Tafuta

Fumbo la Pasaka: Kiini cha imani ya Kanisa inayofumbatwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Baada ya kifo, kuna Ufufuko wa wafu! Fumbo la Pasaka: Kiini cha imani ya Kanisa inayofumbatwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Baada ya kifo, kuna Ufufuko wa wafu! 

PASAKA YA BWANA 2019: Fumbo la Pasaka: Ushuhuda wa wanawake!

Mama Kanisa anafundisha kwamba, Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kanisa katika Kristo. Hii ni imani ambayo Wakristo wa Kanisa la mwanzo waliusadiki na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao kama kiini cha ukweli. Wakauendeleza kwa Mapokeo na kuuthibitisha kwa Maandiko Matakatifu na Kuhubiri kama sehemu muhimu ya Fumbo la Pasaka.

Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB, - Vatican.

Jumatatu ya Juma kuu la Mwaka 2019, katikati ya jiji kuu la Parisi (Ufaransa) kulitokea janga kuu la millenia lililotetemesha Kanisa Katoliki na ulimwengu mzima  hasa Ulaya na Amerika. Watu waliokuwa karibu na tukio walipigwa butwaa na kutetemeka wakitikisha vichwa, ikiwa ni pamoja na akina mama waliolia sana kwa uchungu. Janga hilo ni la moto mkali ulioteketeza kanisa la kihistoria la Notre Dame. Kanisa hilo lilijengwa miaka mia nane iliyopita yaani karne ya kumi na saba na kuwekwa chini ya ulinzi wa Mama wa Mungu na Mama yetu Maria. Kanisa hili ni ishara kwa Ukristo na alama ya chanzo cha Ustaarabu na Maendeleo yaliyofikiwa Ulaya.

Mathalani tendo kuu la utawala wa Ulaya lililofanyika ndani ya kanisa hilo ni la kujivisha taji la kifalme Bwana Napoleon 1804 na kumvisha mke wake Josephine taji la umalkia tendo lilitotakiwa lifanywe na Baba Mtakatifu tu kadiri ya taratibu ya wakati huo. Moto huo umeteketeza vitu vingi vya kihistoria isipokuwa alama takatifu za kihistoria. Kama vile Sakramenti Takatifu, Kinanda kikuu cha kuendesha LiturUjia kwani yapata mwezi mmoja kabla yake Zilihamishwa sanamu kumi za mitume, sanamu ya Mama Maria pamoja na taji la miiba alilovishwa Yesu kutoka humo Kanisani na kupelekwa kwa sonara ili visafishwe. Kumebaki pia bila kuguswa wala kuyumba Msalaba mkubwa ulioko mbele ya Kanisa ulioandikwa maneno yafuatayo chini yake: “stat crux dum volvitur orbis” Msalaba unabaki (umesimama) imara pindi ulimwengu unazunguka.”

Watu wengi wamefikirishwa na kujiuliza maswali mengi sana yasiyo na majibu kuhusu janga hili: Kulikoni, litokee wiki kuu? Kulikoni Kanisa la Mama yetu liunguzwe moto wakati huu ambapo Mama Kanisa kijumla anaunguzwa na kulaumiwa na ulimwengu kutokana na makwazo ya wahudumu wake? Je, yawezekana baada ya kihoro hiki tukatulizika na kapata tena amani na furaha katika Kristo mfufuka? Baada ya kuona Kanisa limegeuka kuwa majivu, Je, tunaweza kuwa tena na tumaini la ufufuko! Hii ndiyo changamoto ya imani katika Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!

Natumaini maswali kama haya yaliulizwa pia na akina mama siku ya Ijumaa kuu waliposimama chini ya Msalaba wakimwangalia Yesu anavyoteseka hadi kukata roho. Kadhalika baada ya maziko ya Yesu, mitume na wafuasi wachache wakiwa pamoja na akina mama walijificha chumbani wakiwa na msongo mzito wa mawazo walijihoji maswali mengi sana juu ya Bwana wao. Kumbe katika kipindi hicho wamama waliompenda sana Yesu walijihoji kwa namna tofauti kabisa na wanaume. Ndiyo maana ilipofika siku ya tatu (Jumapili) asubuhi: “uzalendo ukawashinda.” Wakaondoka mbio kwenda makaburini. Waliporudi kutoka huko walikuwa wamebadilika. Walikuwa wamejawa furaha na muhamasiko mkubwa hata wa kuwaeleza mitume yaliyojiri utadhani waliambiwa: “Kanitangaze.” Kulikoni? Wanawake hawa wamebadilikaje kutoka hali ya simanzi na majonzi hadi kujawa matumaini na furaha ya kuitangaza? Wamepitia hatua zipi hadi wafike hapo?

Ndugu yangu, msafara wa maisha ya wanawake umesheheni hazina ya imani ya maisha hapa duniani. Ukiwafuatilia kwa dhati msafara wawamama wale utayaona maisha yako yote utakuza imani yako pindi unapokumbwa na kihoro cha aina yoyote ile, kama hiki cha moto ulioteketeza kanisa la Mama yetu (Notre Dame). Tulione kwanza jopo la wanawake walioenda makaburini: “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili walikwenda kulitazama kaburi.” (Mt. 28:1). Wa kwanza ni Mariamu Magdalene halafu Mariamu wa pili. Huyu Mariamu wa pili ni yule mke wa mzee Zebedo, mama wa mitume Yakobo na Yohane anayetajwa na Mwinjili Marko kisha anamwongeza mwanamke wa tatu Salome “Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalena na Mariamu mama Yakobo, na Salome”.

Injili ya Luka inaongeza mwanamke wa nne aitwaye Yoana: “Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine waliokuwa pamoja nao”. Yoana huyu ndiye mke wa Chusa aliyekuwa mjumbe wa Herode. Kwa hiyo kulikuwa na idadi ya wanawake wanne walioenda kaburini asubuhi ile yaani: Mariamu Magdalena, Maria mama ya Yakobo na Yohane halafu Salome na Yoana. Kadiri ya fasuli ifuatayo ya Injili tunaweza kuugawa msafara wa wanawake hawa katika hatua nne: “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akaliviringisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi” (Lk. 28:1-4)   

Hatua ya kwanza ni muda: Asubuhi na mapema, siku ya kwanza ya Juma!: Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma”. Wamama hawa walijihimu asubuhi na mapema. Neno la Kigiriki kwa asubuhi lililotumika hapa ni: “te epiphoskouse” kulipoanza kupambazuka. Bado giza, ila kuna matumaini ya kukaribia kucha. Mwinjili Marko anasema: “Alfajiri mapema” yaani asubuhi sana bado kupambazuka. Luka anasema: “Ilikuwa asubuhi sana” kwa Kigiriki “orthrou batheos” kulipoanza kupambazuka, yaani ni asubuhi lakini bado giza. Mwinjili Yohane anasema waziwazi ni “Asubuhi mapema kungali giza bado.” Kwa vyovyote wanawake hawa wanaanza safari yao kulipokuwa bado giza ila siyo giza la usiku kati, bali kunakaribia kupambazuka ila hatuambiwi ni saa ngapi. Giza hilo la asubuhi ni la matumaini ya kusubiri mapambazuko na la kuona mwanga wa jua. Muda huo ni ishara ya kutokukata tamaa katika maisha.

Hatua ya pili: Mtetemeko wa ardhi, hapo ikawa ni patashika nguo kuchanika!: Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi.” Yaonekana mtetemeko ule haukusababisha majanga, na kuwafadhaisha wamama wale vinginevyo wangeachana njia kama wanaokimbia nyuki. Kulikoni? Mtetemeko ule ulikuwa kama ule wa mtu anayetikisa kikapu cha mahindi ili yakae sawasawa kikapuni au kama kurukaruka kwa lori kwenye mabonde na kufanya abiria na mizigo ijipange vizuri. Kwa hiyo mtetemeko ulikuwa ni nguvu za Mungu aliyeamua kuutikisa kidogo ulimwengu ili kufungua milango mipya na mitazamo mipya ya mambo. Sanasana alitaka kulipangua jiwe lililomfungia Bwana kaburini. Mtetemeko ule uliyafungua makaburi ya vionjo, ya fikra za kiroho na za kiakili za wale wanawake. 

Kwa vyovyote mtetemeko ule ulitisha na ulisaidia kuwaweka sawa wanawake wale na kuwafanya wafikiri kwa undani zaidi juu ya kifo cha Yesu na hatima yake. Ndugu zangu budi ieleweke pia kwamba hadi kufikia hatua hii, wanawake hawa hawakuwa wameona wala kusikia chochote kinachohusu ufufuko. Wako gizani bado hakujapambazuka. Kadhalika hata kwetu sisi binadamu, tunapata pia mitetemeko na misukosuko inayoyumbisha misimamo ya maisha yetu. “Siyo bure” hizo ni ishara za nyakati kutoka kwa Mungu tunazotakiwa kuzifanyia kazi katika maisha.

Hatua ya tatu: Kukutana na malaika.: Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni mpatazame mahali alipolazwa.” Wamama hawa wakiwa bado gizani (hakujapambazukz) halafu wameshuhudia mtetemeko na wanashangaa wanapowaona askari walinzi wa kaburi wanaogopa. Wakiwa wanashangaa, anatokea malaika anawaambia: “Msiogope.” Uwepo wa malaika na tamko alitoalo ni ushahidi unaojitosheleza wa kukua kwa imani yao na kuacha wasiwasi. Maneno ya malaika siyo ndoto za mchana, bali ni kauli ya Yesu mwenyewe aliyeahidi. Kwa hiyo, “Ahadi ni deni.” Kitendo alichokifanya malaika ni kuwakumbusha tu wanawake wale ahadi aliyoitoa Bwana wao alipokuwa hai aliposema: “Baada ya siku tatu nitafufuka.”

Kwa hiyo sasa Malaika anawataka wanawake wale watafakari maneno ya Yesu na kufikia ukweli wa alichowaahidi. Malaika anaendelea hata kuwabainishia kwa vielelezo. Anawaonesha kithibiti cha wazi kabisa au alama iliyo mbele yao yaani kaburi wazi anapowaambia: “Njoni mpatazame mahali alipolazwa.” Hapa malaika anawataka wanawake wale wawe na akili ya kuunganisha mambo. Yaani kuunganisha maneno ya ahadi aliyotoa Yesu na kaburi wazi wanaloliona mbele yao. Kwa kufanya hivyo tu ndipo utakapoona jinsi mambo yanavyojikoki yenyewe na kudhihirika zaidi. Kumbe malaika anawapata wanawake hawa somo la hesabu za kuunganisha mambo katika maisha.

Kwamba unaweza tu kufunguka akili zako ukiunganisha Neno la Mungu (tangazo la malaika au mahubiri) ukijumlisha na mang’amuzi ya ishara zitokeazo katika maisha ya kawaida unayoyaona na kuyapitia (kaburi wazi) hapo tu ndipo utakapokomaa kiimani. Tujifunze kwa wanawake kulitafakari kukumbuka ahadi ya Neno la Mungu na kuunganisha na majanga yanayotokea katika maisha yetu. Kwa maneno mengine, tuunganishe Neno lake au Injili yake (mafundisho ya imani) pamoja na kusoma ishara za nyakatiyaani alama za upendo na za baraka ya Mungu (kaburi wazi) apo imani yako itaimarika zaidi na wasiwasi na woga wa maisha vitapungua.

Hatua ya nne: kutangaza na kueneza habari Njema ya Wokovu kwa ushuhuda: Malaika anawaagiza: “Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya nimekwisha waambia.” Baada ya kusikia maelekezo juu ya Fumbo la Pasaka na kufunguka imani yao kidogo, sasa wanatumwa na Malaika kwenda kuwatangazia wengine. Mtume Paulo anasema: “Imani inakuja kwa kuisikia.” Tunapata imani kutoka kwa Mungu kwa njia ya kanisa na maandiko matakatifu yaliyohakikiwa na Kanisa. Kwa hiyo unaagizwa usiende na kubuni tu mambo. Halafu malaika anawasisitizia: “Haya nimekwisha waambia.” Malaika hakuibuni habari ile, bali ni imani ya kweli itokayo kwa Mungu.Kwa lugha ya leo wangesema: “message sent na mjumbe hauawi!”. “Wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”

Hadi hapa “ujuzi au elimu” ya wanawake hawa kuhusu ufufuko imetegemea walichokisema wengine yaani wamefundishwa na Malaika. Kwa hiyo wanawake hawa wanayatambua zaidi mambo baada ya kuunganisha ishara za nyakati (mtetemeko wa ardhi) na maneno (ahadi ya malaika) na mang’amuzi yao baada ya kuona ishara nyingine ya kaburi wazi. Wanawake hawa walimsikia malaika kwamba Yesu amefufuka, na wakayapokea mafundisho hayo kwa furaha, lakini walipokuwa njiani katika msafara au hija ya maisha yao wakienda kutangaza habari Yesu, wakakutana uso kwa uso na Bwana Yesu mwenyewe aliyefufuka. “Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu!”

Hapo ndipo ukweli waliofundishwa na kuhabarishwa na malaika ukaimarika zaidi ndani mwao na ukageuka kuwa sehemu ya maisha yao. Wanawake hawa wametoka kwenye kufundishwa na kuibukia kuwa na mang’amuzi binafsi. Kuanzia sasa  hawataongea tu kile walichokisikia kutoka kwa wengine bali jinsi wanavyoonja wenyewe kutokana na mang’amuzi ya maisha yao. Kwa hiyo katika imani yetu hatua ya kwanza na muhimu sana ni ile ya kufundishwa au kutangaziwa ukweli wa Injili na kutumwa kwenda kuwatangazia wengine. Jambo la pili, tunaalikwa na Bwana kuuzamisha ndani zaidi ukweli huo kwa njia ya mang’amuzi binafsi. Kumbe katika kuwafundisha wengine juu ya Kristu wewe mwenyewe unajifunza na kujua mambo zaidi kuliko wakati ule ulipokuwa mwanafunzi, kwani unaimarika zaidi katika imani ya kumjua na kukutana na Yesu.

Tendo la kufundisha na la kushuhudia linatufanya tukue zaidi katika imani. Ndugu zangu tuwashukuru wanawake hawa kwani hija yao imetuingiza moja kwa moja “katika chumba cha maabara ya maisha yako. Ujitathmini kwa kupitia mang’amuzi yako binafsi ukiyaunganisha na ukweli unaofundishwa na Kanisa na Maandiko Matakatifu ukafikie hatua ya kusema: Kwa njia ya Neno na mafundisho yako ninaweza kutafsiri vihoro na machungu ya maisha. Ninayo furaha yako Yesu Mfufuka. Ninakushuhudia (kukuhubiri) kwa sababu mimi mwenyewe nimekung’amua katika maisha yangu. Kumbe unaishi kweli na anayabadili maisha yangu.” Bwana amefufuka kweli, Alleluya.

 

20 April 2019, 16:54