Tafuta

Vatican News
Ijumaa kuu: Kanisa linaadhimisha: Mateso na Kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kilele cha huruma, upendo na ufunuo wa Mungu kwa binadamu! Ijumaa kuu: Kanisa linaadhimisha: Mateso na Kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kilele cha huruma, upendo na ufunuo wa Mungu kwa binadamu!  (AFP or licensors)

Juma kuu: Ijumaa Kuu: Kuabudu Msalaba & Komunio Takatifu

Kanisa linatafakari Fumbo la Msalaba kwa ukimya mkuu. Ibada ya Ijumaa Kuu inasehemu kuu tatu nazo ni Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Kupokea Komunyo Takatifu. Tukumbuke kuwa Ijumaa kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu kwa sababu ni siku ambapo Yesu mwenyewe alijitoa Sadaka Msalabani, na Jumamosi Kuu Kanisa linakaa kimya kwenye kaburi la Bwana.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, siku ya ijumaa kuu. Siku hii Kanisa linatafakari Fumbo la Msalaba kwa ukimya mkuu. Ibada ya Ijumaa Kuu inasehemu kuu tatu nazo ni Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Kupokea Komunyo Takatifu. Tukumbuke kuwa Ijumaa kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu kwa sababu ni siku ambapo Yesu mwenyewe alijitoa Sadaka Msalabani, na Jumamosi Kuu Kanisa linakaa kimya kwenye kaburi la Bwana likiyawaza-waza Mateso na kifo chake, hivyo haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu hali meza Takatifu iko tupu, mpaka zitakapoanza sherehe za Pasaka baada ya Vijilia takatifu au kesha la ufufuko. Hapo tena sherehe zitaendelea muda wa siku hamsini na kuhitimishwa kwa sikukuu ya pentekoste.

Katika liturujia ya neno mwinjili Yohane anasimulia jinsi Yesu alivyotoka na wanafunzi wake kwenda katika bustani ya mizeituni, sehemu ambayo alikuwa anaenda mara nyingi kulala. Kulala nje ilikuwa kawaida ya Marabi/Manabii na wanafunzi wao maana hawakuwa na vitanda ili waweze kusali na kutafakari matendo ya makuu ya Mungu, ndiyo maana Yesu alisema hakuwa na mahali pa kulaza kichwa chake (Mt.8:20; Lk.9:58). Yuda alipajua mahali pale. Akiwa na askari wenye taa na mienge na silaha na marungu anawaongoza mpaka hapo na kumsaliti Yesu kwao kwa busu. Yesu anakamatwa na kupelekwa katika baraza la wayahudi. Hiki kilikuwa chombo kilichokuwa na mamlaka ya juu ya kidini. Kisha anapelekwa kwa gavana wa Kirumi Pontio Pilato, naye anaamuru apelekwe kwa mkuu wa mkoa wa Galilaya, Herode Antipas kwa vile Yesu alikuwa mwenyeji wa Nazareti katika Galilaya.

Mahangaiko haya yote ni kutafuta sababu za kumwua mtu asiye na hatia. Yesu alishtakiwa kwanza kwa mashtaka ya uongo ya kidini, kwamba aliidhihaki nyumba ya Mungu akidai wangelivunja hekalu angeliweza kulijenga kwa siku tatu, pili alijiita Masiha hali alionekana hana sifa za masiha waliomgonjea, masiha wa kisiasa na tatu alikufuru kwa kujiita mwana wa Mungu. Mashtaka haya yote ni ya uongo kwani Yesu ni kweli mwana wa Mungu hata akida aliyeshuhudia kifo chake anakiri wazi hakika mtu huyu alikuwa mwana wa Mungu, pili hekalu walilolivunja alilisimamisha kwa siku tatu kwa ufufuko wake ndilo mwili wake wa utukufu. Kwa mashtaka haya ya uongo, kadiri ya sheria ya Kiyahudi Yesu alistahili adhabu ya kifo.

Lakini kwa kuwa Wayahudi walikuwa chini ya utawala wa Kirumi, haya hayakuwa makosa ya kutoa hukumu ya kifo, ndiyo maana wanatunga mashtaka mengine ya kisiasa/uhaini kuwa Yesu amejiita mfalme wa Wayahudi, wakati Wayahudi wanatawaliwa na warumi chini ya mfalme Kaisari. Pili amewakataza watu kulipa kodi kwa Kaisari. Lakini sio kweli kwani Yesu alimwambia Petro aende ziwani, samaki wa kwanza atakayemshika achukue humu shekeli akalipe kodi kwa ajili yake na yeye pia. Hata walipomuuliza kama ni halali kutoa kodi au la, jibu la Yesu lilikuwa wazi ya Kaisari mpeni kaizari na ya Mungu mpeni Mungu. Tatu kuwa alichochea Mgomo. Mashtaka haya yote ni ya uongo, ndiyo maana Yuda anasema nimekosa nilipoisaliti damu isiyo na kosa. Anarudisha vile vipande thelathini vya pesa kwa wakuu wa Makuhani.

Pilato anasema mimi sioni kosa la mtu huyu (Yn.18:38). Lakini kwa woga anamtoa auawe akisema, mimi sina hatia juu ya kifo cha mtu huyu ananawa mikono. Baada ya hukumu hii isiyo haki, Yesu alipigwa mijeledi, akavikwa taji ya miiba, akavuliwa nguo, akapigwa kwa mwanzi, akatemewa mate, akabebeshwa Msalaba, alipofika Golgota akasulubiwa msalabani, akafa, nchi ikatetemeka, jua likafifia, kukawa na giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, naye askari mmoja wapo akamtoboa ubavu kwa mkuki na mara ikatoka damu na maji ndizo chemchemi za Sakramenti za Kanisa. Mwinjili Yohane anatuambia, umati wa watu walipiga makelele, wakisema mwondoshe, mwondoshe, asulubishwe, asulubishwe.

Sisi nasi hatuko kinyume na hawa waliopiga makelele asulubishwe, asulubishwe, kwetu sisi kwa mawazo yetu, maneno yetu, matendo yetu maovu, tunatoa mlio na makelele hayo hayo tukisema mwondoshe, mwondoshe, asulubishwe, asulubishwe. Petro anajaribu kupambana na nguvu za giza kwa upanga. Kristo anapambana na kumshinda shetani si kwa mapanga na vitisho bali kwa uvumilivu wake, unyenyekevu wake, upole na utii wake kwa Mungu Baba. Je sisi leo wanakanisa wakristo wakatoliki hatuna fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za shetani kwa nguvu za giza, pesa, mapigano, visasi na fitina?

Tukumbuke ufalme wa Kristo si wa Dunia hii hivyo tunapaswa kumpigania kwa ushuhuda wa maisha yetu kwani yeye anatuambia mkipendana watu watawatambua kuwa mu wanafunzi wangu. Petro anamkana Yesu mara tatu akisema mimi si mfuasi wa Yesu, akasisitiza na kusema mimi simjui mtu huyu. Sisi nasi tunafanya jambo hili la kumkana Yesu katika maisha yetu pale tunapoionea aibu Injili, na kuamua kujiingiza katika maisha ya dhambi, maisha ya kumchukiza Mungu; jogoo amekwisha wika mara ya tatu, tunaalikwa kujirudi na kulia kama Petro. Tujiweke chini ya msalaba kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu sisi ni nguvu ya Mungu, tuutazame sasa msalaba kwa imani kuu na moyo wa toba.

SEHEMU YA PILI YA IBADA YA KUABUDU MSALABA: Wakristo Wakatoliki tunashitakiwa kuwa tunaabudu sanamu. Je, kwetu sisi msalaba ni nini, una maana gani katika maisha yetu? Maana finyu ya msalaba ni vipande viwili vya miti vilivyounganishwa kimoja cha wima-kirefu na cha pili cha ulalo-kifupi. Asili ya msalaba ni Warumi, lengo ni kutoa adhabu kwa wahalifu na fundisho kwa watu wengine kutofanya uhalifu. Mtu aliyepatikana na makosa ya wizi, ujangili, ujambazi, uhaini au uasi licha ya mateso mengine, alisulibiwa msalabani na kuachwa hapo mpaka afe. Kwa hiyo, msalaba ulitumika kama chombo cha kukomesha tabia mbaya katika jamii.

Maandiko Matakatifu pia yanasema, “Ikiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, nawe ukamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utauzika siku hiyohiyo. Kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; asije akatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana Mungu wako, iwe urithi wako (Kum.21:22-23). Sisi tulistahili kutundikwa msalabani kwa makosa na dhambi tulizomkosea Mungu. Lakini, Kristo kwa upendo na hiari yake aliyachukua makosa yetu na adhabu tuliyostahili mwilini mwake. Badala ya kuteswa sisi akateswa yeye, badala ya kusulibiwa sisi akasulibiwa yeye na badala ya kufa sisi kwa dhambi zetu akafa yeye.

Maana Pana zaidi: Msalaba ni bendera na bango la ushindi. Yesu ametukomboa kwa kutumia Msalaba. Msalaba ni alama ya upendo, Yn.3:14-18 ni alama ya maisha ya kila siku ya mkristo, Mk.8:34. Msalaba ni alama ya umoja na ufuasi wa kweli wa Yesu Kristo (Mk 8: 34). Msalaba ni chombo cha Ukombozi wa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Msalaba ni sadaka ya Yesu, zao la upendo (Yn 13:1). Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, “Msalaba siyo ishara ya kifo, bali uzima; siyo ishara ya jambo la kuvunja moyo, bali matumaini; siyo ishara ya kushindwa, bali ya ushindi”. Msalaba sasa si tena alama ya adhabu bali ya wokovu ndiyo maana Katika sala zetu na ibada zetu tunatumia ishara ya Msalaba, wengine tumeweka misalaba majumbani na wengine tunavaa misalaba shingoni. Lakini yawezakuwa ni mazoea tu.

Tutafakari na kujua basi maana na wajibu tunaokabiliwa nao ambao umefichwa katika ishara hiyo ya Msalaba. Kifo cha Kristo Msalabani kitukumbushe kuwa inatupasa kuona fahari juu ya msalaba kama anavyotuambia Mtume wa Kimataifa mtakatifu Paulo, “Lakini mimi hasha, nisione fahari ya kitu chochote ila msalaba wa Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu ulisulubishwa kwangu na mimi na ulimwengu” Gal. 6:14. Msalaba ni muhuri na kitambulisho cha mkristo. Hivyo hatuna sababu ya kuwa na shaka yoyote juu ya Ibada ya siku hii ya ijumaa kuu. Tunachokiabudu ni Wokovu ambaye ni Yesu Kristo Msalabani. Lugha ya mkato inayotumika yaani kuabudu Msalaba, haijitoshelezi kamwe kwa yenyewe, kutokana na upeo mdogo wa ufahamu wetu wa kulielewa hili fumbo la Msalaba kwa undani wake na kuyafahamu matendo makuu ya Mungu kwa akili zetu.

Tunachokiabudu kinatangazwa kwenye mwito unaotolewa mda mfupi kabla ya Ibada yenyewe kwa kurudiwa mara tatu, ukitualika kujongea mbele kwenye Msalaba na kumwabudu Wokovu. Mwaliko huu unasema “huu ndio mti wa Msalaba ambao wokovu wa dunia umetundikwa juu yake, njoni, njoni, njoni tuuabudu”. Kumbe katika tendo hili la kuabudu Msalaba, tunafanya tendo la nje la kuuheshimu mti wa msalaba na kumwabudu Wokovu ndiye Kristo Yesu, nafsi ya Pili ya Utatu Mtakatifu, na ni Mungu halisi aliye juu ya mti wa msalaba naye anayestahili kuabudiwa. Tunapaswa kuliadhimisha tendo hilo kwa ibada, uchaji na unyenyekevu kwa sadaka hii kamilifu aliyoitoa Yesu msalabani.

Mkristo anayeshindwa kuuona Wokovu juu ya Msalaba kwa macho ya Imani, ni aheri asijongee mbele kumwabudu, kwani hatafaidika na chochote, hatajipatia neema na Baraka zozote. Na mwenye macho ya kiimani aukaribie msalaba, kwa unyenyekevu, utulivu, hekima, majuto, toba, ibada na uchaji akiwa na moyo wa sala ya kumshukuru, kumuomba na kumwabudu Mungu wetu Katika nafsi ya pili, Yesu Kristo Mkombozi wetu. Tumpelekee shida na taabu zetu zote wala tusiogope, yupo kwa ajili yetu. Tumtazame kwa imani tumwombe msamaha kwa mateso tuliyomtesa. Huyo ndiye tutakayemwinamia na kumbusu sana, sio kwa busu la kusaliti kama la Yuda bali busu la shukrani. Mwisho tutampokea katika Komunyo Takatifu, kisha tunamaliza ibada hii ya ijumaa kuu kimya kimya tukitafahari fumbo hili la kifo cha msalaba cha Bwana wetu Yesu Kristo.

Ijumaa kuu 2019
18 April 2019, 17:00