hitimisho ya yote haya ambayo sisi tunayaona kuwa ni ya kawaida. Ufufuko ndio hasa kilele cha fumbo la ukombozi wetu. Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ni hakika. Nasi hatupaswi kutilia mashaka. Tunazo kila sababu za kuamini na kuushuhudia. Kwanza kaburi li wazi na mwili wake haupo na ni wazi haukuibiwa maana kaburi lililindwa na askari na vitambaa alivyozungushiwa vipo vimezongwazongwa pembeni. Malaika wanashuhudia hili na Yesu mwenyewe alionekana kwa wafuasi wake, akajifunua kwao katika neno lake nao walimtambua katika kuumega makate.

Wanawake waliokwenda alfajiri kaburini kuupaka mwili wake mafuta nao wanashuhudia kuwa amefufuka naye amewatokea. Baada ya kufa Yesu wafuasi wake walijawa na woga mwingi sana, hata wakajifungia ndani wasitoke kwa hofu ya wayahudi. Kilichowapa nguvu ya kutoka kwa ujasiri na kutoa ushuhuda mbele za watu bila woga ni ufufuko. Hili linajidhihirisha wazi katika hotuba ya Petro akitoa ushuhuda wa ufufuko wa Yesu kwa ushujaa na ujasiri wa ajabu tena mbele yao Waandishi na Mafarisayo. Kama Yesu hangefufuka wanafunzi wake wangetawanyika na kanisa lisingezaliwa na kudumu kama ilivyotokea. Hivyo nasi tuwe na ujasiri wa kuishuhudia imani yetu bila woga wala mashaka.

Ufufuko ni mabadiliko kutoka utu wa kale, kwenda utu upya, kutoka maisha ya dhambi kwenda maisha ya utakatifu. Mtume Paulo katika waraka wake kwa wakolosai, anatuambia kama kweli tumefufuka tuyatafute yaliyojuu kristo aliko, tuyafikirie yaliyo juu na wala sio ya chini. Maana yake nini? Maana yake yote tuyafanyayo yalenge kutufikisha katika ufalme wa Mungu. Tuishi imani yetu ili tuzae matunda ya rohoni ambayo ni upendo, furaha, amani, mshikamamo, uvumilivu, unyenyekevu, utii na uchaji kwa Mungu (Wagalatia 5:22-23). Kwa kuwa tumefufuka pamoja naye hatupaswi kuyahangaikia matendo ya mwili yanayotutia unajisi ambayo anayataja wazi, chuki, fitina, ufisadi, ibada ya sanamu, uadui, ugomvi, kijicho, hasira, ubinafsi, utengano, mafarakano, wivu, ulevi, ulafi, ushirikina, uzinzi na uasherati tunaweza kuongezea ya nyakati zetu kama vile michepuko, ushoga, ndoa za jinsia moja, manyanyaso, dawa za kulevya, za kuzuia na kutoa mimba (Wagalatia 5:19-20). Haya ndiyo ambayo tunaambiwa na Mtume Paulo tusiyahangaikie kwani yanatutia unajisi na kutuzuia kuingia katika ufalme wa mbinguni.

Ufufuko wa Kristo ni wokovu wetu. Hakika tumekombolewa kutoka mautini na tumewekwa huru kutoka utumwa wa shetani na upotevu wa milele. Mlango wa paradisi uliofungwa kutokana na dhambi ya asili ya Adamu wa kwanza, umefunguliwa kwa kifo na ufufuko wa Adamu wa pili yaani Yesu Kristu. Pasaka kwetu ni siku ya kurejesha matumaini baada ya kuwa tumekata tamaa ya maisha kutokana na magonjwa ya mwili na roho, hali ambayo ilisababisha kujiona tumeshindikana kwa tabia zetu chafu, kujiona hatufai katika jumuiya. Pasaka ni Habari Njema kwetu kwamba Kristo Mfufuka yuko kati yetu, yupo pamoja nasi na ndani ya kila mmoja wetu. Ameshinda dhambi na kifo, nasi pia tutashirikishwa ushindi huu endapo tutamruhusu akae nasi na kama tutatelekeza yale aliyoamuru. Mkristo usikie kama bado hujaachana na chachu ya uovu na ubaya.

Katika misa ya mkesha tulirudia ahadi zetu za ubatizo kuonyesha kuwa kwa ubatizo ndio tuliunganishwa na Kristo. Kwa tendo hilo umoja wetu na Kristo mfufuka unaimarishwa kwani katika Ubatizo tulikufa na kufufuka na Kristu; tukaahidi kumfuata daima katika maisha ya taabu na raha. Yatupasa kuishi kadiri ya ahadi zetu za ubatizo. Tuushike kwa moyo wote wosia wa mtume Paulo anapotuasa tuanze maisha mapya baada ya kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tumsifu Yesu Kristo.

Pasaka: Tafakari
20 April 2019, 15:48