Tafuta

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Kristo Yesu ni kielelezo cha huruma na ufunuo wa Mungu kwa waja wake! Jumapili ya Huruma ya Mungu: Kristo Yesu ni kielelezo cha huruma na ufunuo wa Mungu kwa waja wake! 

Jumapili ya Huruma ya Mungu 2019: Imani kwa Yesu Mfufuka!

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Leo Mama Kanisa anatupa mafundisho yafuatayo; mosi ni nguvu ya imani ilivyojidhihirisha katika jumuiya ya kwanza ya wakristo, pili ni kiri kuu ya imani kuwa Yesu ni mtu kweli na Mungu kweli, tatu kuwekwa kwa sakramenti ya kitubio, na nne ni vyanzo vya mafundisho ya Kanisa na njia zinazodhihirisha uwepo wa Kristo katika maisha yetu ya kila siku.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 2 ya Pasaka. Leo Mama Kanisa anatupa mafundisho yafuatayo; mosi ni nguvu ya imani ilivyojidhihirisha katika jumuiya ya kwanza ya wakristo, pili ni kiri kuu ya imani kuwa Yesu ni mtu kweli na Mungu kweli, tatu kuwekwa kwa sakramenti ya kitubio, na nne ni vyanzo vya mafundisho ya Kanisa na njia zinazodhihirisha uwepo wa Kristo katika maisha yetu ya kila siku.

Somo la kwanza kutoka matendo ya mitume linasimulia jinsi Kristo mfufuka alivyojidhihisha kwa ishara na maajabu aliyoyafanya kwa mikono ya mitume (Mdo 5:12). Ni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Kanisa la Mwanzo, lilianza kukua na kustawi na ni kwa nguvu hiyo hiyo wakristo wa kwanza walionyesha moyo wa mapendo na ushirikiano hata watu waliwatukuza wakawa mfano wa kuigwa katika maisha ya kijumuiya. Imani yao iliwawezesha kumwona Kristo mfufuka hata katika vivuli vya Mitume (Mdo 5:15) ndiyo maana waliwaweka wagonjwa njiani ili kivuli cha mitume kikiwapitia waweze kupona. Hii ni imani kubwa mno, imani isiyo na shaka kuwa Kristo Yesu baada ya kufufuka ameendelea kuwepo katika maisha yetu kwa njia ya mitume na katika nyakati zetu anaendelea kufanya kazi ya ukombozi katika nafsi ya mapadre. Imani tu yaelewa mambo haya. Waamini wenye imani juu ya uwepo wa Kristo katika nafsi ya Padre na kuwa ndiye anayeadhimisha sakramenti katika nafsi ya Padre kama alivyofanya kwa Mitume ndio wanaonufaika na kupata baraka zake.

Somo la pili kutoka Kitabu cha Ufunuo, linasimulia maono ya Yohane akiwa katika kisiwa cha Patmo siku ya Bwana yaani Jumapili, ndiyo Domenika, siku ya ufufuko (Ufu 1:13). Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Domenika ni Siku ya Mungu; Siku ya Kristo, Siku ya Kanisa, Siku ya Binadamu na Siku ya Kutafakari kuhusu Fumbo la Kifo! Yesu anajifunua kwa Yohane akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Yesu anajidhihirisha kuwa ni Kuhani kwa ishara ya kanzu aliyovaa, Mfalme kwa mshipi wa dhahabu aliojifunga na hakimu kwa ishara ya vinara 7 vya moto. Kristo ni kweli Kuhani, mfalme na hakimu mwenye haki.

Injili imesheheni mafundisho msingi sana ya imani. Mosi imebeba ujumbe wa Kristu mfufuka, ujumbe huu ni wa amani. Amani iwe kwenu ni maneno ya kwanza ya Yesu mfufuka kwa wanafunzi wake alipowatokea. Kisha anawaambia; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Mwinjili Matayo anasema enendeni ulimwenguni mwote mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu mkiwabatiza kwa jina la Baba na la mwana na la Roho Mtakatifu (Mt. 28:18-20). Mwinjili Marko anasisitiza, fundisheni kuyashika yote niliyowaamuru ninyi aaminiye na kubatizwa ataokolewa, asiyeamini atahukumiwa. Yohane anaendelea kusisitiza; naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

Huu ni udhibitisho wa kuwekwa kwa Sakramenti ya Upatanisho, Sakramenti ya Kitubio au Ondoleo la dhambi na mamlaka waliyopewa mitume ya kuotuondolea dhambi nao wakawaridhisha mapadre. Hivyo hatunashaka juu ya mamlaka haya. Mwenye mashaka na asiyeamini atahukumiwa, bali aaminiye ataokolewa. Bwana wangu na Mungu wangu ni fundisho la kiri kuu ya imani yetu kuwa Kristo mfufuka ni mtu kweli na ni Mungu kweli ni kiri ya Tomaso. Tomaso mwanzoni aliyeshindwa kuamini kuwa Kristo amefufuka na amewatokea wenzake akisema; Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.

Yesu alipowatokea mara ya pili naye Tomaso aitwaye pacha akiwapo alimwambia; Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazama mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. Hivyo Kristo mfufuka ni mtu kweli na Mungu kweli, aaminiye juu ya kweli hii ya imani ataokolewa, asiyeamini atahukumiwa.

Vyanzo vya mafundisho ya Kanisa. Kanisa Katoliki lina vyanzo vikuu vinne vya mafundisho yake ambavyo ni Biblia Takatifu, mapokeo kutoka kwa mitume, mababa wa imani na mitaguso ya Kanisa. Biblia sio chanzo pekee cha mafundisho ya kanisa. Yohane amedhibitisha fundisho hili akisema; basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini muwe na uzima kwa jina lake. Habari ambazo Yohane anasema hazijaandikwa katika Biblia ni mafundisho mengine ya kanisa ambayo tunayapata katika mapokeo kutoka kwa mitume, mababa wa Imani na mitakuso ya Kanisa. Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya mafundisho msingi ya Kanisa ambayo hayajaandikwa katika Biblia Takatifu kwani hayo tunayapata katika vyanzo hivyo vingine.

Wakristo wa kwanza walimwona Yesu mfufuka katika vivuli vya mitume, Tomaso alipomwona ndani ya jumuiya ya mitume akasema Bwana wangu na Mungu wangu naye Yohane alipomwona, anashuhudia kuwa ndiye aliye hai yeye aliyekufa, ndiye kuhani, mfalme na hakimu. Sisi tunamuona wapi Yesu mfufuka? Tunakutana naye wapi? Yesu mfufuka sasa anaishi nasi katika maisha yetu kwa namna ambayo mifumo yetu ya fahamu haiwezi kudhihirisha. Namna ambayo haiwezi kuguswa kwa mikono au kuonekana kwa macho yetu ya kawaida. Imani pekee ndiyo yaweza kuelewa mambo haya, haonekani kwa macho lakini nguvu na neema zake bado zipo nasi daima (Mdo 1:8). Sisi tunakutana na Yesu katika sakramenti, katika Neno lake na katika makasisi wake, katika wahitaji na wenye shida kama vile maskini, wenye njaa, wanye kiu, wafungwa, walio uchi na wagonjwa kwani yeye mwenyewe anasema lolote mliowatendea miongoni mwa wadogo hawa mlinitendea mimi.

Umuhimu wa Jumuiya ya waamini. Katika Jumuiya tunakutana na Yesu mfufuka kwani yeye mwenyewe anatuambia wakutanapo wawili au watatu kwa jina langu mimi nipo katikati yao na lolote watakalo mwomba Baba kwa jina langu atawapatia. Nje ya jumuiya hatuwezi kukutana na Yesu. Ndiyo maana Tomaso alipokuwa nje ya jumuiya hakumuona Yesu, na aliporudi ndani ya jumuiya akamuona na kukiri wazi Bwana wangu na Mungu wangu. Mapadre, Sakramenti na Neno la Mungu ambamo tunakutana na Yesu ni mali ya Kanisa. Hivyo, nje ya Kanisa yaani jumuiya ya waamini hatuwezi kukutana na Yesu mfufuka. Hivyo tunahitaji jumuiya ili tukutane na Yesu. Imani tuliyonayo tumeipata kupitia kwa watu. Jumuiya ndiyo iliyoitunza na kuirithisha tunu hii ya imani vizazi baada ya vizazi. Paulo anauliza: “Wataliitiaje jina lake yeye ambaye hawamwamini? Na watamwaminije yeye ambaye hawajawahi kumsikia? Na watasikiaje kama hakuna mhubiri?” (Rom 10:14).

Tunahitaji Jumuiya ili kusikiliza mahubiri na mafundisho ya imani yanayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji! Katika jumuiya tunaombeana, tunapata mifano kutoka kwa wengine jinsi ya kuishi imani yetu katika matendo, tunapata faida ya kuonywa na kurekebisha pale tunapokuwa tumekosea. Katika jumuiya tunapata nafasi ya kupendwa na kupenda. Tunakutana na upendo wa Mungu kwa kupitia wenzetu na sisi wenyewe tunakuwa vyombo ambavyo Mungu anapitishia upendo wake uwafikie wengine. Ni katika jumuiya Kristo anakutana nasi. Jumuiya ya Wakristo wa Kwanza ni mfano wa kuigwa kwa jumuiya zetu. Wajibu wetu ni kuzifanya jumuiya zetu ziwe kweli ishara ya uwepo wa Kristo ulimwenguni. Watu wamtambue Kristo katika jumuiya zetu. Kama kuna shida yoyote katika jumuiya suluhisho si kujitenga na jumuiya bali ni kutatua matatizo hayo. Je, upo ndani ya jumuiya? Kama haupo ingia sasa, jiunge na jumuiya, jiunge na vyama vya kitume, shiriki katika shughuli za kanisa ili ukutane na Yesu Mfufuka upate neema na baraka tele.

Jumapili ya Huruma
24 April 2019, 14:26